1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa kiarabu wakamilisha mkutano wao Sirte

Josephat Nyiro Charo29 Machi 2010

Wamtaka rais Obama asibadili msimamo kuhusu makaazi ya walowezi wa Kiyahudi

https://p.dw.com/p/Mgqf
Kiongozi wa Libya Muamar Gaddafi (katikati), kiongozi wa Wapalestina, Mahmoud Abbas na katibu mkuu wa jumuiya ya nchi za kiarabu Amr Mussa (kulia)Picha: picture alliance / dpa

Viongozi wa jumuiya ya nchi za kiarabu wamemaliza mkutano wao mjini Sirte Libya, uliotuwama juu ya amani ya Mashariki ya Kati. Siku ya mwisho ya mkutano huo hapo jana, viongozi hao wa Kiarabu wamefutilia mbali kuanza tena mazungumzo ya kutafuta amani ya Mashariki ya Kati hadi pale Israel itakapositisha ujenzi wa makaazi yote ya walowezi wa Kiyahudi huko Jerusalem Mashariki.

Siku ya mwisho ya mkutano wao wa siku mbili uliofanyika mjini Sirte nchini Libya, viongozi wa jumuiya ya nchi za kiarabu wamemtaka rais wa Marekani, Barack Obama, aendelee kupinga ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi huko Jerusalem Mashariki. Wamemtaka pia awe mwaminifu kwa msimamo wake wa awali kufanya kila jitihada kuzuia ujenzi wa makaazi hayo kwenye ardhi ya Wapalestina ambao ni kikwazo hatari kwa amani ya Mashariki ya Kati.

Mkutano wa mjini Sirte uligubikwa na uamuzi wa Israel mwezi huu kujenga makaazi mapya 1,600 katika eneo linalokaliwa na Waarabu wengi la Jerusalem Mashariki, ambalo Wapalestina wanaliona kama mji mkuu wa taifa lao la baadaye. Juhudi za Marekani kusimamia mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana kati ya Israel na Wapalaestina, zilikwamishwa na hatua hiyo, iliyochukuliwa siku chache baada ya Waarabu kukubali kuyapa nafasi nyengine mazungumzo ya amani.

Akizungumza kwenye mkutano huo, mpatanishi mkuu wa Palestina katika mzozo wa Mashariki ya Kati, Saeb Erakat, amesema

"Waarabu wametilia maanani juhudi za kutafuta amani ya Mashariki ya Kati na wanatuma ujumbe mzito kutoka mkutano huu na hata mikutano mingine. Tabia hii ya Isael haifai na naamini Waarabu sasa wamefikia wakati wa kutathimini mapendekezo yao yote."

Viongozi wa kiarabu pia wamekubaliana juu ya mpango unaojumulisha hatua za kisiasa na kisheria kukabiliana na juhudi za Isael kuugeuza mji wa Jerusalem kuwa wa Kiyahudi na kuahidi kuchanga msaada wa dola milioni 500 za Kimarekani kuimarisha kuwepo kwa Wapalestina mjini humo. Taarifa ya mwisho ya mkutano wa Sirte imesisitiza haja ya kuwa na muda maalum wa kufanyika mazungumzo na kwamba yaanze pale yalipokomea na kwa misingi ya makubaliano yaliyofikiwa kwenye mchakato mzima wa amani.

Kundi la Hamas linaloudhibiti Ukanda wa Gaza, limeukosoa mkutano wa Sirte kwa kushindwa kwenda mbali vya kutosha katika kutoa tamko kuhusu hatua ya Israel kuuzingira ukanda huo. Msemaji wa Hamas, Fawzi Barhum, amesema mkutano huo ulitakiwa kutumia kila aina ya shinikizo la nchi za kiarabu kuitenga Israel. Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kwa upande wake aliwalaumu hapo jana Wapalestina kwa kuzuia mazungumzo ya kutafuta amani.

Kiongozi wa jumuiya ya nchi za kiarabu, Amr Mussa, amewatolea mwito viongozi wa kiarabu wadurusu upya mapendekezo yao iwapo mchakato mzima wa kutafuta amani utavunjika.

Ban Ki Moon in Afghanistan
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-MoonPicha: AP

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon,akizungumza siku ya kwanza ya mkutano wa Sirte hapo Jumamosi amewataka viongozi wa kiarabu waunge mkono mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana yanayosimamiwa na Marekani, huku akisisitiza mji wa Jerusalem hatimaye uwe mji mkuu wa Israel na taifa huru la Wapalestina litakaloundwa.

"Licha ya wasiwasi tulio nao, hakuna njia nyengine mbadala ya mazungumzo ya kufikia suluhisho la mataifa mawili. Bila mazungumzo, kuna hatari ya kujiingiza katika hali ya kukata tamaa na uwezekano wa kuzuka machafuko zaidi kama yale tuliyoshuhudia hivi karibuni."

Viongozi wa nchi za kiarabu wamekubaliana kufany amkutano maalum mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu kujadilia pendekezo la kuifanyiia mageuzi jumuiya hiyo na kuibadilisha kuwa Umoja wa nchi za Kiarabu na kuunda eneo la majirani wa nchi za kiarabu, litakalokuwa wazi kwa nchi ziszo za kiarabu kama vile Uturuki na Iran. Irak itaanda mkutano wa kilele wa jumuiya ya nchi za kiarabu wa mwaka ujao, 2011.

Mwandishi:Josephat Charo/afpe

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed