1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vilabu vya Bundesliga vyajinoa kuanza upya

Sekione Kitojo
24 Julai 2017

Vilabu vya Bundesliga  vinajinoa makali  kwa  ajili  ya msimu  ujao , mabingwa Bayern Munich Munich  bado wako  katika  ziara  barani  Asia , kukumbana  na Chelsea  Jumanne.

https://p.dw.com/p/2h4ec
FC Bayern München in China
Picha: picture alliance/dpa

Vilabu vya  Bundesliga  vimeingia  kambini kujinoa  kwa msimu  ujao , ambapo mabingwa  watetezi  Bayern  Munich bado  wako  katika  ziara  barni  Asia  ambako  wamekwisha cheza  michezo  miwili, ambapo waliangukia  pua , baada ya  kushindwa  na  Arsenal  London  katika  mchezo ambao  uliamuliwa  kwa  mikwaju  ya  penalti 3-2 na  kisha kupata  kipigo  cha  mabao 4-0  dhidi  ya  AC Milan.

FC Bayern München in China
Mashabiki wa Bayern Munich nchini China wakiishangiria timu yaoPicha: picture alliance/ZUMA Press

Kesho Jumanne Bayern  inaingia  uwanjani  kujaribu  bahati  yake katika  ziara  hiyo  kwa  kupambana  na  kikosi  cha  kocha Antonio Conte , Chelsea  ambacho  kimeongezwa  makali kwa  kumpata  mshambuliaji Alvaro Morata  kutoka Real Madrid  ya  Uhispania. Kocha Carlo Anceloti  hata  hivyo anasema  hana  wasi  wasi  ama  presha  licha  ya  timu yake  kusuasua  katika  michezo  ya  majaribio. Amesema " iwapo atakuwa  na  presha  wakati  huu , basi msimu utakapoanza  atakuwa  amekufa." Bayern inacheza  pia  na Inter Milan  siku  ya  Alhamis.

Fussball |Training FC Bayern Muenchen | Thomas Müller und James Rodriguez
Wachezaji wa Bayern Munich James Rodriguez (kushoto) na Thomas Mueller (kulia)Picha: picture-alliance/S. Simon

Makamu  bingwa  RB Leipzig  tayari  iko  kambini  na imejiimarisha  kwa  kuwasajili  baadhi  ya  wachezaji chipukizi kadhaa  pamoja  na  kuwabakisha  kikosini wachezaji  wake  muhimu  kama  Naby Keita  ambaye anasakwa  na  Liverpool  ya  Uingereza  kwa  kitita  hadi euro milioni  80. Hata  hivyo  viongozi wa  Leipzig wamesema  hawana  wazo  la  kumuuza Naby Keita, ama mchezaji  mwingine  wa  kati Emil Forsberg.

Borussia  Dortmund ilimaliza ziara  yake  ya  bara  la  Asia wiki  iliyopita  na  inaingia  kambini  rasmi tarehe  26 mwezi huu, nchini  Uswisi, huku  ikikabiliwa  na  tetesi  za mshambuliaji  wake  hatari Pierre Emerick Aubamiyang kuipa mkono wa kwaheri  klabu  hiyo majira  ya  baridi msimu  ujao. Lakini  mkurugenzi  wa  sporti  wa  BVB Michael Zorc  amewahakikishia  mashabiki  wa  klabu  hiyo kuwa  Auba  haendi  kokote  msimu  ujao.

1. Bundesliga - FC Bayern München Muenchen - BVB Borussia Dortmund: Ousmane Dembele & Christian Pulisic
Ousmane Dembele (kushoto) na Christian Pulisic wa Borussia Dortmund Picha: picture-alliance/augenklick/firo Sportphoto/S. el-Saqqa

Pia  mchezaji wa  ulinzi  Sokrates  amehusishwa  na  uhamisho  kwenda Juventus Turin  ya  Italia, baada  ya  klabu  hiyo  bingwa ya  Italia  kumpoteza  mlinzi  wake  muhimu  Bonuci ambaye  katimkia  kwa  mahasimu  wao AC Milan. Schalke 04  pia  nayo imo  katika  ziara  barani  Asia na  ilitoka sare ya  bao 1-1 na  Inter Milan  ya  Italia  wiki  iliyopita. Ligi ya Ujerumani Bundesliga  inaanza  rasmi  tarehe 18 Agosti ambapo  mabingwa  watetezi  Bayern Munich itakwaana  na Bayer Leverkusen.

Mchezaji bora wa mwaka

Wakati  huo  huo Philip Lahm  ambaye  amekuwa  mlinzi imara  wa  kulia  wa  klabu  ya  Bayern Munich  na  timu  ya taifa  ya  Ujerumani Die Mannschaft , na  kutundika madaluga  yake msimu  uliopita  akiwa  nahodha  wa Bayern , ameteuliwa  kuwa  mchezaji  bora  wa  mwaka  na jopo  la  waandishi  habari za michezo wa  Ujerumani. Kocha  bora  msimu  uliopita  ni Julian Nagelsmann wa Hoffenheim  ambaye  ameiweka  timu  hiyo  katika  nafasi ya  nne  msimu  uliopita  na  kuonja  kucheza  katika Champions League msimu ujao. 

FC Bayern München - Philipp Lahm
Nahodha wa zamani wa Borussia Dortmund Philipp Lahm ameteuliwa kuwa mchezaji bora wa msimu uliopita 2016 - 17Picha: picture-alliance/Sven Simon/F. Hoermann

Shirikisho  la  kandanda  la  Ujerumani DFB linakabiliwa  na malipo  ya  kodi  ya  euro milioni 26 kutokana  na uchunguzi kuhusiana  na  malipo  yaliyofanywa  katika fainali za  kombe  la  dunia mwaka  2006.

Katika  ripoti yake  ya  mwisho  kwa  mwaka  2016 , DFB imesema  imefahamishwa  na  mamlaka  ya  kodi kuhusiana  na  mabadiliko ya tathmini ya  kodi  kwa  mwaka 2006 baada  ya  shirikisho  hilo kusema  halikupata  faida kwa  mwaka  huo  na  tathmini  hiyo  kukataliwa. Kutokana na  hilo  shirikisho  la  kandanda  nchini  Ujerumani  DFB litalazimika  kulipa  kiasi  cha  euro milioni  26, imesema ripoti  ya  fedha. Hata  hivyo DFB inaamini  kwamba uamuzi  huo  utabadilishwa  baada  ya  kukata  rufaa.

9. Bildergalerie Tschö Philipp - in seinen Fußstapfen wolltest du aber nicht treten...
Rais wa Bayern Munich Uli Hoeness (kushoto) akiwa na nahodha wa zamani Philip LahmPicha: picture-alliance/GES-Sportfoto

Mabingwa  wa  Ujerumani Bayern Munich wanatarajia kumtangaza  mkurugenzi  wa  spoti  wa  klabu  hiyo  katika muda  wa wiki sita na  kufikisha  mwisho  mwaka  mzima ambapo  nafasi  hiyo  ilikuwa  wazi, amesema  rais  wa klabu  hiyo Uli Hoeness leo Jumatatu. Nafasi  hiyo  ilikuwa wazi  tangu Matthias Sammer  kujiondoa  mwaka  mmoja uliopita. Nahodha  wa  zamani  wa  Bayern Philipp Lahm alionekana  kuwa  mmoja  wa  watu  wanaoweza  kuchukua wadhifa  huo  lakini  alikataa, na  Hoeness hakutaka kuzungumzia  iwapo  mlinda  mlango  wa  zamani  wa Bayern Oliver Kahn ni  mmoja  wa  watu  wanaowania nafasi  hiyo.

 

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre / dpae

Mhariri: Yusuf , Saumu