1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa ulimwengu wamuomboleza Mikhail Gorbachev

31 Agosti 2022

Viongozi wa dunia wameendelea kutuma risala za rambirambi kumuomboleza Mikhail Gorbachev, kiongozi wa mwisho wa uliokuwa Umoja wa Kisovieti aliyeaga dunia usiku wa Jumanne mjini Moscow Urusi akiwa na miaka 91.

https://p.dw.com/p/4GGnt
Michail Gorbatschow tot
Picha: Boris Yurchenko/AP/dpa/picture alliance

Marehemu Mikhail Gorbachev aliyekuwa na mchango mkubwa katika kumaliza Vita Baridi, alisifiwa na kutajwa kama ‘kiongozi adimu' aliyesaidia kubadilisha historia ya ulimwengu.

Akimuomboleza na kutoa rambirambi nyingi kwa familia na marafiki, Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema Gorbachev alikuwa mwanasiasa na mzalendo aliyekuwa na mchango mkubwa katika historia ya ulimwengu. Kwamba aliiongoza nchi hiyo katika kipindi cha mabadiliko magumu. Putin ameongeza kuwa Gorbachev alielewa kwa undani kwamba mageuzi yalihitajika, hivyo alijitahidi kutoa suluhisho lake mwenyewe kuyatatua matatizo ya dharura.

Mikhail Gorbachev, Mrusi anayependwa zaidi na Wajerumani afariki dunia

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier, amesema Ujerumani ina shukrani nyingi kwake kufuatia uamuzi wake madhubuti kuelekea muungano wa zilizokuwa Ujerumani mbili.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz pia alisifia alama ambazo Gorbachev ameacha katika uso wa ulimwengu kufanikisha demokrasia hususan Urusi na Ulaya. Hata hivyo amesikitika kwamba amefariki wakati demokrasia imefeli nchini Urusi.

Kansela wa zamani wa Ujerumani Helmut Kohl (kulia) na Mikhail Gorbachev, rais wa zamani wa uliokuwa muungano wa Soviet wakipanda miti kuadhimisha miaka 15 ya muungano wa Ujerumani Oktoba 3, 2005.
Kansela wa zamani wa Ujerumani Helmut Kohl (kulia) na Mikhail Gorbachev, rais wa zamani wa uliokuwa muungano wa Soviet wakipanda miti kuadhimisha miaka 15 ya muungano wa Ujerumani Oktoba 3, 2005.Picha: picture-alliance/dpa/dpaweb/epa/M. Hanschke

"Alikuwa mwanamageuzi jasiri na kiongozi aliyethubutu mambo mengi. Hatutasahau kwamba mageuzi ya enzi hizo yaliwezesha kuanzisha demokrasia nchini Urusi na kwamba demokrasia na uhuru viliwezekana katika Ulaya, kwamba Ujerumani ikaweza kuunganishwa, na Pazia la Chuma likatoweka," amesema Scholz.

Rais wa Marekani Joe Biden amemtaja marehemu kama kiongozi adimu aliyekuwa na maono ya kuweza kuuona mustakabali tofauti wa dunia, na akaitoa muhanga kazi yake kuyatimiza.

Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka uliopita Dmitry Muratov alimsifu mshindi huyo mwenzake wa Nobel kama mtu aliyezipa kipaumbele haki za binadamu kuliko masuala ya taifa na alithamini amani kuliko madaraka.

Miaka 150 ya chama cha SPD

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amemuelezea Gorbachev kama kiongozi aliyebadilisha mkondo wa historia ya dunia.

Michail Gorbatschow (wa pili kulia) pamoja na rais wa zamani wa Marekani Ronald Reagan (pili kushoto) wakisalimiana wakati Oktoba 11, 1986.
Michail Gorbatschow (wa pili kulia) pamoja na rais wa zamani wa Marekani Ronald Reagan (pili kushoto) wakisalimiana wakati Oktoba 11, 1986.Picha: Ron Edmonds/AP Images/picture alliance

Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen alimmiminia sifa kama kiongozi aliyeaminika na kuheshimiwa, aliyefungua milango kwa Ulaya iliyo huru.

Katibu mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg amesema yaliyokuwa maono ya Gorbachev ya ulimwengu mzuri yanasalia kama mfano na kupongeza mageuzi yake ya kihistoria yaliyowezesha ushirikiano kati ya Urusi na NATO.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amemtaja marehemu kama mtu wa amani aliyefungua milango kwa uhuru wa Urusi.

Kulingana na taarifa ya hospitali ya mjini Moscow, Gorbachev amekufa baada ya kuugua kwa muda mrefu, lakini taarifa hiyo haikueleza zaidi. Soma: Kiongozi wa mwisho wa Kisovieti Mikhail Gorbachev afariki

Shirika la habari la Urusi, TASS, limesema kiongozi huyo atazikwa  katika makaburi ya heshima kubwa ya Novodevichy mjini Moscow.

(Vyanzo: AFPE; RTRE)

Tafsiri: John Juma

Mhariri: Mohammed Khelef