1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yatishia kuiwekea vikwazo Urusi

8 Desemba 2015

Vita vya maneno kati ya Uturuki na Urusi vinazidi kushika kasi, baada ya Uturuki kuelezea uwezekano wa kuchukua hatua dhidi ya Urusi na kusema kwamba itaweka vikwazo iwapo itahitajika kufanya hivyo.

https://p.dw.com/p/1HJKD
Waziri Mkuu wa Uturuki, Ahmet Davutoglu
Waziri Mkuu wa Uturuki, Ahmet DavutogluPicha: Getty Images/AFP/A. Altan

Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu wa Uturuki, Ahmet Davutoglu wakati akizungumza bungeni na wabunge wa chama chake kinachotawala cha AK. Hata hivyo, ameongeza kusema nchi yake itaendelea kuacha milango wazi kwa ajili ya mazungumzo na Urusi.

Urusi imeweka vikwazo kadhaa vya kiuchumi dhidi ya Uturuki, baada ya Uturuki kuidungua ndege ya kivita ya Urusi karibu na mpaka na Syria na Uturuki, mwezi uliopita, kutokana na Uturuki kudai kuwa ndege hiyo ilipuuza onyo lililotolewa mara kadhaa la ndege hiyo kuvuka mpaka na kuingia katika anga yake.

Hata hivyo, Urusi ambayo imeyakanusha madai hayo, imelijibu shambulizi la Uturuki kwa kupeleka mfumo wa kuweka ulinzi angani kukinga makombora ya masafa marefu katika kambi yake nchini Syria.

Aidha, Davutoglu amesema anataka kuzuru Iraq, haraka iwezekanavyo kujaribu kutuliza mzozo kuhusu hatua ya Uturuki kuwapeleka wanajeshi wake nchini Iraq kuwapatia mafunzo wenzao katika mapambano dhidi ya kundi lenye itikadi kali la Dola la Kiislamu-IS.

Davutoglu amwandikia barua mwenzake wa Iraq

''Nimemwandikia barua Waziri Mkuu wa Iraq, Haidar Abadi. Nina matumaini Waziri wa Ulinzi wa Iraq atazuru Uturuki hivi karibuni na mimi nitazuru Baghdad kwa ajili ya mkutano wa ngazi ya juu utakaozungumzia mashauriano. Nataka kuwaeleza watu wa Iraq kwamba siku zote tutawasaidia kupambana na ugaidi. Wairaqi wote ni ndugu zetu,'' alifafanua Davutoglu.

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan na Rais wa Urusi, Vladmir Putin
Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan na Rais wa Urusi, Vladmir PutinPicha: picture alliance/ZUMA Press

Uturuki imetangaza kusitisha kupeleka wanajeshi wake kaskazini mwa Iraq kwa sasa, lakini haitawaondoa wanajeshi ambao tayari wako huko na imesema wanajeshi hao ni sehemu ya kikosi cha kuwapatia mafunzo na kuwapa vifaa wanajeshi wa Iraq.

Serikali ya Iraq imesema haijawahi kukialika kikosi kama hicho na italiwasilisha suala hilo katika Umoja wa Mataifa, iwapo hawatoondolewa. Davutoglu amesema zaidi ya watu 2,000 wamepatiwa mafunzo katika kambi hiyo ya kaskazini mwa Iraq.

Ama kwa upande mwingine Uturuki imesisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa ''maeneo salama'' kaskazini mwa Syria na kutekeleza haraka mapendekezo ya kutoa mafunzo na kuwapatia vifaa waasi wenye msimamo wa wastani. Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, wakati akizungumza na maafisa kutoka maeneo ya jirani kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Ankara.

Wakati huo huo, mwanadiplomasia mmoja katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, amesema Urusi ina mpango wa kuzungumzia vitendo vya kijeshi vinavyofanywa na Uturuki nchini Syria na Iraq, katika mkutano wa baraza hilo unaofanyika Jumanne (08.12.2015). Akizungumza kwa masharti ya kutotajwa jina, mwanadiplomasia huyo amesema Urusi haijatoa maelezo zaidi ya kile itakachokizungumza katika mkutano huo wa siri.

wandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,APE,AFPE
Mhariri:Yusuf Saumu