1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vituko vya Trump Magazetini

Oumilkheir Hamidou
17 Mei 2017

Vituko vya rais wa Marekani Donald Trump, na mpango wa Umoja wa Ulaya wa kuondowa vizuwizi vya kura ya turufu katika kuidhinishwa makubaliano ya kibiashara ni miongoni mwa mada magazetini

https://p.dw.com/p/2d5ka
USA Treffen zwischen Trump und Lavrov
Picha: picture alliance/dpa/A. Shcherbak

Tunaanzia Marekani ambako vituko vinavyozidi kuongezeka vya rais Donald Trump aliyemfukuza kazi kiongozi wa idara ya upelelezi na kufika hadi ya kumfichulia  siri muhimu kuhusu wanamgambo wa itikadi kali wa dola la kiislam, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi , vimepelekea wahariri wa magazeti ya Ujerumani kujiuliza  kama vituko hivyo havijafikia daraja ya kashfa ya Watergate iliyomwangusha rais wa zamani wa Marekani Richard Nixon Agosti 9 mwaka 1974. Gazeti la "Passauer Neue Presse linaandika": "Yadhihirika kana kwamba kiongozi huyo aliyezidiwa, hatambui makosa anayofanya kwasababu anashindwa kutambua upeo wa zahma aliyoizusha. Kama sivyo angetambua aliyoyafanya yanaitia hatarini  maisha ya nchi yake mwenyewe, maisha ya washirika wa nchi yake na yale ya watumishi wote wa idara za upelelezi. Rais huyu wa Marekani ni kitisho bayana kwa usalama, sio stadi na asingestahiki hata wakati mmoja kuwa kiongozi wa taifa na serikali ya nchi yenye ushawishi mkubwa kabisa ulimwenguni kama hii.

 

Maoni kama hayo yameandikwa pia na gazeti la "Hessische Niedersäschsische Allgemeine": "Ingekuwa vituko hivyo vyote si vya kuhuzunisha basi mtu angeangua kicheko. Lakini havichekeshi.Tabia ya Trump inaishushia hadhi yake Marekani na kugeuka kuwa kitisho kwa usalama wa ndani wa Marekani.

 

Kukiuka kura ya turufu ni kinyume na demokrasia

Mjadala umezuka nchini Ujerumani na katika nchi za Umoja wa ulaya kuhusu mpango wa Umoja wa ulaya wa kukiuka utaratibu wa kutumiwa kura ya turufu kupinga makubaliano ya kibiashara. Gazeti la "der neue Tag" linahisi mpango huo utaiendeya kinyume misingi ya kidemokrasi. Gazeti linaendelea kuandika: "Mbinu zinazotaka kufuatwa na Umoja wa ulaya hazifuatani na misingi ya kidemokrasi. Katika mfumo wa kidemokrasi imetajwa kabla ya maamuzi kupitishwa, maoni ya wapinzani pia yanabidi yazingatiwe. Kwamba zoezi hilo ni la usumbufu na linahitaji muda , hiyo pia ni sehemu ya demokrasia. Ikiwa Umoja wa Ulaya utataka kupitishwa makubaliano bila ya kutafuta ridhaa ya wanachama, hilo litakuwa sawa na kuwapokonya haki yao wananchi. Maamuzi ya mahakama kuhusu kura ya turufu yanaimarisha mfumo wa kidemokrasia miongoni mwa nchi za ulaya na kuijongeza karibu zaidi na wananchi halmashauri kuu ya Umojua wa ulaya mjini Brussels.

 

Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Yusuf Saumu