1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yawekeza Somalia

16 Machi 2012

Uturuki imekuwa nchi ya kwanza kupeleka ndege ya kimataifa ya kusafirisha abiria nchini Somalia katika kipindi cha miaka 20. Hivi sasa nchi hiyo ina mpango wa kuwekeza katika maeneo mbalimbali Somalia.

https://p.dw.com/p/14LWl
Erdogan na rais Sheik Sharif Sheik Ahmed wa Somalia
Erdogan na rais Sheik Sharif Sheik Ahmed wa SomaliaPicha: AP

Shangwe na vigelegele vilisikika katika uwanja wa ndege wa mji mkuu wa Somalia, Mogadishu. Hii ilikuwa baada ya ndege ya kusafirisha abiria kutoka barani Ulaya kutua uwanjani hapo kwa mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya miaka 20. Abiria wa ndege hiyo walipokelewa na kundi la wakina mama waliokuwa wakiimba na kucheza.

Mataifa mengi yanaichukulia Somalia kama nchi iliyogubikwa na vita na hivyo kuwa nchi ambayo haipaswi kutemebelewa. Angalau mashirika yanayotoa misaada ndiyo yanayojishughulisha na nchi hiyo. Lakini Uturuki sasa imegundua kwamba Somalia ni mahali panapofaa kuwekeza. Waziri mkuu wa nchi hiyo, Recep Tayyib Erdogan, alikuwa kiongozi wa kwanza asiye wa Kiafrika kuitembelea Somalia Agosti mwaka jana, pale ambapo Somalia ilikuwa imekumbwa na janga la njaa. Tangu wakati huo, Uturuki imefanya juhudi nyingi kuimarisha nguvu zake nchini Somalia.

Shule, hospitali na chuo kikuu kujengwa

Wanafunzi wapatao 100 wanafundishwa katika shule ya kwanza ya Kituruki iliyopo Mogadishu. Mbali na kufundishwa Kisomali na Kiingereza, wanafunzi hao pia wanapata mafunzo ya lugha ya Kituruki. Walimu wa shule hiyo pamoja na familia zao wamehamia Mogadishu na wanajaribu kuishi maisha ya kawaida katika mji huo ulioharibiwa na mabomu. Bülent Ergünes, ambaye ni mwalimu mkuu wa shule, anaeleza. „Ninadhani kwamba sisi tumechanganyikiwa kidogo. Ni kweli kwamba hapa pana matatizo ya kiusalama. Kila siku kuna mahali ambapo mabomu yanaripuliwa. Lakini licha ya hayo ni lazima tutoe msaada.“

Vita na njaa vinayafanya maisha nchini Somalia kuwa magumu
Vita na njaa vinayafanya maisha nchini Somalia kuwa magumuPicha: dapd

Misaada inatolewa pia katika kituo cha afya. Madaktari na wauguzi wapatao 40 kutoka Uturuki wanawahudumia wagonjwa wapatao 1,000 kwa siku. Ipo mipango ya kufungua hospitali na baadaye hata kujenga chuo kikuu. Serikali ya Uturuki pia inatoa msaada wa chakula katika kambi za wakimbizi.

Kwa sasa, nchi ya Somalia ndiyo inayofaidika kutokana na urafiki baina yake na Uturuki. Lakini Uturuki inatarajia kwamba hali hiyo itabadilikia katika siku za usoni. Tayari nchi hiyo imekwishafungua ubalozi wake mjini Mogadishu. Uturuki, kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa, pia imepanga kufanya mkutano kuhusu Somalia mwezi wa sita mwaka huu. Huenda mkutano huo ukazumngumzia fursa iliyonayo Somalia katika kujiendeleza na kujisimamia na si kujadili zaidi kuhusu uharamia, viongozi wa kivita na watu wenye msimamo mkali wa kiislamu.

Mwandishi: Antje Diekhans

Tafsiri: Elizabeth Shoo

Mhariri: Othman Miraji