1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita katika eneo la Caucasus

Hamidou, Oumilkher11 Agosti 2008

Warusi wapania kurejesha hadhi yao ya zamani duniani

https://p.dw.com/p/Eui1
Vikosi vya Urusi mjini Tskhinvali-mji mkuu wa Ossetia ya kusiniPicha: picture-alliance /dpa


Mada mbili zimehanikiza magazetini hii leo:kwanza kuteuliwa mwenyekiti wa zamani wa chama cha Social Democratic,Oscar Lafontaine,kuongoza orodha ya chama cha  "Linke" katika jimbo la Saarland  kwa uchaguzi mkuu mwakani, na pili kuhusu mvutano wa kijeshi katika eneo la Caucasus.


Tuanzie lakini Caucasus.Gazeti la KÖLNISCHER RUNDSCHAU limeandika:



"Kimoja ni dhahiri katika vita hivi:Viongozi wa Georgia wamekosea katika hesabu zao.Ikiwa rais Saakaschwili alifikiri angeweza kufumba na kufumbua kuitumia michezo ya Olympic ili kulikomboa jimbo lililojitenga la Ossetia ya kusini,basi ameula na chuwa.Moscow imeonyesha maguvu yake na kutuma vifaru vya kijeshi ili kubainisha ;bila ya Urusi hakuna kinachowezekana katika eneo la mizozo la Caucasus."



Gazeti linalochapishwa Würzburg-MAIN-POST linalalamika na kuandika:



"Katika kipindi cha miaka yote hii iliyopita,hakuna yeyote kati ya pande hizi mbili,aliyejaribu kufanya juhudi za kupunguza makali ya mzozo unaozidi kutokota.Madhara yake ni kwamba vita vya kimkoa vilivyoripuka, vinatishia kuchukua sura nyengine kabisa na kugeuka mvutano kati ya Mashariki na Magharibi.Kwasababu hoja kwamba Georgia inajaribu kuyakomboa majimbo yake yaliyojitenga ya Ossetia ya kusini na Abkhasia,ni za kijuu juu tuu,kindani ndani lakini huu ni ugonvi wa kutaka kupimana nguvu madola makuu ya dunia."


Maoni kama hayo yamechambuliwa pia na gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE linalohisi "hakuna ugonvi wa kimkoa,dola mojawapo kuu linapoingilia kati."Gazeti linaendelea kuchambua:


"Mara zote dola kuu linapojiingiza ni kwasababu ya kupigania masilahi yake na kudhihirisha maguvu yake dhidi ya madola mengine makuu.Majeshi ya Urusi hayajajiwekea lengo pekee la kukidhibiti kipande cha ardhi cha Osetia ya kusini,linataka pia kuimarisha hadhi yake -kueneza hofu na vitisho sio tuu katika nchi jirani,bali pia mijini Brussels,Beijing na Washington.Urusi haitaki na haitokubali tena kuchezewa."


Ni onyo hilo la FRANKFURTER ALLGEMEINER ZEITUNG.Nalo gazeti la DIE WELT linaandika:


"Georgia inataka kujiunga na jumuia ya kujihami ya magharibi na Umoja wa Ulaya pia.Wamarekani wanaunga mkono mipango hiyo.Kabla ya kujiunga lakini na jumuia ya kujihami ya magharibi,kila nchi inabidi kwanza isawazishe mivutano yake ya mpakani.Kiongozi wa mapinduzi ya mawardi ya mwaka 2004 amefanya pupa-ameshindwa kutambua ,kijeshi hawezi kushindana na Urusi."