1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sheria kali za usafiri

14 Januari 2015

Serikali kuu ya Ujerumani inapanga kuzifanya ziwe ngumu safari za kuingia na kutoka watuhumiwa wa kigaidi humu nchini. Baraza la mawaziri limepitisha mswaada wa sheria leo

https://p.dw.com/p/1EK7H
Waziri wa Mambo ya ndani Thomas de MaizierePicha: picture-alliance/dpa/S. Muylaert

Kuambatana na mswaada huo wa sheria watuhumiwa wa kigaidi wataweza kupokonywa paspoti zao .Hadi wakati huu maafisa wa idara za uhamiaji walikuwa na haki ya kumpokonya mtu paspoti yake ikiwa atakuwa anatuhumiwa kwenda ng'ambo kujiunga na harakati za kigaidi.Hata hivyo watuhumiwa hao wa kigaidi waliweza pia kutumia njia ya nchi kavu katika nchi za umoja wa Ulaya kuingia Syria,wakitumia vitambulisho vyao tu.

Siku za mbele vitatolewa vitambulisho mbadala vitakavyokuwa na muda wa hadi miaka mitatu na ambavyo havitomruhusu mhusika kuihama Ujerumani.Uamuzi huo ulipitishwa na mawaziri wa mambo ya ndani wa serikali kuu na zile za majimbo walipokutana msimu wa mapukutiko mwaka jana.Wamezungumzia hatari kwa usalama wa Ujerumani pindi wafuasi wa itikadi kali wakirejea nyumbani kwa mfano baada ya kushiriki katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.

Mswaada wa sheria uliopitishwa leo unakumbusha shambulio dhidi ya makumbusho ya wayahudi ya mwezi Mai uliopita yaliyofanywa na wanamgambo wa itikadi kali waliorejea nyumbani kutoka Syria.

Hata kabla ya mashambulio ya kigaidi ya Paris,serikali kuu ya Ujerumani inafuatilizia kwa makini hali ya mambo ya kutathmini njia za kuchukua hatua za kinga ili kuepusha balaa la wale wanaorejea nyumbani kuzidi kuwa na misimamo mikali.Akifafanua mswaada huo wa sheria bungeni ,waziri wa mambo ya ndani wa serikali kuu ya Ujerumani Thomas de Maizière anasema:

"Mojawapo ya sheria hizo ni mswaada wa kuifanyia marekebisho sheria ya kumiliki kitambulisho ,na kuanzishwa kitambulisho mbadala.Mswaada huo wa sheria uliopitishwa leo hii na serikali kuu ya Ujerumani lengo lake ni kuzuwia ingia toka ya magaidi wafuasi wa itikadi kali."

Wafuasi 450 wa itikadi kali wamekwenda Syria

Duru za kuaminika zinasema tangu mwaka 2012 wanamgambo 450 wa itikadi kali wameondoka Ujerumani kwenda Syria..Asili mia 60 ya watu hao wana uraia wa kijerumani.

Salafismus in Deutschland
Itikadi kali nchini UjerumaniPicha: picture-alliance/dpa/U. Deck

Mkuu wa kundi la SPD bungeni Christine Lambrecht amesema hatua ziada zitafuata ili kujikinga dhidi ya mashambulio ya kigaidi.

Wafuasi wa chama cha siasa kali za mrengo wa shoto die Linke na walinzi wa mazingira die Grüne wamezikosoa hatua hizo wakidai hazitasaidia pakubwa.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/epd/AFP

Mhariri:Josephat Charo