1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUturuki

Uturuki yawaandama PKK kufuatia mashambulizi Ankara

Mohammed Khelef
2 Oktoba 2023

Uturuki inasema imewauwa wapiganaji kadhaa wa kundi la Kikurdi la PKK baada ya kuyasambaratisha maghala ya silaha na maficho yao, saa kadhaa baada ya kundi hilo kubeba dhamana ya mripuko wa bomu mjini Ankara.

https://p.dw.com/p/4X2k6
Türkei | Ankara | Anschlag in der Nähe des Innenministeriums
Picha: Cagla Gurdogan/REUTERS

Taarifa iliyotolewa siku ya Jumatatu (Oktoba 2) na wizara ya ulinzi ya Uturuki ilisema wapiganaji wengi wa kundi lililohusika na mripuko wa jijini Ankara wameuawa wakati maeneo yao 20 yalipoharibiwa kwa mashambulizi ya anga, yakiwemo mapango, mahandaki, makaazi na maghala ya silaha. 

Soma zaidi: Mashambulizi ya Uturuki Kurdistan yaikasirisha Iraq

Operesheni hiyo ya jeshi la Uturuki ilifanyika kwenye mikoa ya  Metina, Hakurk, Qandil na Gara iliyoko kaskazini mwa Iraq majira ya saa 3:00 usiku wa Jumapili (Oktoba 1), kwa mujibu wa wizara hiyo ya ulinzi iliyosema pia hatua za tahadhari zilichukuliwa kuepuka madhara kwa raia wa kawaida na mazingira. 

Mashambulizi ya Ankara

Mapema asubuhi ya Jumapili, picha za kamera za usalama zilionesha gari moja likiingia hadi kwenye lango la wizara ya mambo ya ndani ya Uturuki na mmoja wa waliokuwamo akielekea haraka kwenye jengo la wizara hiyo kabla hajafunikwa na mripuko mkubwa. 

Türkei Innenminister Ali Yerlikaya
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Uturuki, Ali Yerlikaya, akizungumza na waandishi wa habari baada ya mashambulizi ya Ankara.Picha: Cagla Gurdogan/REUTERS

Kwa mujibu wa wizara ya ulinzi, mshambuliaji huyo alikufa hapo hapo kwa mripuko huo, na mwenzake aliuawa na vyombo vya usalama.  

Soma zaidi: Uturuki kuwashambulia waasi wa Kikurdi nchini Syria

Kundi lililodai kuhusika na mashambulizi hayo ni Chama cha Wafanyakazi wa Kikurdi, PKK, ambacho Uturuki inakitambua kama kundi la magaidi.

Mripuko huo uliolitikisa eneo lote hilo lenye majengo kadhaa ya serikali pamoja na bunge, ambalo lilikuwa ndio linaanza vikao vyake, lilikuwa shambulizi la kwanza la aina hiyo mjini Ankara tangu mwaka 2016 pale mashambulizi ya mara kwa mara yalipouandama mji huo mkuu. 

PKK yabeba dhamana ya mashambulizi

Mashambulizi ya wakati huo yalikuwa yakihusishwa na ama PKK, kundi lijiitalo Dola la Kiislamu au makundi mengine yanayopingana na Uturuki.

Irak PKK-Guerillakämpfer
Wapiganaji wa kundi la PKK kaskazini mwa Iraq.Picha: Yann Renoult/Wostok Press/Maxppp/dpa/picture alliance

Mtandao wa ANF News, ambao upo karibu na kundi la PKK, uliwanukuu wasemaji wa kundi hilo wakisema kuwa kikosi chao maalum ndicho kilichofanya mashambulizi hayo.

Soma: Uturuki yalalamika kwa Ujerumani kuhusu mkutano wa wakurdi

Afisa mmoja wa ngazi za juu kwenye wizara ya ulinzi aliliambia shirika la habari la AFP kwamba washambuliaji hao walitumia gari walilokuwa wameliteka na kumuua dereva wake katika mji wa Kayseri ulio umbali wa kilomita 260 kusini mashariki mwa Ankara kabla ya kufanya mashambulizi hayo.

PKK, ambayo imewekwa kwenye orodha ya makundi ya kigaidi nchini Uturuki, Marekani na mataifa yote ya Umoja wa Ulaya, ilianzisha uasi wa kutumia silaha mwaka 1984 katika eneo la kusini mashariki mwa Uturuki na tangu hapo zaidi ya watu 40,000 wameshapoteza maisha kwenye mgogoro huo.

Vyanzo: AFP, Reuters