1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vitisho vya ugaidi na mwaka mpya

Admin.WagnerD31 Desemba 2015

Sherehe za kuukaribisha mwaka mpya zinatazamiwa kufanyika chini ya ulinzi mkali wakati Ubelgiji ikichukuwa hatua ya kufuta sherehe za mkesha wa mwaka mpya kwa hofu ya mashambulizi ya kigaidi.

https://p.dw.com/p/1HWa1
Wanajeshi wakipiga doria Brussels.
Wanajeshi wakipiga doria Brussels.Picha: picture-alliance/dpa/T. Roge

Sherehe za kuukaribisha mwaka mpya zinatazamiwa kufanyika chini ya ulinzi mkali katika sehemu mbali mbali duniani ,wakati Ubelgiji ikichukuwa hatua ya kufuta sherehe za mkesha wa mwaka mpya kwa hofu ya mashambulizi ya wapiganaji wa kijihadi ikiwa ni wiki chache kufuatia mashambulizi yaliosababisha maafa mjini Paris

Katika kitovu cha Ulaya shamra shamra na fataki za kuukaribisha mwaka mpya zimefutwa wakati mji mkuu wa nchi hiyo Brussels makao makuu ya Jumuiya ya Kujihami NATO na Umoja wa Ulaya yakiwa katika hali kubwa ya tahadhari.

Meya wa mji huo Yan Mayeur amesema hapo jana sio vyema kubahatisha katika hali ya hatari baada ya polisi kuwakamata watu wawili wanaoshukiwa kupanga mashambulizi katika maeneo ya kihistoria mjini Brussels wakati wa sherehe hizo.

Jumla ya watu wanane hivi sasa wanashikiliwa na polisi wakiwemo watu wawili waliofunguliwa rasmi mashtaka yanayohusiana na ugaidi baada ya kukamatwa kwao mapema wiki hii.

Watuhumiwa sita walikamatwa kufuatia misako saba ya polisi ndani na karibu na mji mkuu huo ambapo vifaa vya kompyuta simu za mkono na aina fulani ya bunduki vilikamatwa.

Hali ya tahadhari

Mji huo wa wakaazi milioni 1.2 umekuwa katika hali ya tahadhari kubwa tokea Ufaransa kusema kwamba watu kadhaa waliohusika katika mashambulizi yaliosababisha maafa mjini Paris walikuwa na mahusiano na mji wa Brussels.

Wanajeshi kwenye ulinzi Brussels.
Wanajeshi kwenye ulinzi Brussels.Picha: Reuters/F. Lenoir

Mkaazi huyu wa Brussels Koen Vandaele anaunga mkono uamuzi wa serikali kufuta sherehe za mkesha wa mwaka mpya.

Amesema "Nafikiri ni uamuzi mzuri na wa busara.Nakubali kwamba kunaweza kutokea vurugu kubwa wakati wa fashi fashi. Naishi karibu kwa hiyo kwa sababu za kiusalama nafikiri ni uamuzi mzuri."

Hali ya wasi wasi

Mji mkuu wa Ufaransa Paris ambao bado uko katika hali ya wasi wasi kutokana na shambulio la kigaidi la Nobemba 13 lililouwa watu 130 pia umefuta matumizi ya fashi fashi katika mkesha huo wa mwaka mpya.

Usalama waimarishwa Paris.
Usalama waimarishwa Paris.Picha: Getty Images/AFP/K. Triboullard

Lakini serikali imekubali kwamba mkusanyiko mkubwa wa watu hadharani tokea kufanyika mashambulizi hayo unaweza kuendelea kufanyika katika mtaa wa Champs Elysee huku usalama ukiimarishwa.

Nchini Uturuki polisi imewakamata watuhumiwa wawili wa kundi la Dola la Kiislamu wanaodaiwa kupanga mashambulizi katikati ya mji wa Ankara ambao unatarajiwa kufurika watu wakati wa mkesha wa mwaka mpya.

Mjini Moscow polisi kwa mara ya kwanza wataufunga uwanja wa Red Square ambapo kwa desturi maelfu hukusanyika kwa sherehe za mwaka mpya. Meya wa mji huo Segei Sobyanin amesema "sio jambo la siri kwamba Moscow ni mojawapo ya shabaha ya mashambulizi ya magaidi."

Usalama Ujerumani

Mjini Berlin watu milioni moja wanatarajiwa kumimininika katika Lango la Brandenburg kwa tafrija ya kuukaribisha mwaka mpya.

Rainer Wendt Mkuu wa Polisi Ujerumani.
Rainer Wendt Mkuu wa Polisi Ujerumani.Picha: picture-alliance/dpa/I. Wagner

Rainer Wendt ni mkuu wa polisi nchini Ujerumani amekaririwa akisema "Serikali ya Ujerumani imeanzisha na kikosi cha kupamabana na ugaidi upatikanaji wa taarifa kutoka kituo kimoja kikuu ambacho kitapokea taarifa kutoka nje na kutoka mashirika ya ujasusi na uhalifu ambazo itazichambuwa na kuzitathmini. Ndio sababu unaweza kutegemea hali nzuri ya usalama nchini Ujerumani."

Nchini Uingereza wanausalama 3,000 watamwagwa katikati ya London kwa kile kinachoripotiwa kuwa hatua kubwa ya usalama isio na kifani kupiga vita ugaidi.

Indonesia pia iko katika hali kubwa ya tahadhari baada ya polisi wa kupiga vita ugaidi kugunduwa mipango ya kufanya shambulio la kujitowa muhanga wakati wa sherehe za mwaka mpya katika mji mkuu wa nchi hiyo Jakarta.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman