1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa dunia wataka ugaidi wa nyuklia uzuiwe

27 Machi 2012

Viongozi wanaohudhuria mkutano wa kilele kuhusu nyuklia mjini Seoul wametoa wito kila la kufanya lifanywe tangu katika ngazi ya kitaifa mpaka ya kimataifa kuepukana na balaa la ugaidi wa kinyuklia.

https://p.dw.com/p/14Sju
Viongozi katika mkutano wa kilele wa SeoulPicha: AP

Ugaidi wa kinyuklia bado ni kitisho kikubwa zaidi kwa usalama wa kimataifa,wamesema katika taarifa yao ya mwisho, wajumbe 53 wanaoshiriki katika mkutano huo wa kilele katika mji mkuu wa Korea ya kusini-Seoul,akihudhuria pia rais Barack Obama wa Marekani.

Ili kuepukana na kitisho hicho panahitajika hatua kali- kitaifa na ushirikiano wa kimataifa kutokana na madhara yake tangu kisiasa,kiuchumi,kijamii na kisaikolojia-taarifa hiyo imesema.

Taarifa hiyo ya mwisho haikufafanua hatua zinazobidi kuchukuliwa badala yake imeelezea malengo ya pamoja ya kuepukana na silaha za kinyuklea,kutosambazwa silaha hizo na kuhakikishwa kwamba nishati ya nuklea inatumika kwa mahitaji ya kiraia na kwa amani.

Südkorea Seoul Nukleargipfel Obama
Rais Barack Obama akihutubia mjini SeoulPicha: Reuters

Rais Barack Obama ameshadidia umuhimu wa kuzuwiliwa magaidi kujipatia zana zinazoweza kutumika kutengeneza silaha za kinuklea.

Bila shaka kitisho kingalipo. Bado kuna watu wengi waovu wanaotafuta zana za hatari na zana hizo za hatari bado si salama katika nchi nyingi."Amesema rais Barack Obama.

Wawakilishi wa mataifa 53 wanaohudhuria mkutano huo wa Seoul wametilia mkazo jukumu la kila nchi, kuambatana na masharti yaliyowekwa kitaifa na kimataifa kuhakikisha usalama wa zana zote za kinuklea ili kuepusha zisiangukie mikononi mwa makundi ya wahalifu.

Wawakilishi mkutanoni wanasema hatua hizo zilizolengwa kuimarisha usalama si pingamizi kwa haki za mataifa kutengeneza na kutumia nishati ya kinuklea kwa lengo la amani.

Wameelezea pia umuhimu wa kuhifadhiwa shehena ya maadini ya Uranium yaliyorutubishwa pamoja na yale ya Plutonium - aina mbili za maadini yanayotumiwa kutengeneza silaha za kinuklea.

Taarifa ya mwisho inazisihi nchi, zitangaze kwa khiari,ikiwezekana hadi ifikapo mwaka 2013, hatua zilizochukuliwa ili kupunguza matumizi ya maadini yaliyorutubishwa ya Uranium.

Belgien EU Terror Anti-Terror-Koordinator der Europäischen Union Gilles de Kerchove
Msimamizi wa tume ya Umoja wa Ulaya ya kupambana na ugaidi Gilles de KerchovePicha: AP

Mbali na mataifa hayo 53, mkutano wa Seoul umehudhuriwa pia na viongozi wa ngazi za juu wa mashirika ya kimataifa: Interpol, Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa.

Mkutano watatu wa aina hii, baada ya ule wa Washington mwaka 2010 na huu wa Seoul, utafanyika mwaka 2014 nchini Uholanzi.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman