1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikwazo vipya dhidi ya Korea ya Kaskazini

Abdu Said Mtullya21 Julai 2010

Marekani leo imetangaza vikwazo vipya dhidi ya Korea ya Kaskazini.

https://p.dw.com/p/OQfK
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Rodham Clinton, ziarani Korea ya Kusini .Anaongozana na waziri wa ulinzi Robert Gates.Picha: AP

Marekani leo imetangaza vikwazo vipya dhidi ya Korea ya Kaskazini vitakavyoizuia nchi hiyo kununua au kuuza silaha.Marekani pia itazuia mali za watu fulani binafsi wa Korea ya Kaskazini.

Akifafanua juu ya vikwazo hivyo waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton anaefanya ziara katika Korea ya Kusini amesema kuwa vikwazo hivyo vinaelekezwa kwa viongozi wa Korea ya Kaskazini,shabaha ikiwa ni kuendelea kuibana serikali ya nchi hiyo ya kikomunisti.Baada ya mazungumzo yake mjini Seoul na viongozi wa serikali ya Korea ya Kusini waziri wa mambo ya nje wa Marekani Clinton ameeleza kuwa vikwazo hivyo vipya ni sehemu ya juhudi za jumuiya ya kimataifa zenye lengo la kuizuia Korea ya Kaskazini kuendelea kuunda silaha za maangamizi.

Bibi Clinton amesema hatua hizo zilizochukuliwa na Marekani zitachangia katika kukomesha mipango ya Korea ya Kikomunisti ya kugharimia shughuli za uundaji wa silaha.

Clinton amesema Marekani itaiwekea vikwazo vipya maalum Korea ya Kaskazini vitakavyoelekezwa katika kuizuia nchi hiyo kununua silaha na mahitaji yanayohusiana.Vikwazo hivyo pia vitaelekezwa katika kuizuia nchi hiyo kupata bidhaa za anasa.Amesema hatua hizo mpya zitaimarisha utekelezaji wa vikwazo vilivyowekwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Hata hivyo waziri wa mambo ya nje wa Marekani bibi Clinton amehakikisha kuwa vikwazo hivyo vipya havielekezwi dhidi ya wananchi wa Korea ya Kaskazini.Akizungumza kwenye mkutano na waandishi habari katika mji mkuu wa Korea ya Kusini Seoul, Clinton alisema shabaha ya vikwazo hivyo vipya ni kuikwamisha mipango haramu na ya uchokozi inayotekelezwa na serikali ya Korea ya kaskazini.

Hatua hizo mpya zilizochukuliwa na Marekani zina lengo la kuonyesha mshikamano na Korea ya Kusini baada ya mkasa wa kuzamishwa meli ya nchi hiyo na kusababisha vifo vya mabaharia wake 46.Marekani na Korea ya kusini, kwa kutumia msingi wa utafiti uliofanywa na mashirika ya kimataifa zinailaumu Korea ya Kaskazini kwa kuzamishwa meli hiyo.Marekani na Korea ya Kusini zinadai kwamba Korea ya Kaskazini iliizamisha meli hiyo kwa kuipiga bomu la chini ya maji.

Katika ziara yake ya nchini Korea ya Kusini,bibi Clinton anafuatana na waziri wa ulinzi Robert Gates.Hapo awali mawaziri hao walifanya mazungumzo na mawaziri wenzao wa Korea ya Kusini.

Katika tamko la pamoja baada ya mazungumo yao,mawaziri hao waliionya Korea ya Kaskazini dhidi kufanya vitendo vya uchokozi Wamesema vitendo hivyo vitasababisha madhara makubwa kwa nchi hiyo ya kikomunisti.

Waziri wa mambo ya nje Clinton na waziri wa ulinzi Gates pia walifanya ziara kwenye mpaka wa Korea mbili, kama ishara ya kuonyesha mshikamano na Korea ya kusini.

Mwandishi:Abdul Mtullya /afp/dpa

Mpitiaji:Mohammed Abdul-Rahman