1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi watoa maoni yao kuhusu kifo cha Gaddafi

21 Oktoba 2011

Kufuatia kuuawa kwa aliyekuwa kiongozi wa Libya Moummar Gaddafi hapo jana kumekuwa na hisia tofauti kutoka kwa viongozi mbali mbali duniani.

https://p.dw.com/p/12wOL
Obama akitoa maoni yake kuhusu kifo cha Gaddafi mbele ya Ikulu ya White HousePicha: dapd

Kumekuwa na shamra shamra kote nchini Libya kusherehekea kifo cha aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gaddafi. Waziri mkuu wa baraza la mpito nchini libya Mahmood Jibril alithibitisha kuuwawa kwa Gaddafi hapo jana, Jibril alisema Gaddafi aliuwawa baada ya makabiliano makali kati ya majeshi yanayomtii pamoja na yale ya baraza la mpito.

Rais wa Marekani Barack Obama, amesema kifo cha Muammar Gaddafi kimefunga ukurasa mrefu wa maumivu kwa watu wa Libya, Obama alisema hatimae utawala wa mabavu umemalizika.

"Libya itakuwa na kibarua kigumu katika kupata demokrasia kamili nchini humo, kutakuwa na kibarua kigumu lakini sisi kama Marekani pamoja na nchi nyingine za kimataifa tutawaunga mkono katika kupata demokrasia hiyo kwa sasa mmeshinda mapinduzi," alisema Obama.

Deutschland Politik Merkel PK Strauss-Kahn IWF
Kansela Angela Merkel wa UjerumaniPicha: AP

Kansela wa Ujerumani Angela Markel amesema hatimaye sasa amani imepatikana nchini Libya na kitu cha kuzingatia ni kuiunga mkono nchi hiyo katika maendeleo na kuinua uchumi wa nchi. Nayo uingereza na ufaransa nchi ambazo zimechangia katika kampeni zake za kijeshi nchini humo, wamesema kuwa wanatumai kifo cha Gaddafi kitafungua ukurasa wa demokrasia nchini humo

Nchini Afrika Kusini serikali  imeyahimiza mataifa ambayo yako katika mstari wa mbele kuisaidia libya kuhakikisha kwamba uchaguzi nchini humo utafanyika katika njia ya kidemokrasia.

Hata hivyo kando na mataifa mengi kusherehekea kifo chake, kuna pia wale wanaoomboleza. Itakumbukwa kuwa Gaddafi alikuwa na uhusiano wa karibu sana na mataifa ya Afrika. Kwa wakati mmoja Gaddafi alijitangaza kuwa ni mfalme wa wafalme barani Afrika, na kutokana na hayo aliweza kukusanya wazee wa kijadi na kuwaalika katika hema yake mjini Tripoli. Meshack Reaga ni mmoja wa wazee hao. Meshack amesema "Afrika imepoteza kiongozi muhimu. Ndoto ya Gaddafi ya kuunganisha Afrika sasa imekwisha."

Nchini Tanzania waziri wa mambo ya nje nchini humo Bernard Membe, amehimiza baraza la mpito nchini Libya kuunda serikali kwa ajili ya kutambulika katika mataifa ya Kiafrika."

Ukurasa mpya umefunguliwa nchini Libya na macho yote yanaangalia nchini humo kuona namna watakavyojiendeleza tukiangazia demokrasia amani na kundeleza nchimi wa nchi hiyo ambao umevurugika kutokana na ghasia zilizoendelea kwa mda wa miezi nane mfululizo.

Huku hayo yakiarifiwa baadae leo hii, Rais wa serikali ya mpito ya Libya, Mustafa Abdel Jalil, anatazamiwa kutangaza rasmi kukombolewa kwa nchi hiyo kutoka utawala wa Gaddafi.

Mwandishi: Amina Abubakar/APE

Mhariri: Yusuf, Saumu.