1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa umoja wa Ulaya wakutana leo

Sekione Kitojo27 Oktoba 2010

Viongozi wa kitaifa na serikali wa umoja wa Ulaya wanaanza kikao chao muhimu leo mjini Brussels.

https://p.dw.com/p/PqOp
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy.Picha: AP

Viongozi  wa  kitaifa  wanakabiliana   na   maswali  tete  leo Alhamis  iwapo  wachukue  uamuzi   wa  kuandika  upya mkataba  wa Lisbon, unaoweka  pamoja  mataifa  ya Umoja  wa  Ulaya   katika  juhudi  za  kuzuwia  mzozo mpya  wa  madeni.

Ujerumani  inatarajiwa  katika   mkutano  huo    wa  siku mbili   mjini   Brussels  , kutoa  hoja   kuwa   mkataba  wa Lisbon  unahitaji  kufanyiwa  marekebisho   iwapo  umoja wa  Ulaya  utalazimika kubana  uendeshaji  wa  masuala  ya kifedha   katika   mipaka  yake  ya    ndani,  baada  ya kutokea   mzozo  wa  madeni  mwaka  huu  nchini  Ugiriki.

Ujerumani  inaungwa  mkono  na  Ufaransa,  ambayo imefanikiwa  kupata  maridhio  muhimu  kutoka  kwa serikali  ya   kansela  Angela  Merkel  mjini  Berlin  na kukubali  kulegeza  adhabu   dhidi  ya  zile  nchi zitakazoshindwa  kutimiza  malengo  yaliyowekwa  ya viwango  vya  madeni  katika   bajeti  zao. Ufaransa inataka   adhabu  zisitolewe  papo  kwa  hapo  na  kwamba zitolewe   baada  ya  kupigiwa  kura.

Lakini   makubaliano  baina   ya  Merkel  na  rais  Nicolas Sarkozy  wiki  iliyopita  yamezusha   wimbi  la  upinzani. Hususan  kuna  hofu  ya  kurejewa   kwa  matatizo yaliyojitokeza    na  hatimaye  kuhitajika  kufanya  kazi  ya ziada  kuweza  kuupitisha   mkataba  huo  wa  Lisbon, ambao  ulichukua  miaka  nane  kuweza   kuuidhinisha baada  ya  kampeni  zilizoshindwa  za  kura  ya  maoni nchini  Ufaransa, Uholanzi  na  Ireland.

Wiki  hii  watendaji  wakuu  waandamizi  wa  umoja  wa Ulaya , kamishna  wa  masuala  ya  uchumi  Olli  Rehn  na kamishna  anayehusika  na   sera  za  mambo  ya  kigeni Viviane Reding, kila  mmoja   alipinga  vikali  madai  ya Ujerumani.

Griechenland Finanzkrise
Kamishna wa masuala ya kiuchumi wa umoja wa Ulaya Olli Rehn.Picha: picture alliance/dpa

Kuingilia  kwao  kati  kulifuatia  mlolongo  wa  matamshi  ya upinzani  kutoka   mataifa  mengine  na  hofu  kuwa mipango  ya kuuandika  upya  mkataba  huo  inaweza kusababisha  baadhi  ya  mataifa  miongoni  mwa wanachama  27  kujitokeza  katika  mkutano  wa  leo  na orodha  mpya   ya  madai  ambayo  hayahusiki.

Waziri  mkuu  wa  Uingereza  David  Cameron , kwa  mfano , tayari  amekwisha  eleza   kuwa  anataka   kundi  hilo  la mataifa  kuunga  mkono  wito  wake  wa   kuzuiwa  kabisa kwa  bajeti  ya  umoja  wa  Ulaya  kwa  mwaka  2011.

Mabishano  hayo  yanaleta  utata, wakati  utayari  wa Ufaransa  kuangalia  uwezekano  wa  mabadiliko  katika mkataba  huo  ukijionesha.

Ufaransa  pamoja  na  mambo  mengine  inataka  mfuko wa  fedha  za   mikopo  ya  dharura  ya  miaka  mitatu  ya muda  kwa   ajili  ya  mataifa   ambayo  yanashindwa kujimudu  kifedha, kubadilishwa  na  kuwa  mfuko  wa kudumu  unaoshughulikia   mizozo  ya  kifedha.

Kuufanya  mfuko  huo  kuwa wa  kudumu  kunahitaji  mkataba huo kubadilishwa  kutokana  na  vipengee  vya  katiba  ya Ujerumani. Iwapo  Ujerumani  haitafanikiwa  kupata  kile inachotaka , inaweza  kuleta  hatari  ya  kuuweka  katika hali  ya  wasi  wasi  muundo  na  sura  ya  mfuko  kama huo  wa  usalama  wa  kifedha,  unaozuwia  kusambaa  kwa hali  ya  madeni  katika  nchi  zinazotumia   sarafu  ya euro.

Hatari  kwa  Ufaransa   na  udhaifu  wa  mataifa yanayotumia  sarafu  ya  euro  kama  Ireland, Ureno , ama hata  Ubelgiji, ni  kwamba  Ujerumani  haitaweza  kutoa fedha  nyingi  tena   hapo   siku  za  baadaye   hadi  pale itakapopata  uhakika  wa  kisheria  inaoutaka   kuweza kupambana  na  upinzani  wa  kisiasa  nchini  mwake.

Maoni  ya   wapiga  kura  nchini  Ujerumani  yameeleza upinzani  mkubwa   dhidi ya kugharamia  makosa  ya  kibajeti  ya mataifa   washirika    wa  euro.

Merkel  kimsingi  anataka  kuwatwika mzigo  mdogo  zaidi   walipa kodi  wa  taifa  hilo  na  anataka  kuhusika  zaidi  na  zaidi kwa   mabenki  ya  binafsi.

Duru  katika  serikali  ya  Ujerumani  zinasema   kuwa kansela  anazungumza  na  kila  kiongozi  kwa  hivi  sasa.

Mwandishi  :  Sekione  Kitojo  / AFPE

Mhariri :  Josephat  Charo.