1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Volkswagen yaipiku Toyota mauzo ya magari duniani

Iddi Ssessanga
30 Januari 2017

Kampuni ya magari ya Ujerumani Volkswagen iliuza magari mengi zaidi duniani kuliko mshindani wake wa Japan Toyota mwaka 2016, na kushinda taji la kampuni kubwa zaidi ya utengenezaji magari kwa mara ya kwanza.

https://p.dw.com/p/2WcKF
Symbolbild VW - Toyota
Picha: picture-alliance/dpa/O. Spata/J. Castro

Makampuni ya Toyota, yakiwemo Daihatsu Motor na Hino Motors, yaliripoti kuwa mauzo yake duniani yaliongezeka kwa kwa asilimia 0.2 kutoka mwaka uliotangulia na kufikisha magari milioni 10.17 mwaka 2016.

Mauzo ya Volkswagen au VW kwa kifupi kwa mwaka sawa yalikuwa magari milioni 10.3 yakiongezeka kwa asilimia 3.8 kutoka mwaka uliotangulia, licha ya kashfa ya udanganyifu wa viwango vya uchafuzi wa mazingira, ilisema kampuni hiyo mapema mwezi Januari.

Toyota imetoka kwenye nafasi ya kwanza kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2011, wakati mnyororo wa ugavi wa kampuni hiyo ulivyovurugwa na tetemeko kubwa la ardhi lililosababisha sunami kaskazini-mashariki mwa Japan.

Mwaka 2016 mauzo ya Toyota nje ya Japan yalishuka kwa asilimia 0.5 kutoka mwaka uliotangulia, hadi magari milioni 7.94, kutokana na kupungua kwa mauzo ya nje kwenda Amerika Kaskazini, ambako ndiyo kuna soko kubwa zaidi la kampuni hiyo.

VW Volkswagen Logo
Nembo ya Volkswagen ikionekana katika mmoja ya maonesho ya magari mjini Paris, Ufaransa.Picha: Getty Images

Hatuangalii idadi ya magari

Toyota imepuuza umuhimu wa kupitwa na Volkswagen. "Katika Toyota hatuangalii wingi, tunaamini kwamba wingi wa mauzo yetu ni matokeo tu ya mkakati wetu wa kuunda magari mazuri zaidi na kuwapa uzoefu mzuri wateja," ilisema kampuni hiyo katika taarifa.

"Lengo letu ni kuwa nambari moja kwa wateja kwa kusanifu na kutengeneza magari bora. tunamshukuru kila mteja aliechaguwa gari la Toyota," iliongeza kusema taarifa hiyo.

Septemba 2015, kampuni ya Ujerumani ya Volkwagen ilikiri kwamba iliweka kifaa kinachonuwia kudanganya vipimo vya kiwango cha uchafuzi wa mazingira katika karibu magari milioni 11 ya dizeli yaliouzwa duniani kote.

Kashfa hiyo mpaka sasa imeigharimu kampuni hiyo kubwa zaidi ya magari barani Ulaya, mabilioni ya euro na kupelekea kushtakiwa sita miongoni mwa watendaji wake wa juu nchini Marekani.

Kampuni hiyo pia ianakabiliwa na  madai ya uharibifu kutoka kwa wawekezaji yanayofikia euro bilioni 8.8, na inafanya mazungumzo na wateja kuhusiana na malipo ya fidia kufuatia kurejeshwa kwa magari yalioathiriwa na udanganyifu huo.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae

Mhariri: Saumu Yusuf