1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa nchi za Kiarabu kukutana leo

Kabogo, Grace Patricia30 Julai 2010

Mkutano huo unaofanyika mjini Beirut utawakutanisha viongozi wa Saudi Arabia, Syria na mwenyeji Lebanon.

https://p.dw.com/p/OY1H
Rais wa Syria, Bashar al-Assad (kulia) akiwa na Rais wa Lebanon, Michel Suleiman.Picha: AP

Mkutano mkubwa wa kikanda wa viongozi wa nchi za Kiarabu unafanyika hii leo mjini Beirut, Lebanon wenye lengo la kutuliza wasiwasi uliopo kuhusu ripoti inayotarajiwa kutolewa na Umoja wa Mataifa kuhusu mashitaka rasmi yatakayofunguliwa dhidi ya kundi la Hezbollah kwa kuhusika na mauaji ya Waziri Mkuu wa zamani wa Lebanon, Rafik Hariri, mwaka 2005.

Mkutano huo utakaowakutanisha Rais Michel Sleiman wa Lebanon, Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia na Rais Bashar al-Assad wa Syria unafanyika, licha kuwepo hofu ya kuzuka kwa ghasia kati ya jamii za waumini wa madhehebu ya Suni na Washia nchini Lebanon, iwapo mahakama ya Umoja wa Mataifa inayochunguza mauaji ya Hariri italihusisha kundi la wanamgambo la Hezbollah la jamii ya Washia ambalo linaungwa mkono na Syria, kuhusika na mauaji hayo. Mfalme Abdullah na Rais Assad wanatarajiwa kuwasili kwa pamoja mjini Beirut wakitokea Damascus, Syria na kukutana na Rais Sleiman kabla ya kupata chakula cha mchana pamoja na wajumbe wa serikali ya muungano inayowajumuisha mawaziri watatu kutoka kundi la Hezbollah ambao nao wamealikwa. Bendera za Saudi Arabia na Syria zimekuwa zikipepea kuuzunguka mji huo mkuu wa Lebanon, huku mabango yenye picha za Mfalme Abdullah yakiwa yamesheheni.

Hali ya usalama Beirut

Usalama pia umeimarishwa zaidi kabla ya ziara hiyo, huku vikosi zaidi vya jeshi la polisi na lile la wananchi vikiwa vimetawanywa mjini Beirut na baadhi ya mitaa ikiwa imezingirwa na vikosi hivyo. Mchambuzi wa taasisi ya kimataifa mjini Beirut, Sahar Atrache anasema kuwa ziara hiyo ni kwa ajili ya kutathmini mustakabali wa eneo hilo. Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Assad kuizuru Lebanon, tangu kuuawa kwa Rafik Hariri ambaye ni baba wa Waziri Mkuu wa sasa, Saad Hariri, mauaji ambayo yalififisha uhusiano kati ya Lebanon na Syria. Syria imekuwa ikilaumiwa kwa kiasi kikubwa kwa mauaji hayo ya kiongozi huyo aliyekuwa wa madhehebu ya Sunni, lakini nchi hiyo imekuwa ikikanusha shutuma hizo. Uhusiano kati ya nchi hizo mbili ulirejea tena mwaka 2008 na Saad Hariri ameshazuru Syria mara nne katika kipindi cha miezi minane iliyopita.

Ushawishi wa Syria kwa Hezbollah

Uongozi wa kifalme wa Saudi Arabia unatarajiwa kumshinikiza Rais Assad kutumia ushawishi wake dhidi ya Hezbollah kundi linaloungwa mkono na Syria na Iran kuepukana na ghasia zozote za kidini zitakazofanana na zile zilizotaka kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Lebanon mwaka 2008. Hofu ya kuzuka ghasia mpya ilitokea wiki iliyopita baada ya kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah kusema anajua kuwa uchunguzi unaofanywa na mahakama ya uhalifu ya Umoja wa Mataifa unapanga kuwafungulia mashtaka wanachama wa kundi hilo la Kishia. Kiongozi huyo ameweka wazi kuwa hatokubaliana na suala kama hilo huku akiituhumu mahakama hiyo kwa kuendesha uchunguzi huo kisiasa na Israeli kuwa sehemu ya uchunguzi huo. Kwa upande wake naibu kiongozi wa Hezbollah, Hassan Fadlallah ameliambia shirika la habari la AFP kuwa ziara ya viongozi hao wa Kiarabu ni fursa pekee ya kuonyesha umoja wa mataifa ya Kiarabu.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFP)

Mhariri:Josephat Charo