1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uzio na mabomu ya kutegwa chini ya ardhi kuwekwa mpakani

P.Martin1 Machi 2007

Pakistan imeamua kujenga uzio na kuweka mabomu yanayotegwa chini ya ardhi katika mpaka wake na Afghanistan.Je nini kilichoifanya serikali ya Islamabad kuamua kuchukua hatua ya aina hiyo?

https://p.dw.com/p/CHJ7

Yadhihirika kuwa hatua hiyo inachukuliwa na Pakistan kufuatia lawama za Afghanistan na washirika wake wa magharibi,kuwa Islamabad haifanyi vya kutosha kuwazuia waasi wa Kitaliban na Al-Qaeda kuvuka mpaka huo mrefu wenye milima.Ingawa Pakistan inasema,sababu ya kutega mabomu chini ya ardhi na kujenga uzio huo ni kuwazuia Wataliban kujipenyeza Afghanistan na kuvisaidia vikosi vya NATO na washirika wake katika mikakati ya kuwapiga vita Wataliban,hatua hiyo inachochewa na lengo lake la binafsi kuhalalisha na kulinda eneo la kaskazini-magharibi linalopakana na Afghanistan.

Kwa sababu ya hali iliyokuwepo hivi sasa nchini Afghanistan na katika yale maeneo ya kikabila yanayotawalwa na serikali ya Pakistan,Islamabad ina nafasi nzuri ya kuitumia hali hiyo kutimiza malengo yake na kuimarisha maslahi yake katika eneo ambako kihistoria imekuwa na usemi au ushawishi mdogo tu.

Mwanzoni,Afghanistan ilihisi kuwa mpango wa Pakistan kutaka kujenga uzio na kutega mabomu mpakani katika eneo la mgogoro ni njia iliyo rahisi kwa Pakistan kutokabiliana na tatizo halisi na kujiepusha na dhima yake ya kuwasaka viongozi wa Kitaliban,ambao husemekana kuwa wana makao yao makuu mjini Quetta,katika wilaya ya Baluchistan.Afghanistan inasema,badala yake, Pakistan iwakamate viongozi wa Kitaliban walio nchini humo na makao yao yateketezwe.

Licha ya upinzani mkali wa serikali ya Afghanistan na watu wa kabila la Kipashtu walio pande zote mbili za mpaka,na hata baadhi ya nchi za magharibi kueleza wasiwasi wao,ujenzi wa uzio na kazi za kutega mabomu katika maeneo yanayotenga nchi hizo mbili zinaendelea.

Kanada kwa mfano,inapinga kutega mabomu katika maeneo ya mpakani kwa sababu inasema kitendo hicho huenda kinyume na Mkataba wa Ottawa wa mwaka 1997 unaopiga marufuku kutumia mabomu ya aina hiyo.

Kwa upande mwingine serikali ya rais Hamid Karzai wa Afghanistan imepinga kutega mabomu kwa sababu za kiutu,ikisema kuwa hatua kama hiyo itazitenga jamii za Kipashtu zinazohusiana na itavuruga maisha yao kwa daima.Wakazi wa kabila la Pashtu pande zote mbili za mpaka wamekataa kuutambua mpaka huo kama ni wa kimataifa na mara kwa mara huuvuka bila ya kujali madai ya Afghanistan au Pakistan kuwa ndio yanayotawala eneo hilo.

Ikiwa mpango wa kujenga uzio na kutega mabomu hautozuiliwa,basi utaimarisha msimamo wa Pakistan inayoshikilia kuwa mpaka uliowekwa pale taifa hilo lilipoundwa mwaka 1947 ni halali.

Azma halisi ya Pakistan kujenga uzio na kutega mabomu si kuwazuia wapiganaji wa Taliban na wa Al-Qaeda kuzuka mpaka,kwani mpaka huo ni mrefu sana ni shida kuweza kuudhibiti kwa maana. Pakistan inatumia khofu za nchi za magharibi kuhusu Wataliban wanaojipenyeza Afghanistan kutoka ardhi yake-jambo ambalo husababisha matatizo kwa juhudi za vikosi vya NATO na Afghanistan kuleta utulivu kusini na mashariki mwa Afghanistan.