1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Umoja wa Ulaya waanza mkutano

28 Juni 2012

Viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya wanakutana Brussels, Ubelgiji, kupitisha maamuzi juu ya mikakati ya kukuza uchumi. Hata hivyo kuna matumaini madogo tu ya kupatikana suluhisho la kupunguza madeni.

https://p.dw.com/p/15N91
Francois Hollande na Angela Merkel
Francois Hollande na Angela MerkelPicha: Reuters

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ndiye kiongozi anayeonekana kuwa wa muhimu zaidi katika mkutano wa Umoja wa Ulaya utakaofanyika kwa siku mbili. Viongozi wengi wa nchi za umoja huo wanaliunga mkono wazo la kuwapo kwa hati za dhamana ya fedha kwa ajili ya kulitatua tatizo la uchumi katika kanda inayotumia sarafu ya euro kwani hati hizo zitashusha kiasi cha riba ambacho nchi zinazotaka kukopa fedha zitapaswa kulipa. Lakini Kansela Merkel ana wasiwasi kuwa kuwapo kwa hati hizo kutapunguza shinikizo dhidi ya nchi kama Ugiriki na Uhispania zinazopswa kubadili sera zake za uchumi.

Kwa sasa mfuko wa kuleta ukuaji wa kiuchumi na kwa njia hiyo kuongeza kodi katika nchi zinazotumia sarafu ya euro una kiasi cha euro billioni 130 na unatarajiwa kujumuisha kwa sehemu kubwa fedha ambazo awali zilikuwa zimewekwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo. Viongozi wa nchi za Itali, Ufaransa na Uhispania wanaiwekea shinikizo Ujerumani ili  ikubaliane na mpango wa nchi za Euro kugawana madeni yake. Wakuu wa Umoja wa Ulaya pamoja na Shirika la Kimataifa la Fedha IMF nao wametoa maoni hayo.

Waziri Mkuu wa Itali, Mario Monti
Waziri Mkuu wa Itali, Mario MontiPicha: dapd

Hollande aendelea kupinga mpango wa kubana matumizi

Wawekezaji katika masoko ya hisa wanataka maamuzi juu ya kushirikiana kupunguza madeni yafikiwe wiki hii ili mgogoro wa uchumi wa nchi zinazotumia sarafu ya euro usipanuke zaidi na kuikumba dunia nzima. Hata hivyo wawekezaji hawatarajii kwamba maamuzi kamili yatapitishwa wiki hii.

Kikwazo kikubwa kinaonekana kuwa Kansela Angela Merkel. Mara kwa mara kiongozi huyo ameeleza kuwa suluhu za muda mfupi kama vile suala la kugawana madeni au kuwa na benki kuu ya Ulaya yenye kupewa majukumu mengi zaidi hazina maana yoyote iwapo serikali za nchi husika hazitoonyesha uwezo wa kusimamia bajeti za nchi zao kikamilifu.

Mabenki ya Uhispania yameomba msaada wa fedha
Mabenki ya Uhispania yameomba msaada wa fedhaPicha: picture-alliance/dpa

Kwa upande wake, rais wa Ufaransa Francois Hollande, anaupinga mpango wa Merkel wa kubana matumizi kama namna ya kuutatua mgogoro wa sarafu ya euro. Hollande pamoja na waziri mkuu wa Itali Mario Monti, wameeleza kuwa ni bora fedha kutoka katika mfuko wa uokozi wenye kiasi cha euro billioni 500 zitumike kwa ajili ya kuyasaidia mabenki ya Uhispania au kununua hati za dhamana ya fedha kutoka katika nchi ambazo zinalazimika kulipa kiasi kikubwa cha riba pale zinapotaka kukopa. Lakini Merkel analipinga kabisa wazo la kuyapa fedha mabenki yaliyo katika mgogoro wa kiuchumi au nchi zinazishindwa kuendesha vizuri uchumi wake.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/AP/Ap

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman