1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

G7: Viongozi kuongeza fedha za kukabiliana na hali ya hewa

Zainab Aziz Mhariri: Saumu Njama
13 Juni 2021

Viongozi wa nchi saba tajiri duniani za G7 wanatarajiwa kutangaza leo Jumapili kuhusu kuongeza michango yao ya fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

https://p.dw.com/p/3uonF
G7-Gipfel in St Ives 2021
Picha: Koji Ito/Yomiuri Shimbun/picture alliance

Rais wa Marekani Joe Biden na wenzake wanatarajiwa kuahidi msaada wa dola bilioni 100 kwa nchi zinazoendelea kwa ajili ya kupunguza uzalishaji wa hewa chafu ya kaboni na kukabiliana na ongezeko la joto ulimwenguni.

Nchi saba tajiri duniani za G7 zinaunga mkono hatua za pamoja za kukabili athari za mabadiliko ya tabia nchi kabla ya mkutano wa Umoja wa Mataifa utakaojadili swala la mabadiliko ya tabia nchi COP26 utakaofanyika nchini Scottland mnamo mwezi Novemba.

Kushoto: Kansela wa Ujerumani Angela Merkel. Kulia: Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson
Kushoto: Kansela wa Ujerumani Angela Merkel. Kulia: Waziri Mkuu wa Uingereza Boris JohnsonPicha: Stefan Rousseau/picture alliance/dpa

Kama sehemu ya mipango ya kuharakisha upatikanaji wa fedha za miradi ya kuimarisha miundombinu katika nchi hizo zinazoendelea na kuziwezesha kuingia kwenye matumizi ya teknolojia mbadala na endelevu, nchi hizo saba tajiri kwa mara nyingine tena zitaahidi kufikia lengo.

Nchi zilizoendelea zilikubaliana katika Umoja wa Mataifa mnamo mwaka 2009 kwa pamoja kuchangia dola bilioni 100 kila mwaka hadi ifikapo mwaka 2020 kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa hasa katika nchi masikini, ambazo nyingi zinakabiliwa na kuongezeka kwa kina maji katika bahari, dhoruba na ukame yoteb haya yakiwa yanachochewa na mabadiliko ya tabia nchi.

Lengo hilo halikutimizwa, sababu moja wapo ikiwa ni janga la maambukizi ya virusi vya corona. Janga la corona liliilazimisha serikali ya Uingereza kuahirisha mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP26) hadi mwezi Novemba mwaka huu.

Waandamanaji wanaotetea mazingira katika barabara za Falmouth, Cornwall, Uingereza
Waandamanaji wanaotetea mazingira katika barabara za Falmouth, Cornwall, UingerezaPicha: Oli Scarff/Getty Images/AFP

Uingereza inatumia nafasi yake ya kuwa mwenyeji wa mkutano wa G7 kuhamasisha washirika wake kabla ya mkutano wa COP26 utakaofanyika mwezi Novemba mjini Glasgow, Scottland wakati ambapo shinikizo kubwa linatolewa na makundi ya kutetea mazingira yanayomtaka Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson kuufanya mkutano huo uonyeshe dhamira ya kweli.

Waandamanaji wa kutetea mazingira wamlaumu Boris Johnson

Makundi hayo ya watetezi wa mazingira nchini Uingereza yamemlaumu Waziri Mkuu Boris Johnson, wakisema mwenyeji huyo wa mktano wa viongozi wa G7, hana jipya bali alikuwa anarudia tu ahadi za zamani na kwamba hawatakubaliana na matamko matupu mpaka mataifa yanayokusudiwa yapate pesa.

Mkurugenzi wa asasi ya Greenpeace nchini Uingereza, John Sauven, amesema mataifa tajiri yanatakiwa kuheshimu ahadi zao na amemlaumu Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson kwa kushindwa kuweka mikakati madhubuti kuhusu hali ya hewa na ya kukabiliana na dharura zinazosababishwa na majanga ya asili nchini humo.

Wakati mkutano huo ukiendelea mamia ya watu wameandamana kwa lengo la kuwakumbusha viongozi hao wa G7 pamoja na vyombo vya habari juu ya umuhimu wa kuyalinda mazingira.

Kushoto: Rais wa Marekani Joe Biden. Kulia: Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson
Kushoto: Rais wa Marekani Joe Biden. Kulia: Waziri Mkuu wa Uingereza Boris JohnsonPicha: Kevin Lamarque/REUTERS

Max Lawson, mkuu wa sera wa shirika la misaada la Oxfam, amesema wanaharakati wanawataka viongozi wa kundi la G-7 la mataifa ya Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Uingereza na Marekani kuweka mikakati ya kiwango kikubwa cha kupunguza uzalishaji wa gesi chafu na kuzifadhili nchi masikini kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mabadiliko ya tabia nchi na janga la Covid-19, ni mada zilizowekwa juu kabisa kwenye ajenda ya mkutano wa mataifa tajiri uliofanyika wikendi hii katika kaunti ya Cornwall iliopo kusini magharibi mwa Uingereza.

Mkutano huo pamoja ni muhimu kwa Uingereza, ambayo inaandaa mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP26) mwezi Novemba.

Vyanzo:/RTRE/AFP