1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikwazo dhidi ya wakuu wa ujasusi Urusi

26 Julai 2014

Ikighadhibishwa kutokana na kudunguliwa kwa ndege ya abiria ya Malaysia Umoja wa Ulaya imewaingiza kwenye orodha yake ya vikwazo wakuu wa ujasusi wa Urusi wakati ikijiandaa kuchukuwa hatua kali zaidi dhidi ya nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/1CjLK
Alexander Bortnikov Mkuu wa Shirika la Usalama la Urusi (FSB).
Alexander Bortnikov Mkuu wa Shirika la Usalama la Urusi (FSB).Picha: picture-alliance/dpa

Kwa mujibu wa waraka rasmi ya Umoja wa Ulaya Mkurugenzi wa shirika la usalama la FSB Alexander Bortnikov na Mkuu wa Shirika la Ujasusi la Kigeni la Urusi Mikhail Fradkov ni miongoni mwa watu 15 na asasi 18 zilizokumbwa na hatua za kuzuiliwa mali zao na marufuku ya viza.

Taarifa hiyo imesema Bortnikov na Fradkov ambao wote wawili ni wajumbe wa Baraza la Usalama la Urusi wamejumuishwa kwenye orodha hiyo kwa kuhusika na "kuitishia mamlaka ya dola,haki ya kujitawala na uhuru wa Ukraine."

Waathirika kwa vikwazo

Miongoni mwa watu wengine waliojumuishwa kwenye vikwazo hivyo ni Rais Ramzan Kadyrov wa Chehchnya kwa kupendekeza kutuma vikosi vyake kuwasaidia waasi wanaoiunga mkono Urusi mashariki mwa Ukraine ambao wamelaumiwa kwa kuiangusha ndege hiyo ya Malaysia safari nambari MH 17 kwa kutumia kombora lililotengenezwa Urusi.

Rais wa Chechnya Ramzan Kadyrov amejumuishwa kwenye vikwazo vya Umoja wa Ulaya.
Rais wa Chechnya Ramzan Kadyrov amejumuishwa kwenye vikwazo vya Umoja wa Ulaya.Picha: picture-alliance/dpa

Makundi yaliyoingizwa kwenye vikwazo hivyo ni wanamgambo waasi, mamlaka zilioko Ukraine pamoja na kampuni zinazotajwa kusaidia na kurahisisha kunyakuliwa kwa rasi ya Crimea na Urusi hapo mwezi wa Machi ambako ndiko iliko kambi ya manowari za Urusi katika Bahari Nyeusi.

Maafisa wa Umoja wa Ulaya wamesema orodha ya majina zaidi inatarajiwa kutolewa hapo Jumanne yumkini ikawalenga watu waliko karibu na Rais Vladimir Putin wa Urusi.

Tangazo hilo lililotolewa Jumamosi (26.07.2014) inamaanisha jumla ya watu 87 na asasi 20 zimekumbwa na awamu ya pili ya vikwazo ya kuzuwiya mali na marufuku za viza vya Umoja wa Ulaya wakati ukijiandaa kupitisha awamu ya tatu ya vikwazo itakayokuwa pana zaidi kwa kulenga sekta kuu za uchumi.

Vikwazo vikali zaidi

Wawakilishi wa nchi wanachama 28 wa Umoja wa Ulaya walikubaliana hapo Ijumaa juu ya waraka wa kisheria wa kuwezesha utekelezaji wa hatua hizo mpya zenye kulenga nyanja nne masoko ya mtaji, ulinzi, matumizi ya bidhaa kwa pande mbili na teknolohjia nyeti ikiwemo sekta ya nishati.

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Umoja wa Ulaya katika mkutano wa Brussels.(22.07.2014)
Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Umoja wa Ulaya katika mkutano wa Brussels.(22.07.2014)Picha: picture-alliance/dpa

Wawakilishi hao na maafisa wa serikali wataendelea kujadiliana mwishoni mwa juma na Jumatatu kwa lengo la kukamilisha mkutano wao wa mwisho hapo Jumanne.

Kwa kawaida viongozi wa Umoja wa Ulaya watakutana ili kutowa baraka zao za kisiasa lakini Rais wa Baraza la Ulaya Herman Van Rompuy tayari amewataka katika baruwa kuwaagiza mabalozi wao kukubali hatua hizo hapo Jumanne.

Mpango wa vikwazo unafaa

Mkuu wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barosso amesema hapo Ijumaa mpango huo wa vikwazo iliopendekezwa unafaa,shabaha zake ni mahsusi una uwiano na unaweza kufanyiwa mabadiliko ya kutosha kuuwezesha Umoja wa Ulaya kuurekebisha kwa kulingana na hali ya mambo yanavyokwenda.

Jose Manuel Barroso Mkuu wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya.
Jose Manuel Barroso Mkuu wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya.Picha: /AFP/Getty Images

Barosso pia amerudia wito uliokuwa ukitolewa kwa Urusi kubadili mkondo wake kwa Ukraine ,kuwacha kuwasaidia waasi na kujitolea kwa mazungumzo makini ya kutafuta ufumbuzi wa amani kwa mzozo huo.

Hadi sasa kutokana na ukweli kwamba nchi nyingi wanachama wa Umoja wa Ulaya zina uhusiano mkubwa wa kiuchumi na Urusi zimeufanya umoja huo kusita kuchukuwa hatua kali za kiuchumi zinazoungwa mkono na Marekani lakini kudunguliwa kwa ndege ya Malaysia kulikogharimu takriban maisha ya watu 300 kumeufanya ubadili msimamo huo.

Uchumi wa Urusi kuathirika

Katika baruwa yake Van Rompuy amesema hatua hizo zitakuwa na taathira kubwa kwa uchumi wa Urusi lakini athari haitokuwa kubwa kwa uchumi wa Ulaya ambao bado uko katika mchakato wa kufufuka.

Jose Manuel Barroso Mkuu wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya (kushoto) na Rais wa Baraza la Ulaya Herman Von Rompuy (kulia).
Jose Manuel Barroso Mkuu wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya (kushoto) na Rais wa Baraza la Ulaya Herman Von Rompuy (kulia).Picha: picture alliance/AA

Vikwazo vya silaha vilivyopendekezwa vitaathiri mikataba ya usoni tu na kuiepusha Ufaransa na tahayuri kutokana na mauzo yake ya meli mbili za kivita chapa ya Mistral yenye thamani ya euro bilioni 1.2 yaliokosolewa mno.

Katika sekta ya teknolojia vikwazo hivyo vitawekwa katika sekta ya mafuta na sio gesi ambapo kwayo Urusi husambaza theluthi moja ya mahitaji ya Ulaya na hii ni kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa nishati wa Umoja wa Ulaya.

Urusi imekuwa ikishutumu vikwazo hivyo vya Marekani na Umoja wa Ulaya kuwa havifai, havileti tija na vina madhara kwa maslahi yao ya pamoja hususan kutokana na vitisho vya ugaidi vinavyozidi kuongezeka na ukosefu wa utulivu duniani.

Imerudia tena ujumbe wake huo Jumamosi kwa kusema Umoja wa Ulaya umetamka kwa vitendo lakini kwa kuhatarisha ushirikiano wa kimataifa katika fani ya usalama.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri : Sudi Mnette