1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Ulaya wakutana tena kuiokoa Euro

Admin.WagnerD26 Oktoba 2011

Viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya wanakutana leo mjini Brussels wakitarajiwa kupitisha maamuzi muhimu ya kuutatua mgogoro wa madeni barani Ulaya, lakini wabunge wa Ulaya wanaonekana kupoteza imani na viongozi hao.

https://p.dw.com/p/12zFN
Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk (kushoto) Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais wa Baraza la Ulaya, Herman Van Rompuy.
Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk (kushoto) Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais wa Baraza la Ulaya, Herman Van Rompuy.Picha: picture-alliance/dpa

Katika muda mfupi baina ya vikao viwili vya viongozi wa Umoja wa Ulaya, wabunge wa vyama vya siasa vinavyowakilishwa kwenye Bunge la Ulaya wanajaribu kuelewa jinsi mambo yanavyoendelea.

Sawa na viongozi wa nchi, nyuso za wabunge wa Ulaya pia zinaonyesha hali ya wasiwasi. Wanajiuliza jee kitatokea nini endapo mkutano wa leo utashindwa kupata suluhisho?

Baadhi ya wabunge hao wamefikia umbali wa kuzishuku serikali zao kwamba hazina dhamira ya kweli wala hazijajaribu kupata suluhisho kamili la mgogoro wa madeni.

Wabunge wapoteza matumaini na viongozi wa serikali

Rais wa Bunge la Ulaya, Jerzy Buzek.
Rais wa Bunge la Ulaya, Jerzy Buzek.Picha: dapd

Kiongozi wa wabunge wa chama cha kisoshalisti kwenye Bunge la Ulaya, Martin Schulz, anasema waliyoyaona katika wiki zilizopita na yale wanayoyaona sasa "yamekuwa yanatokea kwa muda wa mwaka mmoja na nusu, sasa barani Ulaya, akimaanisha kuwa hatua kadhaa zinatangazwa lakini hazitekelezwi.

"Mawazo mapya yanajadiliwa, panafikiwa mwafaka, lakini bila ya kutekelezwa. Halafu kinafanyika kikao kingine cha dharura. Kwa kweli sijui, labda tayari pana orodha ya vikao vingine vya dharura." Anasema Schulz.

Zimetolewa lawama kubwa katika Umoja wa Ulaya, kwamba pamefanyika vikao viwili vilivyofuatana ambapo suala lile lile moja ndilo lililojadiliwa, yaani mpishano wa mawazo kati ya Ujerumani na Ufaransa kuhusiana na dhima ya Mfuko Maalum wa Kuiokoa Sarafu ya Euro (EFSF).

Sababu hazikuwa tu tofauti za mitazamo baina ya Ujerumani na Ufaransa kuhusiana na maudhui ya Mfuko huo, bali pia ni kushiriki kwa bunge la Ujerumani katika kuuimarisha Mfuko wenyewe.

Bunge la Ujerumani kumuongezea nguvu Kansela Merkel

Kansela Angela Merkel
Kansela Angela MerkelPicha: dapd

Hapo awali ni kamati ya bajeti ya bunge hilo ndiyo iliyokuwa iamue juu ya Mfuko huo wa madeni. Lakini kwa sababu matumizi ya fedha za mfuko huo ni makubwa sana, ambapo nchi zinapaswa kutoa dhamana kubwa vile vile, sasa Bunge la Ujerumani litapiga kura ili kumpa Kansela Angela Merkel jukumu la kufanya mazungumzo kwenye mkutano wa leo mjini Brussels.

Chama cha Kijani kimehusika sana katika mchakato wa kufikiwa kwa uamuzi huo wa Bunge la Ujerumani kupiga kura. Lakini mwenyekiti mwenza wa chama hicho kwenye Bunge la Ulaya, Rebecca Harms, amesema kuwa serikali ya Ujerumani imepitwa na mambo fulani.

"Angela Merkel hayumo miongoni mwa viongozi wanaoweza kupiga kifua na kusema: 'Katika mgogoro huu tunapaswa kuchukua hatua za kijasiri, hata ikiwa na maana ya kushindwa katika uchaguzi.'" Amesema Harms, akitaka pawepo uwazi katika kuushughulikia mgogoro huu wa madeni.

Mbunge wa chama cha Waliberali, Guy Verhofstadt, amesema lazima viongozi wa Umoja wa Ulaya wachukue hatua ya kuongeza fedha kwa kiwango kikubwa katika Mfuko huo, "ili kuyapa masoko uhakika na ili kuiwezesha Benki ya Ulaya (CBE) kuendelea kuzinunua dhamana za nchi zilizolemewa na madeni."

Mwandishi: Christoph Hasselbach/DW
Tafsiri: Abdu Mtullya
Mhariri: Oummilkheir Hamidou