1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

VIENNA: Iran kutayarisha mpango wa kutenzua mgogoro wa nyuklia

23 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBpB

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomu la Umoja wa Mataifa,IAEA bwana Mohamed El-Baradei amesema, msuluhishi mkuu wa Iran kuhusu masuala ya nyuklia,bwana Ali Larijani,amekubali kuandaa katika kipindi cha miezi miwili,mpango wa kutafuta njia za kuutenzua mgogoro wa nyuklia wa Iran.El-Baradei amesema,mkutano wake wa saa mbili pamoja na Larijani siku ya Ijumaa umeridhisha. Wakati huo huo,akaongezea kuwa tatizo kuu la shirika hilo la Umoja wa Mataifa ni kutekeleza ukaguzi kamilifu nchini Iran.Hii leo,Larijani anakutana na mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya,Javier Solana nchini Ureno.Nchi za Magharibi zina hofu kuwa mradi wa Iran utatumiwa kutengeneza silaha za nyuklia.Iran lakini inashikilia kuwa mradi wake wa nyuklia ni kwa matumizi ya kuzalisha nishati.