1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa APEC waiunga mkono China

11 Novemba 2014

Wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya Nchi za Asia na Pasifiki-APEC, wameahidi kuunga mkono mpango wa kuwepo eneo la biashara huru, uliopendekezwa na China.

https://p.dw.com/p/1DlAE
Viongozi wa APEC katika picha ya pamoja
Viongozi wa APEC katika picha ya pamojaPicha: picture-alliance/dpa/Sergei Ilnitsky

Kauli hiyo ya pamoja imetolewa leo baada ya mkutano wa kilele wa APEC wa siku mbili uliohudhuriwa na wakuu wa mataifa, mjini Beijing. Wanachama 21 wa APEC, wameonyesha dhamira yao katika kuunga mkono mpango wa biashara huru katika eneo la Asia na Pasifiki, unaojulikana kama-FTAAP, hatua kwa hatua kulingana na makubaliano.

Katika tamko lao la pamoja, viongozi wa APEC, wamekubaliana kwamba jumuiya hiyo inapaswa kuchangia zaidi na kwamba FTAAP, itatambulika nje ya APEC, sambamba na mchakato wa APEC. Wamesema APEC ni lazima idumishe masuala yake yasiyofungamana kisheria pamoja na kanuni za ushirikiano wa hiari katika michango yake ya kuitambua FTAAP.

Rais Obama akiwa na viongozi wa TPP
Rais Obama akiwa na viongozi wa TPPPicha: Reuters/Kevin Lamarque

Mpango huo wa biashara huru wa FTAAP, umekuwa ukipigiwa debe na China na baadhi ya mataifa yanauona mpango huo kama mbinu ya kuepukana na makubaliano ya mpango tofauti wa ushirikiano wa biashara unaojulikana kama Trans-Pacific, TPP, ambao unaungwa mkono na Marekani lakini haiuhusishi China.

Rais Xi Jinping wa China amekuwa akisisitiza kuhusu mpango huo, huku mazungumzo ya leo yakiwa na lengo la kupunguza tofauti zao kuhusu kufungua biashara huru kwenye eneo la Asia na Pasifiki lenye uwezo mkubwa kibiashara.

Kivuli cha wasiwasi wa kisiasa na kibiashara chatawala mkutano

Miongoni mwa viongozi waliohudhuria mkutano huo unaofikia kilele chake leo unaoongozwa na China, ni pamoja na Rais Barack Obama wa Marekani na Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe, viongozi wa mataifa yenye uchumi mkubwa duniani. Hata hivyo, mkutano huo umefanyika huku kukiwa na wasiwasi wa kisiasa na kibiashara.

Rais Obama amesema kuwepo kwa China ambayo ina mafanikio, ni kwa ajili ya maslahi ya Marekani na dunia, lakini serikali ya China pia inapaswa iwe mshirika katika kujenga mfumo wenye utulivu wa kimataifa.

''China na Marekani zinaweza kufanya kazi pamoja na dunia itafaidika. Na hicho ni kitu ambacho watazamaji wanavutiwa nacho. Tunaendelea kufanya kazi ya kuimarisha biashara kati ya nchi zetu na uwekezaji kati ya nchi zetu mbili, alisema Rais Obama.''

Rais Obama akisalimiana na Rais Xi
Rais Obama akisalimiana na Rais XiPicha: Reuters/K. Kyung-Hoon

Marekani imekuwa ikishinikiza kuwepo kwa mpango wa TPP, kwa lengo la kupunguza masharti ya kibiashara. Aidha, wakati wa kikao cha ufunguzi, Rais Jinping aliuambia mkutano huo kuwa APEC inapaswa kuondoa vizuizi vya kibiashara katika eneo la Asia na Pasifiki.

China na Marekani zimeonyesha kuwa huenda zikawa na msimamo wa pamoja, huku Ikulu ya Marekani ikitangaza kuwa nchi hizo mbili zimefikia makubaliano ya kupunguza ushuru katika biashara ya teknolojia ya habari. Baadaye leo, Rais Obama atakutana na Rais Jinping.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/ AFPE,RTRE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman