1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Ulaya wakutana kujadili njia za kukabiliana na mgogoro wa fedha

Mohamed Dahman4 Oktoba 2008

Viongozi wa Ulaya wanakutana leo hii kujaribu kuweka mkakati wa pamoja kukabiliana na mgogoro wa fedha duniani katika mkutano wao mdogo wa viongozi mjini Paris Ufaransa.

https://p.dw.com/p/FTu7
Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa ameitisha mkutano huo wa viongozi juu ya mgogoro wa fedha.Picha: AP

Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa ambaye nchi yake hivi sasa inashikilia urais wa kupokezana wa Umoja wa Ulaya atakuwa mwenyeji wa mkutano huo utakohudhuriwa na viongozi wa Ujerumani,Uingereza na Italia.Ujerumani imelikataa pendekezo lililowasilishwa na Ufaransa la kuwepo kwa mfuko wa euro bilioni 300 kuzipa nguvu benki zenye matatizo.

Ujerumani na Uingereza nchi zote mbili zimekuwa zikikataa kutowa fedha za walipa kodi kwa mfuko huo utakaosimamiwa na Umoja wa Ulaya.Badala yake zimependekeza hatua zichukuliwe kwa kutegemeana na kesi kuokowa taasisi za kifedha.

Viongozi wa Ulaya wanatumai kuwa na msimamo wa pamoja juu ya namna ya kukabiliana na kimbunga hicho cha fedha kilichozushwa na mgogoro wa mabenki ya Marekani kabla ya mkutano wa mawaziri wa fedha wa Kundi la Mataifa Manane yenye maendeleo makubwa ya viwanda duniani utaofanyika mjini Washington wiki ijayo.