1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikwazo vya Ulaya kwa Urusi sio vikali

30 Aprili 2014

Vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya vya marufuku ya viza na uzuwiaji wa mali dhidi ya Urusi vinaonekana kuwa sio vikali kulinganishwa na vile vilivyowekwa na Marekani dhidi ya nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/1Bqvf
Wanaharakati wanaotaka kujitenga katika mji wa Donetsk mashariki mwa Ukraine.
Wanaharakati wanaotaka kujitenga katika mji wa Donetsk mashariki mwa Ukraine.Picha: Stepanov/AFP/Getty Images

Orodha ya vikwazo ya Umoja wa Ulaya iliochapishwa leo hii imewajumuisha wanasiasa waandamizi wa Urusi lakini haikuhusisha kampuni kama ilivyofanya serikali ya Marekani wakati ilipoongeza orodha yake ya vikwazo dhidi ya nchi hiyo hapo jana.

Serikali ya Urusi imeshutumu mara moja vikwazo hivyo vipya vya Umoja wa Ulaya kwa kusema kwamba vinatii tu amri ya Marekani na kwamba nchi za umoja huo zinapaswa kuona aibu kwa kitendo chao hicho. Mwanasiasa mwandamizi wa Urusi amesema serikali ya nchi hiyo inashughulikia hatua za kukabaliana na vikwazo hivyo vipya.

Lakini wakati masoko ya hisa ya Urusi yakiimarika kufuatia tangazo la vikwazo ambavyo sio vikali vya Umoja wa Ulaya kuliko vile ilivyokuwa ikitegemewa dalili zimekuwa zikizidi kuongezeka kwamba mzozo wa Ukraine unasababisha athari kwa sehemu kuu za uchumi wa Urusi.

Athari ya vikwazo

Kampuni ya Urusi ya kusafirisha nje gesi ya asili ya Gazprom imesema vikwazo zaidi vinaweza kutibuwa mauzo ya gesi kwa Ulaya na kuathiri biashara yake wakati waziri mmoja wa Urusi akisema vikwazo vya Marekani kwa mauzo ya vifaa vya teknolojia ya hali ya juu kwa Urusi litakuwa pigo kwa makampuni ya Urusi yalioko kwenye sekta hiyo.Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limesema linajiandaa kushusha uwezo wa ukuaji wa uchumi wa Urusi kwa mara ya pili katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja.

Makao makuu ya kampuni kubwa ya gesi ya Urusi Gazprom mjini Moscow.
Makao makuu ya kampuni kubwa ya gesi ya Urusi Gazprom mjini Moscow.Picha: Vasily Maximov/AFP/Getty Images

Kampuni yenye kutowa kadi za mikopo ya Marekani ya Visa imesema itasitisha huduma zake za mtandao kwa benki mbili za Urusi zilizowekewa vikwazo na Marekani hapo jana.

Marekani imekuwa wakali zaidi katika kuiadhibu Urusi kwa vikwazo kuliko Umoja wa Ulaya ambayo inategemea mno Urusi kwa nishati na ina mahusiano ya karibu ya biashara. Umoja wa Ulaya imewaekea vikwazo watu binafsi tu na sio kampuni.

Wizara ya mambo ya nje ya Urusi imesema vikwazo vya Umoja wa Ulaya havitosaidia kupunguza mvutano nchini Ukraine ambapo serikali ya nchi hiyo imekuwa mbioni kuwadhibiti wanaharakati wanaotaka kujitenga wanaoiunga mkono Urusi.

Kimbunga cha kisiasa Ujerumani

Kwa upande mwengine uamuzi wa kansela wa zamani wa Ujerumani Gerhard Schroeder kusheherekea miaka yake sabini katika tafrija ya kifahari kwenye mji wa St.Petersburg nchini Urusi imesababisha kimbunga cha kisiasa nchini Ujerumani.

Kanserla wa zamani wa Ujerumani Gerhard Schroeder (katikati) akimkaribisha Rais Vladimir Putin wa Urusi katika Kasri la Yusupov mjini St.Petersburg Urusi. (28.04.2014).
Kanserla wa zamani wa Ujerumani Gerhard Schroeder (katikati) akimkaribisha Rais Vladimir Putin wa Urusi katika Kasri la Yusupov mjini St.Petersburg Urusi. (28.04.2014).Picha: picture-alliance/dpa

Sherehe hizo za jana zinakuja wakati Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akiongoza juhudi za Ulaya na Marekani kumlazimisha Rais Vladimir Putin wa Urusi kutekeleza makubaliano ya amani ya Geneva yenye lengo la kupunguza mvutano mashariki ya Ukraine.

Afisa wa serikali ya Ujerumani amesisitiza hapo jana kwamba Schroeder ambaye ni mwenyekiti wa mradi wa pamoja wa North Stream wa bomba la kampuni ya gesi ya Urusi alikuwa haiwakilishi Ujerumani kwa njia yoyote ile rasmi katika tukio hilo ambapo alikumbatiana na Putin mbele ya wapiga picha mlangoni mwa Kasri la Yusupov la karne ya 18 ambapo tafrija hiyo ilifanyika.

Hatua hiyo imeshutumiwa katika fani nzima ya kisiasa nchini Ujerumani ambapo kiongozi wa chama cha Kijani Katrin Goering -Eckhard akisema tafrija hiyo imedhoofisha juhudi za serikali ya mseto ya Merkel kuutatuwa mzozo wa Ukraine.

Mwandishi : Mohamed Dahman / Reuters/dpa

Mhariri: Yusuf Saumu