1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano juu ya mgogoro wa Zimbabwe.

Stäcker,Claus.18 Agosti 2008

Mkutano juu ya mgogoro wa Zimbabwe wamalizika bila ya mafanikio.Lakini matumaini bado yapo.

https://p.dw.com/p/F095
Msuluhishi katika mgogoro wa Zimbabwe,rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini.Picha: AP

Viongozi  wa nchi za  kusini mwa  Afrika wameshindwa kuwaleta  pamoja  rais Mugabe na  kiongozi  wa upinzani Morgan Tsvangirai ili wapatane juu ya kugawana  mamlaka.

Hatahivyo   matumaini ya kufikia suluhisho  nchini  Zimbabwe bado yapo.

Mkutano  wa viongozi  wa  nchi  za jumuiya ya     maendeleo ya kusini mwa Afrika SADC  uliomalizika   mjini Johannesburg  ulishindwa kuzipatanisha pande  za serikali  na  upinzani  juu ya kugawana mamlaka nchini  Zimbabwe.

Rais Robert Mugabe  na  kiongozi  wa upinzani  M.Tvsangirai pia walihudhuria mkutano huo ambapo mpatanishi  rais Thabo Mbeki wa Afrika  Kusini alikuwa na matumaini  ya suluhisho kufikiwa. Hatahivyo Mbeki amesema mazungumzo   yataendelea.

Rais  Thabo  Mbeki pia  ameitaka jumuiya ya   kimataifa  iwe  na subira na isijiingize  katika   mgororo  wa Zimbabwe.

Rais  Mugabe  na kiongozi  wa  upinzani hawakuweza kukubaliana  juu ya kugawana mamlaka  katika  serikali ya umoja nchini Zibmabwe. Pande mbili hizo bado hazijafikia ufafanuzi juu ya madaraka  ya rais na ya waziri mkuu. Hatahivyo  waziri  wa  mambo ya  nje wa Angola  aliehudhuria mkutano  wa   mjini Johannesburg Joao Miranda  amesema tofauti  zilizobakia ni ndogo.  Lakini  pia amesema  kwamba Mugabe  na Tvsangirai bado wanatofautiana juu ya suala  la mamlaka ya  kiutendaji.

Mjumbe  aliekaribu na rais Mbeki amesema miongoni mwa masuala magumu ni iwapo rais Mugabe atakuwa na  mamlaka ya kuwateua  na kuwafukuza  mawaziri,  na kwa muda gani serikali ya mpito itakuwa madarakani.

Chama cha upinzani kinataka kuwepo kwa ibara itakayoeleza wazi kuwa ,ikiwa upande mmoja utajitoa  kwenye  serikali, lazima uchaguzi ufanyike mnamo  kipindi cha siku 90.

Kiongozi wa upinzani Tsvangirai anaamini kuwa ana  haki ya kuwa na mamlaka makubwa  zaidi kutokana  na kushinda katika raundi ya kwanza ya uchaguzi wa  rais. Lakini  chama kinachotawala  Zanu PF. kinasema Mugabe  lazima  atambuliwe  kuwa  rais kutokana  na  kushinda  uchaguzi wa raundi ya pili    ambapo  chama cha upinzani  hakikushiriki.

Akizungumza baada  ya  mkutano huo katibu mkuu wa chama cha upinzani MDC,bwana  Tendai Biti amesema pana ulazima wa kufikia suluhisho   haraka. Amesema upande  wa upinzani una dhamira ya kweli  katika  kuutatua mgogoro wa  Zimbabwe.