1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Venezuela waandamana kumpinga Rais Maduro

Yusra Buwayhid
27 Oktoba 2016

Mamia ya watu waliandamana Venezuela wakidai kura ya maoni kumngo'a madarakani Rais Maduro. Kulizuka machafuko, baadhi walijeruhiwa na wengine walitiwa mbaroni na polisi, lakini upinzani umesema utandamana tena kesho.

https://p.dw.com/p/2RlCU
Venezuela Protest gegen Präsident Nicolas Maduro in Caracas
Picha: Getty Images/AFP/J. Barreto

Waaandamanaji wanaoipinga serikali nchini Venezuela wamemiminika katika mitaa ya mji mkuu wa Caracas, pamoja na miji mengine mikubwa, wakipinga utawala wa Rais wa nchi hiyo Nicolas Maduro, ambaye washirika wake waliukasirisha upinzani kwa kupinga kura ya maoni ya kumuondoa madarakani kiongozi huyo wa siasa za kisoshalisti.

Upinzani umeitisha maandamano mengine ya masaa 12 kesho, na umeapa kutumia nguvu yake ya wingi wa viti bungeni kuwasilisha azimio la kumuwajibisha kiongozi huyo wa siasa za kisoshalisti, kwa namna alivyoshindwa kuudhibiti mgogoro wa kiuchumi nchini humo.

Wanaharakati wa upinzani wanakisia kuwa watu milioni 1.2 walijitokeza katika maandamano ya mji mkuu wa Caracas, ikiwani idadi kubwa kabisa kwa maandamano ya siku moja yaliyosambaa nchi nzima.

Kulizuka machafuko kati ya waandamanaji hao wa upinzani na polisi. Watu watatu walipigwa risasi, mmoja wao akiwa afisa wa polisi ambaye alipoteza maisha. Watu wapatao 20 walijeruhiwa na wengine 80 walitiwa mbaroni na polisi nchini kote.

Maduro naye alifanya maandamano nje ya ikulu ya Venezuela, na maelfu ya wafuasi wake walimuunga mkono. Maduro pia aliitisha mkutano na Baraza la Ulinzi wa Taifa na alitolea wito wa kuwepo mazungumzo ya kuleta amani.

"Kwa upande wetu tunachokitaka Venezuela ni mazungumzo, amani, haki, … na kwa wale wanaochochea vurugu wajue kuwa wana majukumu ya kisheria, walikabili taifa na waombe msamaha, watambue kuwa kuna walioathirika na washiriki katika kuwapatia fidia na kwa wale wanaotaka haki jambo la busara ni kutafuta amani," amesema Nicolas Maduro.

Upinzani wataka kumfungulia kesi Maduro

Venezuela Nicolas Maduro
Rais wa Venezuela, Nicolas MaduroPicha: Getty Images/AFP/R. Schemidt

Muungano wa vyama vya upinzani MUD nchini humo umesema utakubali mazungumzo, kama serikali itaheshimu haki ya kikatiba ya kuitishwa kwa kura ya maoni, na kuwaachilia huru wanaharakati pamoja na viongozi wao kadhaa waliowekwa kizuizini, miongoni mwa madai mengine.

Maandamano hayo yanakuja baada ya mamlaka ya uchaguzi kupinga kupinga kampeni ya upinzani ya kutaka kufanyike kura ya maoni ya kumuondoa Maduro madarakani. Mvutano ulizidi kushika kasi pale Jumanne iliyopita bunge linalongozwa na upinzani lilipopiga kura ya kumfungulia mashitaka kiongozi huyo na kumtuhumu kwa kutaka kufanya mapinduzi nchini humo.

Serikali inasisitiza kwamba tokea mwaka 1999 hakujawahi kuwepo kifungu cha katiba kuhusu kosa la kiongozi kutotimiza wajibu wake, au kuhusu bunge kupiga kura ya kile kitakachowezesha mchakato wa kumfungulia mashitaka. Lakini Upinzani unapinga hoja hizo.

Matokeo ya kura za maoni ya taifa ya hivi karibuni yanaonyesha kwamba, asilimi 70 ya watu wa Venezuela hawamkubali Maduro. Wengi wanamlaumu Maduro kwa mfumuko wa bei nchini humo, uhaba wa chakula na madawa pamoja na mahitaji mengine muhimu.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/afpe/ap

Mhariri:Iddi Ssessanga