1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongoz wa ulimwengu waomba utulivu Libya

10 Juni 2015

Viongozi wa kimataifa wamekutana mjini Berlin, hapa Ujerumani, na kutoa taarifa ya pamoja wakitoa wito wa kusitishwa mapigano nchini Libya na kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa

https://p.dw.com/p/1Fehe
Pressekonferenz Steinmeier Leon Libyen
Picha: Getty Images/Afp/O. Andersen

Serikali za China, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Urusi, Uhispania, Uingereza, Marekani na Umoja wa Ulaya wamesisitiza nia yao ya pamoja ya kufanya kazi na Libya yenye amani na umoja.

Msaada utakaotolewa na jumuiya ya kmataifa ni pamoja na vita dhidi ya ugaidi na uhalifu wa kupangwa, kusaidia katika suala la uhamiaji usio na mpango maalum, kuziimarisha taasisi za Libya na kuisaidia nchi hiyo kujikwamua kijamii na kiuchumi.

Mkutano huo uliandaliwa na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier na kuhudhuriwa na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Libya Bernardino Leon na wawakilishi wengine kutoka Libya.

Libyen Kämpfe bei Sirte
Libya inakabiliwa na kitisho cha kuwa nchi iliyoporomokaPicha: Reuters/G. Tomasevic

Hapo jana, bunge lililochaguliwa na wananchi lenye makao yake mjini Tobruk, lilipiga kura ya kuupinga mpango wa Umoja wa Mataifa wa kugawana madaraka na serikali pinzani ya mjini Tripoli. Leon amekuwa akifanya mashauriano na pande zote mbili ili kuepusha nchi hiyo kutumbukia katika hali ya kutoweza kufanya kazi tena kwa kufuata misingi ya sheria.

Rasimu ya Umoja wa Mataifa inapendekeza miongoni mwa mambo mengine kuundwa Serikali ya mpito ya Umoja wa Kitaifa kwa kipindi cha mwaka mmoja, na kisha kuongezwa muhula mwingine wa mwaka mmoja. Inaeleza kuwa bunge lililochaguliwa mwezi Juni, ambalo wabunge wengi wanaunga mkono serikali ya Tobruk, litachukua majukumu ya kutunga kisheria kwa kipindi kizima cha mpito. Pia Baraza Kuu la Taifa litaundwa hasa kutoka kwa wanachama wa serikali pinzani ya Tripoli, ambalo litaelezea maoni kuhusiana na sheria zitakazotungwa.

Pande zote mbili zitayaleta pamoja makundi pinzani ya wapiganaji na kuunda jeshi jipya chini ya udhibiti wa moja kwa moja wa serikali ambapo wanajeshi wa zamani waasi watapewa fursa ya kujiunga au kuwarejesha katika maisha ya kiraia.

Aidha rasimu hiyo inasema serikali ya umoja wa kitaifa kupitia taasisi zake mbalimbali za usalama, - jeshi na polisi – itachukua hatua mwafaka za kupambana na vitisho vya ugaidi nchini Libya.

Na wakati mazungumzo yakiendelea Berlin, takribani wapiganaji 20 wameuawa katika mapigano yaliyozuka mashariki mwa Libya baina ya kundi la Dola la Kiislamu na kundi jingine la kiislamu ambalo kisha baadaye lilitangaza vita vya jihadi dhidi ya hasimu wake mwenye msimamo mkali.

Vita vilizuka katika mji wa Derna baada ya kiongozi wa kundi la kiislamu la Majlis alShura kuuawa, kwa madai kuwa alikataa kuapa kuwa mtiifu kwa kiongozi wa Dola la Kiislamu Abu Bakr-alBaghdadi, kwa mujibu wa wakaazi wa eneo hilo

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef