1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa kimataifa wakusanyika kwa mkutano wa G-8

7 Julai 2009

Viongozi wa mataifa makuu wamekusanyika nchini Italia mkesha wa mkutano wa kilele wa G-8 kundi la nchi nane tajiri zilizoendelea kiviwanda duniani.

https://p.dw.com/p/IikS
Italian Premier Silvio Berlusconi attends a joint press conference with European Union Commission President Romano Prodi, unseen, after their talks Friday, July 4, 2003, in Rome. Berlusconi hosted the EU Commission in the first high-level meeting of Italy's already rocky EU presidency. (AP Photo/Plinio Lepri)
Mwenyeji wa mkutano wa G-8, Rais wa Italia Silvio BerlusconiPicha: AP

Lengo la mkutano wa G-8 ni kuafikiana njia ya kukabiliana na mtikisiko wa uchumi duniani,mabadiliko ya hali ya hewa na ghasia za nchini Iran. Mwenyeji wa mkutano huo, Waziri Mkuu wa Italia Silvio Berlusconi amesema yupo tayari kuwakaribisha viongozi wa nchi nane tajiri zilizoendelea kiviwanda na zile zinazoibuka kiuchumi. Mkutano huo unafanywa katika mji wa LÁquila kaskazini mashariki ya mji mkuu Rome. Lakini matayarisho ya mkutano huo wa siku tatu yalikumbwa na ripoti zinazohusika na maisha binafsi ya Berlusconi na pia wasiwasi kuhusu usalama katika mji wa L Áquila ambako tetemeko la ardhi liliua takriban watu 300 Aprili mwaka huu. na bado kunatokea mitetemeko midogo.

Kawaida mkutano wa kilele wa G-8 huwaleta pamoja viongozi wa nchi nane tajiri zilizoendelea kiviwanda-Italia,Marekani, Kanada,Russia, Japan,Ujerumani,Uingereza na Ufaransa. Lakini mkutano wa juma hili utazijumuisha pia nchi zinazoinukia kiuchumi kama vile China,India na Brazil.Rais wa China Hu Jintao ni miongoni mwa viongozi waliokwishafika huku wengine wakitazamiwa kuwasili leo hii. Rais wa Marekani Barack Obama atawasili Jumatano asubuhi baada ya kumaliza ziara yake mjini Moscow.

Sehemu kubwa ya mkutano wa G-8 utashughulikia mpango wa kuimarisha uchumi duniani uliokubaliwa mwezi wa Aprili wakati wa mkutano wa G-20 mjini London. Kwenye mkutano huo Rais Obama na viongozi wenzake walikubaliana kutoa dola trilioni moja kwa Shirika la fedha la Kimataifa IMF na mashirika mengine ya kimataifa ili kuzisaidia nchi zilizoathirika kiuchumi.

Jana Jumatatu,Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown na Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozywalikuwa na mkutano wao wenyewe kuratibu msimamo wao kwenye mkutano wa L´Aquila. Wamesema kuwa watawasilisha mapendekezo ya kujadili mfumuko wa bei ya mafuta duniani. Sarkozy akaongezea kuwa ulimwengu hauwezi kuvumilia kuona bei ya mafuta ikiyumba.

Na kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa duniani, Brown na Sarkozy watawashinikiza washirika wao katika kundi la G-8 kujitahidi zaidi kupata makubaliano ya kupunguza uzalishaji wa gesi inayochafua mazingira watakapokutana Copenhagen nchini Denmark hapo mwezi Desemba.

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon atakaehudhuria pia mkutano wa L´Aquila, anatazamia kulishinikiza kundi la G-8 kutimiza ahadi zilizotolewa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na msaada kwa nchi za Kiafrika. Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la Financial Times, kundi la G-8 litatoa dola bilioni 12 katika kipindi cha miaka mitatu ijayo kusaidia kuimarisha sekta ya kilimo katika nchi zinazoendelea.Marekani na Japan zitatoa sehemu kubwa ya fedha hizo.

Na kuhusu suala la Iran,viongozi wa magharibi wameeleza waziwazi kuwa mzozo uliozuka nchini humo kufuatia uchaguzi wa rais wa Juni 12 ni mada itakayotanguliza katika ajenda yao. Lakini China na Russia hazipendelei kuliingiza suala hilo katika ajenda ya kimataifa. Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Human Rights Watch,Kenneth Roth amesema Teheran inajaribu kuzilaumu serikali za kigeni kuchochea vurugu zilizozimwa kwa mabavu. Akaongezea kuwa mkutano wa G-8 unapaswa kueleza waziwazi kuwa Iran haiwezi kuwatupia lawama wengine na kwamba wasiwasi kuhusu haki za binadamu, ni suala litakalopewa kipaumbele katika majadiliano ya siku zijazo kati ya kundi la G-8 na Iran.

Mwandishi: P.Martin/RTRE

Mhariri: M.Abdul-Rahman