1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita Gaza- Israel yakataa azimio la Umoja wa mataifa

Eric Kalume Ponda9 Januari 2009

Bazara la mawaziri nchini Israel limekubaliana kuendeleza mashambulizi dhidi ya Hamas licha ya azimio lililopitishwa na Umoja wa mataifa kuitaka nchi hiyo ikomeshe vita katika eneo la Mashariki ya kati

https://p.dw.com/p/GVFh
Mashambulizi makali yanayotekelezwa na Israel Gaza.Picha: AP


Kufuatia hatua hiyo,sasa ufanisi wa azimio hilo unayumba kwani pia wafuasi wa chama cha Hamas kwa upande wao pia wamesema kuwa hawalitambui kwani hawakuwakilishwa ipasavyo kwenye kikao maalum kilichopitisha azimio hilo.


Hilo lilidhihirishwa na mashambulizi yaliyoendelea alasiri ya leo ndani ya Gaza na pia upande wa Israel. Hata hivyo baraza la usalama la umoja huo linaishtumu vikali Israel kwa kushindwa kuheshimu maazimio ya Umoja wa mataifa.


Likitoa uamuzi wake baada ya kikao maalum kilichoitishwa kujadilia azimio hilo leo alasiri, baraza la mawaziri nchini Israel lilisema kuwa haitakubali shinikizo la kutoka nje katika maamuzi yake kwenye vita hivyo.


Badala yake lilisema kuwa linajadiliana kuhusu utekelezwaji wa awamu ya tatu ya mashambulizi ambayo ni kupelekwa kwa wanajeshi zaidi wa ardhini katika maeneo yenye idadi kubwa ya watu ndani ya ukanda wa Gaza.

Hivyo basi wanajeshi wa Israel waliendelea na mashambulizi yao ndani ya Gaza na kuwaua jumla ya Wapalestina 11 wakiwemo sita wa familia ya kiongozi wa chama cha Ukombozi wa Wapalestina.


Kwa kujibu mashambulizi hayo, Chama cha Hamas leo alasiri kimerusha makombora 11 ya roketi ndani ya Israel na kuwajeruhi wanajeshi watatu.


Waziri wa wa mambo ya nchi za nje wa Israel Tzipi Livni alisema Israel inadhamiria kutimiza malengo yake ya kuhakikisha kuwa hakuna mashambulizi ya maroketi yatakayotekelezwa kutoka upande wa Gaza.


Hali kadhalika azimio hilo pia limepingwa vikali na chama cha Hamas kikisema kuwa hakikuwakilishwa wakati wa kikao maalum kilichopitisha azimio hilo. Msemaji wa chama cha Hamas Sami Abu Zuhri alisema kamwe hawatambui azimio hilo kwani linapendelea Israel kuliko maslahi ya Wapalestina huko Gaza.


Azimio hilo lilipitishwa kwa kauli moja baada ya kuungwa mkono na mataifa 14 wanachama wa kudumu wa baraza hilo huku Marekani ambayo ni mshirika wa karibu wa Israel ikisita kupiga kura.


Maziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condolleza Rice ilisema kuwa licha ya kutoshiriki kwenye kura hiyo Marekani inaunga mkono kwa dhati azimio ingawa bado inasubiri kwanza matokeo ya mpango wa amani ya eneo la mashariki ya kati ulioanzishwa na Misri.


Rais wa sasa wa baraza la usalama la Umoja huo Miguel d`Escoto Brockman alishtumu vikali Israel akisema kuwa kwa kuendeleza mashambulizi Israel haithamini tena maisha ya binadamu wanaoendelea kuteseka katika ukanda wa Gaza kutokana na vita hivyo.


Azimio hilo linaitaka Israel ikomeshe mapigano hayo yanayoingia siku yake ya 13 hii leo ambapo watu 800 wameuawa na wengine 3000 wamejeruhiwa. Jumla ya wanajeshi 11 wa Isarael wameuawa tangu vita hivyo Disemba 27.


Wakati huo huo Waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Ujerumani Frank Walter Steinmeire anatarajiwa kusafiri hadi nchini Misri katika juhudi za kukomesha mapigano ya ukanda wa Gaza.


Waziri huyo anatarajiwa kuwasili Sharm el Sheikh hivi leo jioni kufanya mashauri na Rais Hosni Mubarak wa Misri na mwenzeka Mohmud Abbas wa Palestina. Alisema kuwa ziara yake itashirikisha juhudi za pamoja za Umoja wa mataifa ya Ulaya katika kuutanzua mzozo huo.


Ziara yake inafuatia ile ya Rais wa Ufaransa Nicholas Sarkozy katika eneo hilo wiki iliyopita ambapo pamoja na Rais Hosni Mubaraka walitangaza mpango wa amani inaoitaka Israel ikomeshe mapigano, ifungue maeneo ya mpakani na kukomeshwa kuingizwa silaha kimagendo katika eneo la Gaza.