1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Umoja wa Ulaya warekebisha mkataba wa Lisbon.

17 Desemba 2010

Mkakati wa kudumu katika Umoja wa Ulaya utaanza kutekelezwa 2013.

https://p.dw.com/p/QeBr
Rais wa Umoja wa Ulaya, Herman van Rompuy amesema watahakikisha sarafu ya Euro haianguki.Picha: DW/Samir Huseinovic

Viongozi wa mataifa ya Umoja wa Ulaya wamekubaliana kuweka mkakati wa kudumu kuhakikisha kuna uimara kifedha kuanzia mwaka wa 2013.

Viongozi wa mataifa 27 wamesema msisitizo wa mkakati wa Ujerumani wa kusitisha mzozo wa kiuchumi kwa muda mrefu, utakaoongezwa katika mkataba wa Lisbon unaotumiwa kuuongoza Umoja wa Ulaya, utafaa ikiwa utalenga kuhakikisha uimara wa sarafu ya Euro kwa ujumla.

Viongozi hao pia walikubaliana kwamba kuna haja ya kuongeza hazina ya sasa ya kusaidia kuyakwamua mataifa yatakayolemewa kiuchumi ingawa wachunguzi wachache wanadai haitatosheleza ikiwa Uhispania na Ureno zitahitaji kusaidiwa na Umoja huo na Shirika la fedha duniani, IMF.

Rais wa Umoja wa Ulaya, Herman von Rompuy alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kuongoza siku ya kwanza ya mkutano mjini Brussels, alisema wako radhi kuhakikisha sarafu ya Euro haianguki. Na kwamba ukakamavu wao ni wa wazi kuwa viongozi wa nchi na serikali katika kanda ya Euro wako tayari kufanya lolote litakalohitajika kuhakikisha uimara wa kanda inayotumia sarafu ya Euro kwa ujumla.

Benki kuu ya Umoja wa Ulaya, ambayo inasimamia sera ya fedha katika mataifa 16 yanayotumia sarafu ya Euro, itaongeza kiwango chake cha mtaji hadi Euro bilioni 10.76 ili kukabiliana na kitisho cha madeni na uimara wa masoko. Mataifa wanachama yatachangia kupata fedha hizo.

Rais wa benki hiyo kuu, Jean-Claude Trichet, aliwaambia waandishi habari kwamba baraza la uongozi katika benki hiyo, linadhani ni muhimu kuongeza kiwango cha mtaji.

Mkurugenzi mkuu wa shirika la fedha duniani, Dominique Strauss-Kahn ambaye amekuwa akiwakosoa viongozi wa Umoja wa Ulaya kwa kuchukua hatua za polepole za kukabiliana na mzozo wa kiuchumi, amesema ana wasiwasi na hali ya uchumi barani Ulaya ambayo inaimarika kwa mwendo wa kinyonga.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya ambao wanakutana kwa mara ya saba mwaka huu, walipitisha kuongezwa kwa sentensi mbili ya mabadiliko katika mkataba wa Lisbon baada ya shinikizo la Ujerumani ya kuwa na mkakati madhubuti wa kukabiliana na mizozo ya kiuchumi kuanzia mwezi Juni mwaka wa 2013.

Umoja wa Ulaya pamoja na shirika la fedha duniani, IMF zilitenga Euro bilioni 750 katika hazina itakayotumiwa kuyasaidia mataifa katika kanda ya Euro yatakayolemewa na tatizo la madeni siku zijazo.

Huku hayo yakijiri, sarafu ya Euro iliimarika dhidi ya Dola barani Asia wakati ambapo wawekezaji wakisubiri matokeo ya mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels. Sarafu ya Euro ilibadilishwa kwa Dola 1 na senti 33 kutoka Dola 1 na senti 32 mjini Tokyo, Japan.

Mwandishi: Peter Moss /Reuters/AFP

Mhariri: Josephat Charo.