1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi mbalimbali duniani walaani mashambulio ya Uganda

Kabogo Grace Patricia12 Julai 2010

Mashambulio hayo yamesababisha watu 74 kuuawa na wengine zaidi ya 60 walijeruhiwa.

https://p.dw.com/p/OHVm
Mmoja wa majeruhi wa mashambulio hayo akipatiwa matibabu katika hospitali ya Mulago, Kampala, Uganda.Picha: picture-alliance/dpa

Viongozi mbalimbali duniani wamelaani vikali mashambulio ya mabomu yaliyotokea nchini Uganda na kuwaua kiasi watu 74, wakati watu hao wakitazama fainali za mashindano ya Kombe la Dunia hapo jana katika mikahawa miwili kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Kampala.

Miongoni mwa viongozi waliolaani mashambulio hayo ni Rais Barack Obama wa Marekani ambaye ameahidi kutoa msaada kutokana na tukio hilo ambalo limepoteza pia maisha ya raia mmoja wa Marekani. Msemaji wa Baraza la Usalama la Marekani, Mike Hammer amesema katika taarifa kuwa, Rais Obama amesikitishwa na vifo vilivyotokana na mashambulio hayo na ametuma salamu zake za rambi rambi kwa wananchi wa Uganda. Naye Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Uingereza, William Hague amesema mashambulio hayo yametokea wakati wa tukio lililokuwa likionekana kama maadhimisho ya kusheherekea umoja wa Afrika. Amesema Uingereza itasimama upande wa Uganda kupambana na vitendo hivyo vya kikatili vya kigaidi. Aidha, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle ameyaelezea mashambulio hayo kuwa ni mabaya na ya chuki dhidi ya watu waliokuwa wanaangalia kwa utulivu na amani tamasha la michezo.

Mashambulio hayo yamelaaniwa vikali pia na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ufaransa, Bernard Kouchner na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton. Ethiopia na Somalia pia zimelaani vikali mashambulio hayo ya jana usiku. Aidha Umoja wa Afrika umesema mahsmabulio hayo yameilenga nchi ya Afrika ambayo imekuwa ikiunga mkono jitihada za kufanikisha malengo ya umoja huo. Kamishna wa Umoja wa Afrika wa Amani  na Usalama, Ramtane Lamamra amesema hiyo inadhihirisha kuwa vitendo vya kigaidi havina mipaka na kwamba vinaweza kutokea popote pale ikiwemo Afrika. Kwa upande wake Rais Yoweri Museveni wa Uganda amelaani mashambilio hayo na kuahidi kupambana na wahusika. Akizungumza baada ya kuutembelea mkahawa wa klabu ya mchezo wa Raga ambako bomu moja liliripuka hapo, Rais Museveni alisema watu waliokuwa wanaangalia mpira siyo watu waliopaswa kulengwa. Bomu jingine liliripuka katika mkahawa wa Kiethiopia kilometa nne kutoka kwenye klabu hiyo.

Katika mashambulio hayo watu wengine zaidi ya 60 walijeruhiwa. Viongozi wa Uganda wanahisi kuwa mashambulio hayo yamefanywa na kundi la wanamgambo la al-Shabaab lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda ambalo liko nchini Somalia ambako maelfu ya wanajeshi wa Uganda wako katika kikosi cha Umoja wa Afrika kwa lengo la kuiunga mkono serikali ya mpito ya nchi hiyo. Mapema mwezi huu, kiongozi wa ngazi ya juu wa al-Shabaab alitoa wito wa kufanyika kwa vita vitakatifu vya Jihad dhidi ya nchi zilizoko kwenye kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika. Lengo la mashambulio hayo bado halijajulikana ingawa awali wanamgambo wa Kisomali walitishia kuishambulia Uganda kutokana na nchi hiyo kuwa na wanajeshi wake katika mji mkuu wa Somalia-Mogadishu. Aidha, mashambulio hayo yamefanyika wakati ambapo Uganda inatarajia kuwa mwenyeji wa mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika uliopangwa kufanyika kuanzia tarehe 19 hadi 27 mwezi huu.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE/RTRE)

Mhariri:Abdul-Rahman