1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vijana upande wa Magharibi wanavyojihisi sasa

30 Septemba 2010

Asilimia 20 ya Wajerumani hawakushuhudia Ujerumani iliyotengana, kwani wao walizaliwa baada ya mwaka 1990. Je tarehe 3 Oktoba ina umuhimu gani kwa wale waliozaliwa baada ya muungano wa Ujerumani?

https://p.dw.com/p/PLdf
Matteo Brossette kutoka ColognePicha: DW

Je, vijana wanaoishi Cologne na Frankfurt-Oder wana mipango gani kuhusu maisha yao? Mwandishi wetu Birgit Görtz amezungumza na wanafunzi wa shule moja katika mji wa Cologne na ametuletea ripoti ifuatayo. Msomaji ni Prema Martin.

Kufuatia miaka 20 ya muungano wa Ujerumani,hakuna tofauti kati ya vijana wa mashariki na magharibi ya Ujerumani.Hiyo ni kwa mujibu wa mtaalamu wa masuala ya vijana,Thomas Gensicke. Sababu ni kuwa vijana hao wameshuhudia takriban hali zile zile katika miaka hiyo 20 ya muungano. Lakini kiuchumi, vijana wa magharibi wapo katika hali bora zaidi.

Kwa kijana Matteo Brossettes hivi sasa muziki ni sehemu muhimu ya maisha yake na hajishughulishi sana na masuala ya kisiasa. Hiyo ni kinyume na vijana wanaoishi mashariki ya Ujerumani kama alivyojionea hivi karibuni, alipohudhuria tamasha la muziki wa Punk mjini Leipzig. Anasema huko vijana wengi walikuwa wamevaa fulana zenye kaulimbiu za kisiasa kama vile kupinga sera kali za mrengo wa kulia na kuunga mkono amani badala ya vita. Anasema:

" Kwetu vijana hufanya hivyo wakati wa maandamano. Lakini huko mashariki daima hutembea na fulana zenye kauli mbio za kisiasa. Naamini kuwa kwa wao hilo ni jambo la kawaida tu."

Hata rafiki yake mmoja, Josephine, alishuhudia hali kama hiyo, lakini vijana hao walihusika na sera tofauti kabisa za kisiasa. Anasema, ilikuwa wazi kabisa kwamba vijana aliowaona walikuwa wafuasi wa sera kali za mrengo wa kulia. Kwani alipotembelea kijiji kimoja kidogo kisiwani Usedom, kila mmoja alikuwa akisikiliza nyimbo za bendi inayojulikana kwa sera zake kali za mrengo wa kulia.Kwa maoni ya Josephine hiyo imepindukia mipaka.

"Huko pia kila mmoja alivaa fulana za bendi zenye sera kali za mrengo wa kulia."

Lakini Josephine anafahamu kuwa katika mashariki ya Ujerumani, wachache ndio walio wafuasi wa sera kali za mrengo wa kulia. Hata mtaalamu wa masuala ya vijana Gensicke anakubaliana nae. Lakini yeye amegundua mwelekeo mmoja: Vijana wa mashariki wanaikosoa zaidi mifumo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ya serikali kuu kuliko vijana wenzao katika magharibi ya Ujerumani.Hata hivyo, Josephine alipoulizwa iwapo angependelea kuhamia mashariki, amesema kuwa yeye yupo wazi kwa kila kitu. Lakini baadae angependa kuishi katika mji mkubwa. Ni vijana wachache sana wa magharibi walio tayari kuhamia mashariki. Kwani wengi wao wanaamini kuwa katika magharibi ya Ujerumani wana nafasi bora zaidi kusomea kazi na kupata ajira. Hata vijana wa mashariki wanaamini hivyo hivyo.

Mhariri: Görtz,Birgit/ZPR

Mpitiaji: M.Abdul-Rahman

ENDE