1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uuzaji wa vifaru vya Kijerumani Saudi Arabia unafadhaisha

5 Julai 2011

Jarida la Kijerumani, "SPIGEL", limefichua kwamba Ujerumani itaizuia Saudi Arabia vifaru 200 vya kijeshi baada ya Baraza la Usalama la Ujerumani kuamua hivyo katika kikako chake cha siri.

https://p.dw.com/p/11pQE
Kifaru cha kijeshi chapa Leopard 11A4 kutoka Ujerumani kitakachouziwa Saudi ArabiaPicha: picture-alliance/dpa

Ujerumani haisafirishi silaha kwa eneo ambalo liko katika mzozo. Kwa haki, hiyo ndio siasa rasmi ya serekali ya Ujerumani, na jambo hilo halifai kutikiswa. Kusema kweli, bila ya shaka, Saudi Arabia sio eneo la mzozo; nchi hiyo ni mshirika wa nchi za Magharibi.

Hata hivyo, biashara hii iliojipenyeza ya kupeleka vifaru vya kijeshi huko Saudi Arabia ni ya kufedhehesha. Pale michafuko katika Ulimwengu wa Kiarabu ilipoikumba nchi ndogo jirani ya Bahrein, utawala wa Saudi Arabia wenye utajiri wa mafuta ulipeleka vifaru vya kijeshi huiunga mkono serekali inayoitaka huko Manama, na kuyakomesha maandamano ya wapinzani wa serekali hiyo.

Pia vifaru vya kijeshi vya chapa ya Leopard ambavyo vitapelekwa huko Saudi Arabia ni venye kufaa kuyatawanya maandamano. Nafasi ya kujikinga katika upande wa mbele wa vifaru hivyo vinavifanya kuwa ni vyombo vya ukandamizaji vilivyo vya hatari kabisa. Kwa hivyo, biashara hiyo ya silaha iliojulikana inakwenda kinyume na  misingi ya kisiasa na kiadilifu ya Ujerumani. Na kutokana na hali maalumu ya kihistoria ya Ujerumani, jambo hilo linaleta mkanganyiko. Vipi tunaweza kuwaelezea watu wa eneo hilo ambao wanataka  kujikwamua na tawala za mabavu kwamba Wajerumani, kwa upande mmoja, wanakataa kuendesha shughuli za kijeshi dhidi mdikteta wa Libya, Muammar Gaddafi, na kwa upande mwengine, lakini wanatuma silaha kwa utawala ambao hata hauwaruhusu wanawake kuwa na liseni ya kuendesha gari?

Bado, lakini, Masheikh wa Saudi Arabia wenye utajiri wa mafuta wako kwenye  viti vyao. Lakini nani, katika hali hii ya sasa ya mwamko katika Ulimwengu wa Kiarabu, atatia dau kwamba mambo yatabakia hivi hivi hata siku za mbele? Na vipi mambo yatakavokuwa pale vifaru vya Kijerumani vitakapotumiwa dhidi ya waandamanaji wa amani ambao wanataka demokrasia na uhuru zaidi?

Usafirishaji huo nje wa vifaru unafuatiliza, kwa muda mfupi ujao, maslahi ya kiuchumi ya viwanda vya silaha ambavyo biashara yao ya ngambo katika  miaka iliopita imezidi mara mbili. Pia hata bila ya kuuzwa kwa Saudi Arabia, vifaru hiyvo vya kisasa kabisa vya chapa ya Leopard vitapata watu wa kuvinunua. Lakini vifaru hivyo visipewe serekali ambayo inapambana na waandamaji wa amani.

Saudi Arabia kwa nguvu inaingia katika mzunguko huu wa kujirundukizia silaha, na jambo hilo linafanyika katika eneo ambalo wakati huo huo, hata katika nyakati za kawaida, ni kama kasiki la baruti . Ni katika siku hizihizi Wasaudia wametishia kutengeneza bomu la atomiki, pindi Iran nayo itabakia inaishikilia programu yake ya kinyukliya. Serekali ya Ujerumani katika ngazi ya kimataifa inapigania kwa nguvu upunguzaji wa silaha za kinyukliya. Kutokana na hali hiyo, basi mauzo haya ya silaha yana hatari.

Ikiwa serekali ya Ujerumani inataka ipimwe kutokana na vitendo vyake, lazima biashara hiyo ya silaha hadi Saudi Arabia izuiliwe. Aama sivyo Ujerumani itaingia katika hatari ya kutoaminika.

Mwandishi: Daniel Schechkewitz / Miraji Othman/ZR

Mhariri: Miraji Othman