1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vijana wa Afrika warejea nyumbani baada ya masomo ughaibuni

Oumilkheir Hamidou
13 Januari 2017

Uamuzi wa kujerea nyumbani vijana wa kiafrika, serikali kuu ya Ujerumani kuzidisha idadi ya wanajeshi wa kulinda amani Mali na kilio cha wanafunzi wa chuo kikuu cha Makerere ni miongponi mwa mada magazetini wiki hii.

https://p.dw.com/p/2VmIl
Uganda Studentenproteste Makerere Universität
Picha: picture-alliance/AA/L. Abubaker

 

 Tunaanza na gazeti la Die Zeit linalozungumzia kuhusu shauku ya kurejea nyumbani Afrika. Katika nchi nyingi za Afrika uchumi unanawiri. La kufurahisha zaidi ni kuona kwamba vijana wengi waliokwenda ughaibuni kusoma, wanaamua kurejea nyumbani, linaandika gazeti hilo linalotoa mfano wa Lagos nchini Nigeria. Die Zeit linasimulia kuhusu watumishi wa kituo cha kukusanya takataka cha kampuni la WeCyclers ambako chupa zote za vinywaji tangu vya Cola, Pepsi mpaka maji, ndogo na kubwa hukusanywa na kati kati wako wanawake wanaokwangua vikaratasi vilivyobandikwa juu ya chupa hizo na kuzisafisha na baadae kuzitia ndani ya magunia.

"Chupa lazma ziwe safi zinapopelekwa kusagwa sagwa" anasema Bilikissi Adebiyi-Abiola-baadae tu ndipo wanapolipwa Naira 90-sawa na centi 45, kwa kila kilo moja ya chupa tupu. Bilikissi Adebiyi-Abiola ana umri wa miaka 34,anashughulikia mradi  wa kuzipatia thamani takataka mjini Lagos. Msichana huyo amesomea katika taasisi mashuhuri ya teknolojia ya mjini Massachusettes nchini ambako amemaliza kwa kujipatia shahada ya uzamili. Angeweza kupata kazi mahala kokote Marekani, lakini ameamua kurjea nyumbani-linaandika gazeti la Die Zeit, linalomalizia kwa kusema Bilikissi-Adebiyi-Abiola si peke yake aliyeamua hivyo, wengi wa wanafunzi waliomaliza masomo yao katika vyuo vikuu vya Marekani au Uingereza wanaamua kurejea nyumbani.

 Ujerumani yaamua kutuma wanajeshi zaidi Mali

Gazeti la Neues Deutschland limeandika kuhusu uamuzi wa serikali kuu ya Ujerumani kuzidisha idadi ya wanajeshi wa bundeswehr wanaotumikia kikosi cha umoja wa mataifa cha kulinda amani nchini Mali-MINUSMA."Wanapelekwa jangwani kwa muda" ndio kichwa cha maneno cha ripoti ya gazeti hilo linalosema uamuzi huo umezusha mjadala mkali hivi sasa humu nchini. Kwa mujibu wa uamuzi huu mpya idadi kubwa ya wanajeshi wa Ujerumani watashughulikia masuala ambayo si ya kijeshi katika nchi hiyo ya Afrika magharibi na katika eneo la Sahel. Makubaliano ya awali ambayo muda wake unamaluizika mwishoni mwa mwezi huu yalikuwa yakizungumzia juu ya kuwekwa wanajeshi hadi 650 wa Bundeswehr nchini Mali. Idadi yao itazamiwa kuongezeka na kufikia elfu moja watakaotumikia juhudi za amani katika nchi hiyo ya jangwani.

"Serikali kuu haijajifunza na yaliyotokea Afghanistan", linaandika gazeti la Neues Deutschland linaloutaja mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani kuwa ni wa hatari. Lakini Ujerumani inafuata malengo manne nchini Mali. Mbali na kuwajibika kimataifa na kuonyesha mshikamano na Ufaransa, muhimu zaidi  kwa Ujerumani, linamaliza kuandika gazeti la Neues Deutschland, "ni kupunguza sababu zinazopelekea maelfu ya waafrika kukimbilia Ulaya."

 Kilio cha wanafunzi wa chuo kikuu cha Makerere

Ripoti yetu ya mwisho katika ukurasa huu wa Afrika katika magazeti ya Ujerumani inatufikisha katika mji mkuu wa Uganda-Kampala kinakokutikana chuo kikuu mashuhuri cha Makerere. "Kilio cha kudai elimu" ndio kichwa cha maneno cha gazeti la mjini Munich, "Süddeutsche" linalozungumzia maandamano ya wanafunzi wakilalamika dhidi ya ughali wa masomo na walimu wasiofika madarasani. Shida hizo wanakabiliana nazo pia wanafunzi wa Ujerumani wanaokwenda kusoma Uganda linaandika gazeti la Süddeutsche.

"Hii si mara ya kwanza kwa wanafunzi wa chuo kikuu cha Makerere kuandamana lakini  maandamano ya Novemba iliyopita yalikuwa makali zaidi" linaandika gazeti hilo. Süddeutsche linajiuliza "kwanini chuo kikuu mashuhuri cha "Mak" kama kinavyojulikana miongoni mwa wanafunzi wa Uganda na Afrika kwa jumla, "kina shida ya fedha katika wakati ambapo kila mwanafunzi mmoja kati ya wanafunzi zaidi ya 30.000 analazimika kulipa Euro kati ya 300 na 400 kila mhula mmoja wa mafunzo."

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/ BASIS/PRESSER/ALL/presse

Mhariri: Iddi Ssessanga