1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wimbi la wakimbizi limepita makadirio

5 Novemba 2015

Kuna ishara ya kupatikana maridhiano kati ya vyama vinavyounda serikali ya muungano kuhusu sera ya pamoja ya wakimbizi. Kansela Merkel anautaka Umoja wa Ulaya ubuni sera mpya kuhusu kinga ya ukimbizi.

https://p.dw.com/p/1H0jB
Kituo cha kuwaandikisha wakimbizi mjini BerlinPicha: Getty Images/S. Gallup

Kabla ya duru mpya ya mazungumzo, wakuu wa vyama vinavyounda serikali kuu ya muungano mjini Berlin, kansela Angela Merkel wa chama cha Christian Democratic Union- CDU, mwenyekiti wa chama ndugu cha Christian Social Union-CSU-Horst Seehofer na mwenyekiti wa chama cha Social Democratic SPD,Sigmar Gabriel wamedhihirisha azma ya kufikia maridhiano haraka kuhusiana na suala la wakimbizi. Baada ya mkutano wao ulioshindwa kuleta tija jumapili iliyopita,vyama vinavyounda serikali kuu ya muungano vinakabwa na shinikizo kubwa.Kansela Merkel amekwepa kusema mengi kuhusu uwezekano wa kufikiwa maridhiano katika duru ya mazungumzo itakayofanyika baadae hii leo katika ofisi ya kansela mjini Berlin."Wote wanataka tufikie ufumbuzi wa maana. Tutaangalia kama tunaweza kufikia maridhiano,na kama tutashindwa basi tutabidi kuendelea na mazungumzo.Haitakuwa mara ya kwanza kufanya hivyo" amesema kansela Merkel.

Maridhiano yawe ya maana na sio ya kijuu juu

Sigmar Gabriel anategemea makubaliano yatapatikana. Ameliambia gazeti la Bild tunanukuu:"SPD,CDU na CSU bila ya shaka watatoa pendekezo la pamoja kama wanavyotarajia wananchi kutoka kwetu.Ndio maana tunabidi tukubaliane."Mwenyekiti huyo wa SPD amesisitiza hata hivyo kwa kusema watakachokiamua kinabidi kiwe imara na ambacho kitaweza kutekelezeka na sio maridhiano ya kijuu juu akimaanisha vituo vya muda vutakavyowekwa nje ya mpaka wa Ujerumani ,vitakavyokuwa na jukumu la kuwachuja wale wenye nafasi ya kukubaliwa kinga ya ukimbizi na wengine ambao wakikataliwa watabidi warejeshwe haraka walikotokea.

Berlin Bundeskanzleramt Seehofer Gabriel Merkel Spitzentreffen zu Flüchtlingen ARCHIV
Kansela Angela Merkel,mwenyekiti wa SPD Sigmar Gabriel na mwenzake wa CSU Horst Seehofer katika mkutano wao wa kilele kuhusu wakimbizi mjini BerlinPicha: picture-alliance/dpa/W. Kumm

Wimbi la wakimbizi halina dalili ya kupungua;Umoja wa ulaya unaashiria wakimbizi milioni tatu zaidi wanaweza kuingia katika jumuia hiyo ya mataifa 28 hadi ifikapo mwaka 2017.

Idadi ya wanaomba kinga ya ukimbizi ni kubwa kupita kiasi

Wakati huo huo wizara ya mambo ya ndani ya Ujerumani imesema watu laki 780 000 wameomba kinga ya ukimbizi humu nchini kuanzia january hadi octoba mwaka huu.Thuluthi moja ya watu hao wanatokea Syria.Mwezi wa Octoba tu wahamiaji 181.000 waliomba kinga ya ukimbizi wakipindukia kwa namna hiyo rikodi ya watu 161 000 kwa mwezi waliosajiliwa mwezi wa septemba uliopita.Jumla ya wakimbizi milioni moja wanatarajiwa kuomba kinga humu nchini mwaka huu idadi inayowafanya maafisa wa serikali za miji,mikoa na majimbo kupata shida ya kuwahudumia ipasavyo.

Österreich Grenze Deutschland Kollerschlag Transitzelt
Eneo la mpakani Kati ya Ujerumani na Austria ambako wakimbizi wanaandikishwa wakiwa ndani ya mahema ya mudaPicha: picture-alliance/dpa/D. Scharinger

Ujerumani imeanza pia kusaka njia za kuzuwia wimbi la wakimbizi kutoka Afghanistan."Kuna idadi kubwa ya raia wa tabaka la kati wanaotokea pia Kabul na tumekubaliana na serikali ya Afghanistan kwamba vijana wa kiafghani wanaotokea katika familia zinazojimudu wanastahiki wasalie nchini na kuijenga nchi yao" amesema waziri wa mambo ya ndani wa serikali kuu ya Ujerumani Thomas de Maizière.Wakimbizi 31.000 wa Afghanistan wameomba kinga ya ukimbizi nchini Ujerumani mwezi uliopita wa Octoba.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/afp/dpa

Mhariri:Yusuf Saumu