1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yazidisha mashambulizi ndani ya Syria

Mohammed Khelef28 Agosti 2016

Waasi wanaoungwa mkono na Uturuki wamekabiliana na vikosi vinavyoungwa mkono na Wakurdi kaskazini mwa Syria, huku jeshi la Uturuki likiendeleza kampeni yake ndani ya ardhi ya Syria.

https://p.dw.com/p/1Jr9m
Kifaru cha Uturuki kwenye ardhi ya Syria.
Kifaru cha Uturuki kwenye ardhi ya Syria.Picha: Reuters/U. Bektas

Serikali ya Uturuki, ambayo yenyewe inapambana na uasi wa Wakurdi ndani ya ardhi yake, inasema kampeni yake nchini Syria inahusiana pia na kuwazuwia Wakurdi kutwaa maeneo zaidi ndani ya Syria sambamba na kuwarejesha nyuma wapiganaji wa kundi lijiitalo Dola la Kiislamu (IS).

Uturuki inataka kuwazuwia wapiganaji wa Kikurdi kujiimarisha ndani ya Syria karibu na mpaka wake, jambo ambalo inahofia litakipa nguvu chama cha Wakurdi, PKK, ambacho kimekuwa kwenye vita vya miongo mitatu sasa kuwania utawala wake wa ndani.

Vyanzo kutoka vyombo vya usalama vya Uturuki vinasema ndege mbili chapa F-16 zililishambulia eneo linalodhibitiwa na wanamgambo wa YPG wa Kikurdi, ambao ni sehemu ya muungano wa wapiganaji wanaoungwa mkono na Marekani, Syrian Democratic Forces (SDF). Vyanzo hivyo vinasema ndege hizo zilishambulia pia maeneo sita yanayodhibitiwa na IS.

Askari wa Uturuki auawa

Jeshi la Uturuki lilisema askari wake mmoja aliuawa na watatu wengine kujeruhiwa pale kifaru chao kiliposhambuliwa kwa roketi ambalo lilirushwa kutoka eneo linalodhibitiwa na wapiganaji wa YPG. Jeshi lilijibu mashambulizi hayo kwa kulitwanga eneo hilo kwa mizinga.

Uwanja wa Ndege wa Diyabakir.
Uwanja wa Ndege wa Diyabakir.Picha: Getty Images/C. Hondros

Waasi nchini Syria wanaopingana na uingiliaji kati huu wa Uturuki wanasema kuwa jeshi la Uturuki lilivishambulia vikosi vyenye mafungamano na YPG lakini hakukuwa na vikosi vya Wakurdi kwenye eneo hilo. Waasi wanaoungwa mkono na Uturuki walipambana na wapiganaji wenye mafungamano na SDF karibu na mji wa Jarablus.

Vikosi vinavyopingana na Uturuki vilisema Uturuki imetuma vifaru vyake kwenye mji huo, ingawa serikali mjini Ankara ilikanusha.

Kwenyewe nchini Uturuki, watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Kikurdi walirusha makombora katika uwanja wa ndege wa mji mkubwa wa kusini mashariki wa Diyarbakir.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Dogan, makombora yapatayo manne yalilengwa kwenye kituo cha ukaguzi cha polisi kilichopo nje ya ukumbi wa kupumzika, ambapo wafanyakazi na abiria walilazimika kuhamishiwa sehemu salama.

Diyarbakir ni mji mkuu katika eneo la kusini mashariki mwa Uturuki linalokaliwa kwa kiasi kikubwa na Wakurdi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Sylvia Mwehozi