1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yapiga marufuku tovuti ya YouTube

28 Machi 2014

Uturuki imepiga marufuku tovuti ya jamii ya kuchangia picha za video, YouTube baada ya kutumika kusambaza kanda za sauti zilizovujishwa ambazo zinaathari kubwa kwa taifa hilo baada ya mkutano wa usalama wa taifa

https://p.dw.com/p/1BXdh
Türkei Premierminister Erdogan Präsident Gül
Waziri mkuu Erdogan(shoto) na rais Abdullah Gül(kulia)Picha: AFP/Getty Images

Sauti hizo zimepatikana kutokana na mkutano ambao ulikuwa ukijadili kuhusu uwezekano wa hatua za kijeshi dhidi ya Syria.

Mwishoni mwa juma lililopita nchi hiyo pia ilipiga marufuku mtandao mwingine wa kijamii wa Twitter, hatua ambayo imezusha shutuma kali kimataifa, baada ya huduma hiyo kutumika kusambaza kanda nyingine zinazomhusisha waziri mkuu wa nchi hiyo Recep Tayyip Erdogan na washirika wake katika rushwa.

Erdogan auf Wahlkampftour
Waziri mkuu Erdogan katika mkutano wa kampeniPicha: Reuters

Sauti zilizorekodiwa zinasadikiwa kuwa ni za viongozi waandamizi wa serikali ya Uturuki, jeshi na maafisa wa idara ya ujasusi wakijadiliana mipango ya kuanzisha mapambano ya silaha ndani ya Syria ama mashambulio ya makombora ambayo yatakuwa kama kisingizio kwa ajili ya kujibu kijeshi iwapo Syria itafanya mashambulizi ya kulipiza .

Waziri mkuu na changamoto kadha

Waziri mkuu Recep Tayyip Erdogan , ambaye tayari amehusishwa katika kashfa ya rushwa na amekabiliana na maandamano ya umma hivi karibuni kabla ya uchaguzi muhimu wa serikali za mitaa utakaofanyika siku ya jumapili, amewashutumu vikali wapinzani wake.

"Wamevujisha kitu katika tovuti ya YouTube;" Erdogan ameuambia mkutano wa kampeni kusini mashariki mwa jimbo la Diyarbakar. Ulikuwa mkutano kuhusu usalama wa taifa letu. Ni kitendo cha , kuchukiza, cha kiuwoga, na kinyume na utu. Tutakwenda katika mapango yao. Mnasaidia maslahi ya nani kwa kufanya udukuzi? Ameuliza Erdogan.

Erdogan hakuwataja mahasimu wake kwa majina, lakini hapo zamani alitumia neno "pango" akimaanisha washirika wake wa zamani ambao wamegeuka kuwa mahasimu, kiongozi wa kidini ambaye anaishi sasa nchini Marekani Fethullah Gulen, ambaye harakati zake zina wafuasi wengi katika jeshi la polisi na mahakama nchini Uturuki.

Türkei Istanbul CHP Kundgebung Anti Korruptionsproteste
Maandamano dhidi ya rushwa mjini IstanbulPicha: Ozan Kose/AFP/Getty Images

Waziri mkuu huyo wiki iliyopita alipiga marufuku mtandao wa kijamii wa Twitter, hatua iliyozusha shutuma kali kimataifa, baada ya huduma hiyo ya jamii kutumiwa kusambaza kanda zenye sauti zikimhusisha Erdogan na watu wake wa karibu katika kashfa ya rushwa.

Mahakama mjini Ankara siku ya Jumatano ilibadilisha amri hiyo kwa kusema ni inaweka mipaka dhidi ya uhuru wa kutoa mawazo. Shirika linalosimamia mawasiliano nchini Uturuki la TIB lina siku 30 kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo, na ukurasa wa Twitter bado haujarejesha huduma zake, licha ya kuwa marufuku hiyo kwa kiasi kikubwa imeepukwa.

Erdogan alaumiwa

Uturuki ambayo ni mwanachama wa NATO imeshutumiwa na wanachama wenzake wa jumuiya ya NATO na mshirika wake mkuu Marekani kutokana na hatua hiyo ya marufuku dhidi ya YouTube.

"Hii ni hatua nyingine ya kutapatapa na inayokatisha tamaa nchini Uturuki," ameandika katika ukurasa wa Twitter makamu wa rais wa halmashauri ysa Ulaya Neelie Kroes.

Türkei Twitter Sperrung 21.03.2014 Istanbul
Tovuti ya Twitter ikionekana imefungwaPicha: Bulent Kilic/AFP/Getty Images

Naibu msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani Marie Harf amesema Marekani imekuwa ikitoa matamshi mazito kwa maafisa wa Uturuki kuwa wanahitaji kuacha kufanya hivyo."

Uvujaji katika mtandao wa YouTube jana Alhamis ni wa kwanza kulenga usalama wa taifa. Waziri wa mambo ya kigeni wa Uturuki Ahmet Davutoglu amekuita, "tangazo la vita dhidi ya serikali na taifa la Uturuki", wakati wizara yake imesema baadhi ya sehemu zimetiwa chunvi.

Shrika linalodhibiti masuala ya mawasiliano nchini Uturuki TIB limesema linazuwia YouTube kwa misingi ya "kitisho cha msingi dhidi ya usalama wa taifa," kimeripoti kituo cha televisheni cha binafsi cha NTV.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri.Daniel Gakuba