1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya jeshi la muungano vyaishambulia Libya bila huruma

26 Machi 2011

Vikosi vya jeshi la muungano linaloongozwa na Marekani vimeongeza shinikizo kwa kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi kutokana na mfululizo wa mashambulio ya anga bila huruma.

https://p.dw.com/p/10hpK
Wanajeshi wanaoshiriki kwenye operesheni za LibyaPicha: picture-alliance/dpa

Miripuko ilisikika kwenye mji mkuu wa Tripoli mapema leo na walioshuhudia wamesema kuwa eneo la rada ya kijeshi lilikuwa likiwaka moto.

Ndege za kivita za jeshi la muungano zilifanya mashambulio 150 zaidi dhidi ya vikosi vya jeshi la Kanali Gaddafi, ukiwemo mji wa mashariki wa Adjabiya. Mashambulio hayo yamewawezesha waasi kuudhibiti tena mji huo.

NATO Libyen Kampfflieger
Baadhi ya ndege za kijeshi zinazoshiriki katika operesheni nchini LibyaPicha: AP

Kuna taarifa kwamba mtoto wa kiume wa Kanali Gaddafi, Saif al-Islam ameondoka kwa siri nchini humo ikiwa ni katika kuchukua hatua za kidiplomasia kwa ajili ya kuzuia mapigano zaidi na kuidhibiti hali iliyopo sasa ya kisiasa na kijeshi ambayo inazidi kuwa mbaya.

Marekani na Jumuiya ya Kujihami ya NATO zinafikiria kuwapatia silaha wapinzani, zikisema kuwa azimio la Umoja wa Mataifa linaruhusu uwezekano huo.

NATO hatimaye pia imekubali kuchukua jukumu la kuongoza operesheni za kutekeleza marufuku ya ndege kuruka katika anga ya Libya. Operesheni hiyo itakuwa chini ya Jenerali Charles Bouchard kutoka Canada.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE,RTRE,DPAE)
Mhariri: Mohamed Dahman