1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya Libya ni hisabu isiyojuilikana

20 Machi 2011

Maamuzi ya Jumuiya ya Kimataifa kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Libya yanatajwa kuwa ni hisabati yenye mambo mengi yasiyofahamika, na kwamba nchi washirika zimeingia kwenye mgogoro zisiojua namna ya kuutoka.

https://p.dw.com/p/10cy6
Ndege ya kijeshi ya NATO
Ndege ya kijeshi ya NATOPicha: AP

Kile kinachoitwa "Muungano wa Kimataifa", chini ya uongozi wa Ufaransa, umeanza harakati zake za kijeshi dhidi ya utawala wa Libya, lakini bila ya shaka ni jambo lenye gharama zake.

Japokuwa pana vituo vichache vya jeshi la anga ambavyo unaweza kuvishambulia nchini Libya, huko hakutamaanisha kwamba nguvu za kijeshi za nchi hiyo zimemalizwa kabisa.

Muungano huu wa kimataifa unaweza kuingia kirahisi, na yumkini ndani ya wiki moja tu, ukawa umeweza kuwasaidia watu wa Benghazi kupata huduma zote muhimu, yakiwemo maji na umeme.

Lakini Muammar Gaddafi anadhibiti asilimia 80 ya Libya, na ana mkono wake juu ya kila rasilimali ya nchi hiyo. Ikiwa Muungano huu hauko tayari kukabiliana na ukweli huu, basi mashambulizi ya angani na udhibiti wa mipakani, hautakuwa chochote zaidi ya ushindi kwa Gaddafi, na sio kinyume chake.

Rais Barack Obama wa Marekani
Rais Barack Obama wa MarekaniPicha: AP

Marekani yenyewe bado ipo kwenye njia panda: upande mmoja inataka ijiingize kabisa kabisa, upande mwengine inataka iwe kando kando tu.

Rais Barack Obama ameondoa uwezekano wa kupeleka majeshi ya ardhini au hata kujiingiza kwenye mzozo huu kwa kipindi kirefu, lakini yeye na wenzake wanataka Gaddafi apate funzo.

Ikiwa hivyo ndivyo, basi lengo la kile kinachoitwa hatua za kijeshi dhidi ya utawala wa Gaddafi halifahamiki sawa sawa.

Maana ikiwa lengo lake ni kuwalinda raia tu dhidi ya mashambulizi ya vikosi vya Gaddafi, basi vikosi vya Muungano vina, kwa uchache, muda wa mwezi mmoja, kulifanikisha hilo. Kwa hivyo, Gaddafi anao muda wa kungojea.

Kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi
Kiongozi wa Libya, Muammar GaddafiPicha: AP/RTP TV

Lakini ikiwa lengo la hatua hizo ni kuuondosha utawala wa Gaddafi, basi majeshi ya Muungano lazima yafanye mashambulizi makali, tena ndani ya kipindi kifupi dhidi ya vituo vya kijeshi vya Gaddafi.

Bila ya mashambulizi hayo, kuuondoa utawala wa Gaddafi ni jambo lisilowezekana. Na huko kutakuwa ni kujiingiza kamili kamili kijeshi.

Ila ikumbukwe kuwa, hilo halikuwa azimio Namba 1973 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lililoidhinisha marufuku ya anga dhidi ya Gaddafi hapo juzi, na pia haukuwa uamuzi uliotajwa wazi na viongozi wa mataifa makubwa yaliyokutana mjini Paris, Ufaransa, hapo jana (19.03.2011).

Na kwa vita hivi, kuna suali jengine la kujibiwa: Umejua kuvianza, lakini je unajua lini na vipi utavimaliza?

Inatarajiwa kuwa Muungano huu wa Mataifa haujapitikiwa bado na mafunzo ya vita vya Balkan, vya Iraq na kadhia inayoendelea hadi sasa nchini Somalia. Mwisho wa hili la Libya nao, hauonekani kuwa mzuri.

Mtu angeliweza kusema kuwa, ule uamuzi wa mwanzo wa Ujerumani kujiepusha kuingia kwenye mgogoro wa kijeshi na Libya ulikuwa sahihi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido WesterwellePicha: dapd

Huo ulitakiwa uwe mtazamo wa Umoja wa Ulaya pia. sio kuchukuliwa na andasa za siasa za ndani za Nicolas Sarkuzy wa Ufaransa, ambaye anaukimbia mbinyo wa kisiasa ndani ya nchi yake kwa kujibebesha dhima ya kuongoza shinikizo dhidi ya Libya.

Ikiwa Muungano huu wa Mataifa utakuwa na bahati njema, basi utaweza kumdhibiti Gaddafi kijeshi na kisha kuushawishi Umoja wa Mataifa umuwekee vikwazo vya silaha. Lakini ukikumbwa na bahati mbaya, basi ujitayarishe kwa hasira za mkizi kutoka kwa Gaddafi mwenye silaha.

Je Ufaransa na Italia zimejitayarisha kuyakaribisha makombora ya Gaddafi kwene miji ya Neapal au Marseille? Maana anaweza kuwa tayari kuyatuma huko.

Na kwa upande mwengine, ikiwa mashambulizi ya majeshi ya Muungano yataleta maafa makubwa kwa raia, basi si vigumu kwa maoni kwenye nchi za Kiarabu na Kiislamu kubadilika haraka sana, yakazigeukia nchi washirika.

Kwa kila hali, safari ya mkasa na yenye mwisho usiojuilikana ndio imeanza.

Mwandishi: Bernd Riegert/ZPR
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman