1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vyama vya CDU na SPD vyanusurika kikumbo cha AfD Ujerumani

Saumu Mwasimba
2 Septemba 2019

Matokeo ya uchaguzi wa majimbo ya Saxony na Brandenburg yamewashusha pumzi wapinzani wa siasa kali za AfD ingawa bado vyama vikuu vilivyoshinda katika majimbo hayo vinaweweseka na nguvu za chama hicho cha siasa kali.

https://p.dw.com/p/3OsR3
Landtagswahl in Sachsen 2019 | Dresden | Michael Kretschmer, CDU
Picha: Reuters/M. Rietschel

Vyama vikuu vya kisiasa vinakutana leo kutathmini matokeo ya uchaguzi  yalioonesha kuporomoka kwao katika eneo la Mashariki mwa  Ujerumani. Katika uchaguzi uliofanyika jana kwenye majimbo mawili ya Saxony na Brandenburg chama cha siasa kali za mrengo wa kulia kimejiongezea umaarufu.

Licha ya kupata pigo kubwa,chama cha Kansela Angela Merkel cha Christian Democratic Union CDU na kile cha siasa za wastani cha mrengo wa kushoto Social Democrats SPD vilifanikiwa kuivuka changamoto kubwa  ya chama cha siasa kali za mrengo wa kulia AfD katika uchaguzi wa Saxony na Brandenburg.

Landtagswahl in Brandenburg 2019 | Potsdam | SPD
Picha: Getty Images/AFP/M. Skolimowska

Viongozi wa vyama hivyo viwili huenda wanashusha pumzi ya ahueni wakati wakuu wa vyama vyao wakikutana mjini Berlin kujadili matokeo,na hasa baada ya kura za maoni za miezi kadhaa iliyopita kutowa sura ilioonesha kuna hatari ya chama cha AfD kuibuka kuwa chama kikubwa katika mabunge ya majimbo yote mawili.

Ushikiano na AfD utakuwepo?

Lakini baada ya CDU kuendelea kuongoza katika jimbo la Saxony na SPD kurudi katika jimbo la Brandenburg vyama hivyo hivyo vinakabiliwa na masuali magumu juu ya vipi vitaweza kukishughulikia chama cha siasa kali cha AfD ambacho sasa kimeibuka kuwa chama cha pili chenye nguvu katika majimbo yote mawili.Kiongozi wa AfD Alexander Gauder anasema matokeo hayo yamewatia nguvu.

'' Nafahamu kwamba tumechaguliwa na bado tutaendelea kuchaguliwa kwasababu wengine wameshindwa kabisa katika masuala muhimu. Kuna sera ya wakimbizi kuna sera ya kuinusuru Yuro.Watu wengi hawajioni tena kuwakilishwa na siasa na wametuchagua sisi''

Chama cha CDU kimeshaondowa uwezekano wa kushirikiana na AfD. Annergret Kramp Karrenbauer kiongozi wa chama hicho amesema ni kweli matokeo ya uchaguzi katika jimbo la Saxony yalikuwa magumu.

''Kwanza ni matokeo magumu na ambayo yanaonesha dhahiri kwamba juu ya yote pia yalistahili kwa Michael Kretzschmer. Amefanikiwa kuweka wazi kwamba kuna upande mwingine zaidi ya wenye siasa kali-upande ulio rafiki,na wenye uwazi,na wenye mtazamo wa kusonga mbele kwa jimbo la Saxony''

Landtagswahl in Sachsen 2019 | Jörg Urban & Jörg Meuthen, AfD
Mgombea wa AfD -jimbo la Saxony Joerg Urban akipongezwa Picha: Reuters/W. Rattay

Chama cha CDU kilipata asilimia 32.1 ya kura dhidi ya Afd kilichopata asilimia 27.5.Chama cha kijani kiko katika nafasi kubwa ya kushirikiana na CDU chaguo ambalo kura za maoni zinaonesha ndilo pekee linaloonekana huenda likawepo kitaifa ikiwa unafanyika uchaguzi mkuu. Katika jimbo la Brandenburg Afd kiliondoka na asilimia 23.5 kikishindwa na SPD kilichochukua asilimia 26.2.Chama cha FDP huenda kikashindwa kuingia bungeni kufuatia matokeo mabaya kabisa.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Iddi Ssessanga