1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya Irak vyamalizika rasmi

Abdu Said Mtullya19 Agosti 2010

Vikosi vya mapambano vya Marekani vyaondoka rasmi Irak.

https://p.dw.com/p/OrKU
Majeshi ya Marekani yaondoka Irak baada ya miaka saba.Picha: AP

Miaka saba baada ya kumwangusha Saddam Hussein, Marekani imeviondoa vikosi vyake vya mapambano kutoka Irak na vilivyobakia vilivuka mpaka alfajiri ya leo na kuingia Kuwait.Ulikuwa usiku wa kihistoria. Kwa usemi mwingine vita vimemalizika nchini Irak.

Rais Barack Obama ameitekeleza ahadi yake.Alitamka wazi kwamba hadi tarehe 31 mwezi agosti mwaka 2010 jukumu la mapambano kwa majeshi ya Marekani litamalizika nchini Irak. Alisema na hilo ndilo hasa tutakalolifanya,kwa saa iliyopangwa juu ya alama, kama jinsi ilivyoahidiwa.

Saa mbili za usiku jana vyombo vya habari vya Marekani vilitangaza kwa wakati mmoja mwisho wa mapambano kwa vikosi vya Marekani katika vita vya Irak.

Muda mfupi tu baadae wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilitangaza rasmi mwisho wa vita kwa majeshi ya Marekani nchini Irak.

Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo imezungumzia juu ya wasaa wa kihistoria.

Ilikuwa furaha kubwa kwa askari wa mwisho alfu 2 wa Marekani wakati walipouvuka mpaka na kuingia Kuwait. Askari hao waliruka kutoka kwenye vifaru na kuanza kupepea bendera ya Marekani.

Zoezi la kuviondoa vikosi vya mapambano kutoka Irak limekuja mapema kuliko iliyvotarajiwa.Hadi tarahe mosi ya mwezi wa agosti mapambano yalipangwa kumalizika.

Kwa kuyaondoa majeshi hayo,rais Obama ameitekeleza ahadi aliyoitoa juu ya sera za nje, yaani kuvimaliza vita vya Irak kwa njia ya busara. Obama alivipinga vita vya Irak kabla hata ya kuingia katika madaraka ya urais.

Hatua ya kuyaondoa majeshi mapema imekuja wakati mzuri kwa rais Barack Obama, yaani kabla ya kufanyika uchaguzi wa bunge.Obama alisema,kuwa hadi mwishoni mwa mwezi huu wanajeshi wa Marekani 9,000 watakuwa wameondolewa kutoka Irak.

Lakini wachunguzi wametilia maanani kwamba askari hao wanaondoka wakati ambapo raia wengi wa Irak wanauawa.Mwezi uliopita ulikuwa mbaya sana nchini Irak. Raia 535 waliuawa. Idadi hiyo haijawahi kufikiwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.Na jana tu watu zaidi ya 50 waliangamizwa katika mji wa Baghdad baada ya mshambuliaji wa kujitoa mhanga kujiripua.

Majeshi ya Marekani pia yanaondoka wakati ambapo wairaki bado hawajafanikiwa kuunda serikali, miezi mitano baada ya kufanyika uchaguzi mkuu.Lakini rais Obama amesema kuwa askari wa mwisho kabisa ataondoka Irak tarehe mosi desemba mwaka ujao-2011.

Mwandishi/Sina,Ralph/ARD/ZDF/

Tafsiri/Mtullya abdu.

Mhariri/Abdul-Rahman