1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita kati ya Sudan ya Kaskazini na Kusini vinanukia

23 Mei 2011

Jeshi la Sudani ya Kaskazini limefanikiwa kulidhibiti jimbo la utajiri wa mafuta la Abyei na kulazimisha maelfu ya watu kuyakimbia makazi yao. na hivyo kuashiria pande hizo kuingia katika mgogoro kamili.

https://p.dw.com/p/11Lf1
Ramani ya pande mbili za Sudan

Umoja wa Mataifa unasema baada ya wiki kadhaa ya vuta n'kuvute na kila upande ukiutuhumu upande mwengine, jumamosi iliyopita serikali ya Sudani Kaskazini ilipeleka vifaru kadhaa mjini Abyei, eneo ambalo ni makaazi ya watu wa makabila mbali mbali.

Wachambuzi wanahofu kwamba mapigano baina ya Sudan Kaskazini na Kusini kuhusu kugombania eneo la Abyei yanaweza kuziingiza katika katika vita kamili, ambapo muendeleo wake utaathiri nchi nyingine jirani, kama Kenya, Uganda na Ethiopia.

Mvutano wa udhibiti wa Abyei bado ni sababu kubwa na muhimu wakati Sudan ya Kusini ikitarajiwa kujitenga Julai 9.

Douglas Johnson ambae ni raia wa Uingereza na mtaalamu wa siasa za jimbo la Abyei "Kwa sasa, yote haya yanaweza kutatuliwa kwa kutumia makubaliano ambayo tayari yamekwisha sainiwa, vile vile na itifiki iliofikiwa juu ya Abyei ambayo inaainisha utaratibu juu ya nani atakaepiga kura kuamua eneo hilo liende upande gani."

Kuendelea kwa vurugu katika eneo hilo la jimbo la mpakani lenye rutuba kumelaaniwa vikali na Marekani, Uingereza na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lilitembelea nchini Sudan.

Balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa, Gerard Aroud, aliwaambia waandishi wa habari mjini Khartoum kwamba Baraza hilo limetoa wito kwa serikali ya Sudan kusimamisha operesheni zake za kijeshi na kujiondoa mara moja kutoka jimbo hilo.

Baraza hilo pia limelaani mashambulizi ya majeshi ya Sudani Kusini dhidi ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika jimbo la Abyei alhamisi iliyopita. Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasema Sudan ya Kaskazini imepeleka kiasi cha vifaru 15 katika mji wa Abyei.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Hua Jiang, ameliambia shirika la habari la Uingereza, Reuters, idadi kubwa ya wakazi wa jimbo hilo wameanza kuondoka na kuelekea upande wa kusini wa nchi hiyo tangu jumamosi kwa kuhofia usalama wao.

Msemaji huyo aliongeza kwa kusema kuwa mji huo unakadiriwa kuwa na kiasi ya watu elfu 20.

Mapema Januari wananchi wa Sudan ya Kusini walipiga kura ya kujitenga na Sudani Kaskazini kufuatia makubaliano ya amani yaliyofikiwa mwaka 2005 ambayo yalihitimisha vita ya baina ya pande hizo mbili.

Vita hiyo hasa baina ya Waislamu wa upande wa Kusini na upande wa Kusini ambako kuna Wakristo wengi na watu wenye dini za kiasilia vinakadiriwa kusababisha vifo vya kiasi cha watu milioni mbili.

Wachambuzi wanasema kuna uwezekano wa vita ya Sudan Kaskazini na Kusini vitakuwa na athari itakayofanana na ile iliyomalizika na kwamba mapigano yatasambaa mpaka nje ya mipaka ya Sudan nzima.

Mwandishi Sudi Mnette// RTR

Mhariri:Miraji Othman