1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongzoi wa Sudan Kusini waaswa kuacha uchochezi

Admin.WagnerD22 Januari 2014

Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa viongozi wa Sudan kusini kujiepusha na kutoa kauli zitakazochochea zaidi vurugu nchini humo, wakati mkutano wa dharura wa EGAD ambao ulipaswa kufanyika Juba umeahirishwa

https://p.dw.com/p/1AvD9
Konflikt im Südsudan Flüchtlinge 17.01.2014
Wimbi la wakimbizi wa Sudan KusiniPicha: Phil Moore/AFP/Getty Images

Farhan Haq, msemaji wa umoja huo jana aliwaambia waandishi habari mjini New York kwamba ni muhimu kwa viongozi wa serikali ya Sudan Kusini na viongozi wengine mashuhuri nchini humo kujihadhari katika taarifa zao na kauli zao kwa lengo la kupunguza mvutano na uwezekano wa kuongeza zaidi machafuko.

Onyo hili la Umoja wa Mataifa limetolewa siku moja baada ya rais Salva Kiir wa Sudan kusini kuutuhumu umoja huo kuwa unajaribu kuunda utawala mwingine katika taifa lake, kwa kusema anafikiri unataka kuwa serikali ya Sudan Kusini.

Ban Ki-moon PK zu Syrien Konferenz 19.01.2014
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moonPicha: picture alliance/Zumapress.com

Akinukuliwa na vyombo vya habari vya ndani nchini Sudan Kusini, Kiir amesema kama msimamo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa basi anapaswa awe wazi.

Kwa mujibu wa msemaji wa Umoja wa wa Mataifa, Farhan Haq, kauli hiyo ya hasira ilitolewa baada ya kitendo cha walinzi wa amani wa umoja huo kuwazuia wanajeshi wa Sudan Kusini, ambao walikuwa wakilazimisha kuingia katika kambi ya Umoja wa Mataifa iliyopo katikati ya mji wa kusini wa Bor.

Walinzi amani wanatekelza wajibu wao

Haq amesema walinzi hao wa amani wa umoja huo wapo katika hatua ya kutekeleza mamlaka waliyopewa na baraza lake la usalama katika namna isiyo ya upendeleo, ambapo walinzi hao wa amani wanawalinda watu zaidi ya 70,000, katika kambi zake nane tofauti nchini humo.

Msemaji mwingine wa Umoja wa Mataifa, Ariane Quentier, alikanusha madai ya serikali ya Sudan Kusini ya kwamba kambi ya umoja huo ya Bor, ambayo inawahifadhi karibu wakimbizi 10,000 inatoa malazi kwa waasi watiifu kwa makamo wa rais wa zamani Riek Machar. Aidha Haq alisema umoja huo utaendelea kuacha milango yake wazi kwa lengo la kuwapokea watu wa aina tofauti wanaokimbia mapigano.

Umoja wa Mataifa una walinzi wa amani 7,000 nchini Sudan Kusini na wengine kiasi ya 5,500 wapo katika kuwasili nchini humo.

Umoja wa Afrika wasitisha mkutano wake wa Juba

Katika hatua nyingine mkutano wa dharura wa shirika la maendeleo la EGAD uliopaswa kufanyika kesho mjini Juba umeahirishwa lakini masuala muhimu ambayo yalipaswa kujadiliwa katika mkutano huo yatawasilishwa katika mkutano wa umoja huo unaotarajiwa kufanyika wiki ijayo mjini Addis Ababa.

Rais wa halmashauri ya Umoja wa Afrika, Nkosazana Dlamini-Zuma, ambaye alizuru Juba Jumatatu iliyopita alizitaka pande zote hasimu Sudan Kusini kuachana na mauwaji ya kiholela ya raia.

Mzozo wa kuwania madaraka kati ya Rais Kiir na Machar katikati ya mwezi Desemba mwaka uliopita umesababisha vifo vya zaidi ya watu 10,000 na wenginez zaidi ya laki 400,000 kuyakimbia makazi yao.

Mwandishi: Sudi Mnette AFP
Mhariri: Josephat Charo