1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya Gaza vimeathiri mazingira

H.Jeppesen - (P.Martin)2 Machi 2009

Ili kuweza kukadiria uharibifu wa mazingira uliosababishwa na operesheni za kijeshi za Israel kwenye Ukanda wa Gaza,shirika la kimataifa-UNEP- linaloshughulikia miradi ya mazingira,limeombwa kutayarisha ripoti ya kwanza.

https://p.dw.com/p/H4KA
Palestinians inspect the damage at a building following Israeli military operations, in the Sheikh Radwan neighborhood in Gaza City, Wednesday, Jan.14, 2009. Israeli aircraft pounded militants' rocket-launching pads, weapons arsenals and dozens of arms smuggling tunnels near the Gaza-Egypt border, the military said Wednesday, as U.N. chief Ban Ki-moon headed to the region to lend his heft to diplomatic efforts to wrest an end to Israel's bruising, 19-day-old assault. (AP Photo/Hatem Moussa)
Majengo yaliyobomolewa Gaza katika operesheni za kijeshi za Israel.Picha: AP

Vita vinapozuka mazingira pia huathirika-haidhuru ni silaha gani inayotumiwa. Mifumo ya maji inapobomoka,ardhi inapochafuka au asbestosi ikitawanyika katika nyumba zilizobomolewa,bila shaka matokeo ya aina hiyo vitani huathiri afya ya umma.Henrik Slotte,mkuu wa ofisi ya UNEP inayoshughulikia maafa baada ya migogoro anasema,ni muhimu sana kupeleka tume za wataalamu wa mazingira katika maeneo hayo upesi iwezekanavyo. Mapigano yaliposita tu katika Ukanda wa Gaza,wataalamu wa UNEP waliombwa na Umoja wa Mataifa kwenda huko kufanya uchunguzi wa mwanzo.

Migogoro ikitulia,basi hali ya usalama na fedha za kugharimia kazi zao ni mambo yanayoamua miradi itakayoweza kutekelezwa na UNEP sawa na mashirika mengine ya kiutu na Umoja wa Mataifa.Ripoti kamilifu ya wataalamu wa UNEP kuhusu hali ya mazingira inayokutikana Ukanda wa Gaza inagharimu kiasi cha dola nusu milioni-hiyo ni gharama isiyokuwepo katika bajeti ya kawaida ya UNEP.Kwa hivyo ni matumani ya Slotte kuwa baada ya mkutano wa wafadhili huko Sharm el-Sheikh,kutatolewa ahadi ya kuhakikisha usalama wa wafanya kazi na kusimamia gharama za kutayarisha ripoti kamili.Anasema,kati ya wataalamu sita hadi kumi wanahitajiwa ili uchunguzi wa kina unaopaswa kufanywa katika Ukanda wa Gaza uweze kutimizwa kabla ya kutayarisha ripoti kamilifu.

Kwanza watachunguza hali ya maji ya kunywa.Baadae watachukua sampuli za udongo kwani watu watataka kujua iwapo vyakula vinavyopandwa ni salama. Isitoshe,kuna uchafuzi wa asbestosi. Kwani asbestosi ilitumiwa katika ujenzi wa baadhi ya nyumba zilizobomolewa. Kwa hivyo vifusi vya nyumba hizo vikitumiwa tena bila ya hapo kwanza kufanyiwa uchunguzi basi hilo ni tatizo kubwa sana.

Lakini ripoti ya wataalamu wa UNEP haitohusika na uchafuzi wa mazingira uliosababishwa na silaha maalum.Kwa mfano ikihusika uranium iliyorutubishwa katika silaha zilizotumiwa,basi hapo watakaohusika na uchunguzi ni wataalamu wa shirika la atomu la kimataifa IAEA.Hata uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na silaha za aina nyingine unahitaji kufanyiwa uchunguzi maalum. UNEP haina mamlaka ya kufanya uchunguzi kama huo.Lakini wataalamu wake wamewahi kuombwa na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa kusaidia uchunguzi wa aina hiyo.

Ni dhahiri kuwa ripoti ya UNEP itakuwa na umuhimu maalum katika majadiliano yanayohusika na ujenzi upya wa Ukanda wa Gaza.Lakini kabla ya kazi hizo za ujenzi kuweza kuanza,wataalamu wa UNEP na mashirika mengine wanahitaji kujua kiwango cha uharibifu uliosababishwa na vita vya Gaza.