1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uwanja umeandaliwa Bashir kushinda uchaguzi Sudan

Josephat Nyiro Charo7 Aprili 2010

Bashir hana mpinzani mwenye mbavu

https://p.dw.com/p/MpfP
Rais wa Sudan Omar Hassan al-BashirPicha: picture-alliance/ dpa

Huku kukiwa na ari ya kufanya mageuzi makubwa nchini Sudan, hususan miongoni mwa kizazi kipya cha kaskazini mwa nchi hiyo, hakuna mazingira ya kampuni za kupamba moto wala wafuasi wanaowafuatafuata wagombea katika eneo la Sudan Kusini. Na huku kampeni za uchaguzi zikikaribia kufika kikomo, mchezo unaonekana umeshakwisha, kwani jukwaa limshaandaliwa kwa rais wa Sudan Omar Hassan al Bashir kushinda uchguzi huo.

Kukosekana kwa hamasa na mazingira ya uchaguzi nchini Sudan kwa sehemu fulani kunatokana na ukweli kwamba wapigaji kura wanatilia shaka hatua ya Yasir Arman kukiwakilisha chama cha Sudanese People´s Liberation Movement, SPLM, kama mgombea urais katika uchaguzi wa Aprili 11 hadi 13.

Arman ni mmoja kati ya Waarabu wachache waliojiunga na vuvugu la mapinduzi katika miaka ya mwanzo ya mapinduzi, lakini wakereketwa ndani ya chama cha SPLM wanasema, mtetezi huyo wa Sudan iliyoungana, hayuko radhi kuvaa jukumu ambalo huenda likashuhudia kugawanyika kwa taifa hilo.

Arman angeweza kushinda kura nyingi kwa chama cha SPLM katika eneo la kusini mwa Sudan, huku akishinda kura kadhaa katika eneo la kaskazini za waarabu wenye msimamo wa wastatni. Lakini kiongozi huyo anaonekana kama msaliti katika eneo la kaskazini kwa kusaliti ndoto ya Waarabu waislamu nchini Sudan.

Shinikizo dhidi ya Arman lilikuwa kubwa na hatimaye mnamo Aprili mosi akajiondoa kwenye kinyang´anyiro cha kuwania urais wa Sudan, akisingizia hitilafu katika mchakati wa maandalizi ya uchaguzi na mzozo katika jimbo la Darfur.

Chama tawala nchini Sudan, National Congress Paty, NCP, cha rais Bashir, ambacho kinadai kuyalinda masilahi ya Waarabu waislamu nchini Sudan, kina mtazamo tofauti: "Arman hana nafasi ya kushinda uchaguzi. Alipewa taarifa potofu kuhusu nafasi yake ya kuweza kushinda uchaguzi huo. Bashir atashinda" amesema Ibrahim Ahmed Omar, afisa wa ngazi ya juu wa chama cha NCP wakati alipozungumza na shirika la habari la Uingereza, BBC, mnamo Aprili 3 mwaka huu.

Vyama vya upinzani vinasema rais Bashir anataka kubakia madarakani kwa kuhalalisha mamlaka yake kupitia uchaguzi utakaosimamiwa na jumuiya ya kimataifa, na kwa njia hiyo kukwepa kukabiliwa na mashtaka katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC mjini The Hague nchini Uholanzi.

Uchaguzi wa Sudan umeandaliwa kumuwezesha mtu mmoja tu kushinda; naye ni rais Bashir. Chama cha NCP kinaandaa uchaguzi ili kuepukana na shinikizo la kimataifa dhidi ya kiongozi wake. Huku mgombea wa chama cha SPLM akiwa hayumo tena katika mashindano ya kugombea urais wa Sudan, dalili zinaonyesha wazi kwamba rais Bashir hana mpinzani na atashinda uchaguzi huo kwa mbwembwe. Sio kwa sababu yeye ni kiongozi maarufu bali ni kwa kuwa anadhibiti vyombo muhimu vya mamlaka, ikiwa ni pamoja na jeshi na vyombo vya usalama, ambavyo amekuwa akivitumia tangu aliponyakua madaraka kwenye mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 1989.

Rais Bashir anadhibiti pia vyombo vya habari vya kitaifa, ikiwemo radio na televisheni na anatumia fedha za umma na raslimali nyengine kama vile helikopta na magari kufanyia kampeni. Idadi kubwa ya zaidi ya asilimia 80 ya vyama vya upinzani vya Sudan havina nafasi kama hiyo iliyonayo chama tawala. Hakuna anayezungumzia juu ya uwezekano wa kufanyika duru ya pili ya uchaguzi nchini Sudan kutokana na kukosekana mgombea wa chama cha SPLM, mwenye mbavu za kushindana na rais Bashir. Uwanja uko wazi kabia kwa rais Bashir kushinda na kuendelea kuidhibiti Sudan.

Mwandishi: Josepht Charo/ IPS

Mhariri: Abdul-Rahman