1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita kuepuka kushuka daraja yaanza rasmi

18 Aprili 2016

Vita ya kuepuka kushuka daraja yapamba moto katika ligi za Ulaya , katika Bundesliga timu saba roho juu wakati ikibakia michezo minne ligi kufikia ukingoni.

https://p.dw.com/p/1IXu9
Fußball Bundesliga Borussia Dortmund - Hamburger SV
Wachezaji wa Hamburg SV wakitoka nje vichwa chini baada ya kufungwa na Dortmund 3-0Picha: picture-alliance/dpa/G. Kirchner

Katika Bundesliga, Bayern Munich inanyemelea ubingwa wake wa nne mfululizo baada ya kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Schalke 04. Schalke inashikilia nafasi ya saba hadi sasa, na kuna uwezekano wa kushindwa kucheza michuano ya Ulaya mwakani iwapo haitajitahidi kufikia nafasi ya tano ama ya sita ikiwa imebakia michezo minne hadi ligi kufikia mwisho.

Bundesliga 30.Spieltag FC Bayern Muenchen gegen FC Schalke 04
Eric Maxim Choupo-Moting wa Schalke akipambana na wachezaji wa BayernPicha: Getty Images/Bongarts/A. Hassenstein

Borussia Dortmund iliweka kando maumivu ya kutolewa katika robo fainali ya kombe la Europa League dhidi ya Liverpool katikati ya wiki iliyopita, na kuelekeza hasira zao dhidi ya SV Hamburg kwa kukandika mabao 3-0 licha ya kuingiza uwanjani Signal Iduna Park kikosi cha vijana na kuongozwa na nahodha Mats Hummels.

Huyu hapa kocha wa Dortmund Thomas Tuchel. "Nimeridhika sana na kile kilichotokea. Kulikuwa na wakati fulani tuliteleza na kufanya makosa madogo, kama ilivyotokea kwa Manni Bender, kosa ambalo lingetugharimu kufungwa bao. Lakini kwa wastani tuliweza kupambana vizuri. Ilichukua muda kidogo, hadi tulipoweza kutengeneza maeneo, na uwezo wa kupeana pasi, na kwenda kasi kidogo. Na ndio sababu kila kitu kilikwenda vizuri."

Fußball Bundesliga Borussia Dortmund - Hamburger SV
Kikosi cha timu ya DortmundPicha: Getty Images/Bongarts/L. Baron

Ushindi huo wa Dortmund dhidi ya Hamburg SV umeilazimisha timu hiyo kujikita sasa katika harakati za kujinasua kutoka janga la kushuka daraja licha ya kuwa na pointi 34 ikiwa katika nafasi ya 12. Timu za Damstadt 98, Hamburg SV, TSG Hoffenheim , FC Augusburg, VFB Stuttgart, Werder Bremen , Eintracht Frankfurt na Hannover 96 zinajishughulisha sasa kuweka mikakati ya kutoshuka daraja.

Hannover 96 hata hivyo inajikuta katika wakati mgumu kubakia katika daraja la juu ikiwa na pointi 21 tu mkiani na imezidiwa pointi 6 na timu iliyoko juu yake Eintracht Frankfurt. Hivyo njia imekwisha safishwa kwa Hannover kurejea katika daraja la pili licha ya karatasini kuwa inaweza kufikisha pointi 33 katika michezo minne iliyobakia pointi ambazo tayari VFB Stuttgart inazo ikiwa katika nafasi ya 15.

Niko Kovac ni kocha wa Eintracht Frankfurt: "Kila siku tunamsalimu panyabuku shimoni, kila wakati ni kitu kile kile. Tunatengeneza nafasi, ambazo tunazipata, lakini hatufungi. Na timu kama Leverkusen inafunga mabao. Hii ndio tofauti . Lakini naweza tu kusema hivi: Timu imefanya kila linalowezekana, lakini juhudi hizo hazikuweza kuzaa matunda. Hali kwa kusema kweli ni ngumu kwetu."

Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / afpe / dpae / rtre
Mhariri: Josephat Charo