1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi wa Ujerumani

Sylvia Mwehozi
15 Septemba 2017

Wananchi wa Ujerumani wataelekea katika sanduku la kupigia kura katika uchaguzi mkuu Septemba 24 mwaka huu. Ukiacha chama cha CDU na kile cha SPD, vipo vyama vidogo vinavyoweza kuamua juu ya uwiano wa madaraka.

https://p.dw.com/p/2k3rD
Deutschland Wahlplakate Schulz Merkel
Picha: picture-alliance/F. May

Utafiti wa maoni unaonesha chama cha kihafidhina cha Kansela Angela Merkel kinaongoza kwa tarakimu mbili dhidi ya wapinzani wake wa karibu, Wasocial Democrats. Lakini kinyang'anyiro hicho katika nafasi ya tatu kipo wazi na katika mfumo wa Muungano wa hapa Ujerumani, vyama vidogo vinaweza kuamua juu ya uwiano wa madaraka. Vyama vinavyotarajiwa kujipatia asilimia 5 ili kungia bungeni. 

CDU

Chama cha Christian Democratic Union CDU kilianzishwa baada ya kumalizika vita ya pili ya dunia, ndicho chama kikuu cha kihafidhina kilicho maarufu na chenye wasomi wa kati na wataalamu.

Chini ya Merkel CDU imejisogeza kati kwa kukumbatia sera za mrengo wa kushoto kama vile kuhitimisha uandikishaji jeshini kwa mujibu wa sheria, kuondoa mitambo ya nyuklia na kufungua mipaka yake kwa ajili ya wakimbizi.

Chama hicho kimeonyesha utiifu thabiti kwa Merkel kwani amekaa madarakni miaka 12 lakini hakuna mrithi wake wa wazi na wakosoaji wanakilaumu kwa kushindwa kumuandaa mrithi wa baadae.

CSU

Christian Social Union ni chama dada cha kihafidhina kwa CDU, kikipatikana katika jimbo la kitajiri, na lililosheheni utamaduni la Bavaria.  Kiongozi wake Horst Seehofer alikuwa ni mkosoaji mkubwa wa uamuzi wa Merkel wa kuwachukua mamia ya waomba hifadhi mwaka 2015. CSU inafungamana na CDU katika ngazi ya kitaifa. Kwa pamoja vimekuwa vikiongoza katika serikali nyingi za Ujerumani baada ya vita.

SPD

Conflict Zone - The Debate
Picha: DW/M. Altmann

Hiki ni chama kikongwe hapa Ujerumani takribani kina umri wa karibu miaka 150 na wanachama wake ni tabaka la wafanyakazi na vyama vikuu vya wafanyakazi vyenye nguvu. Wafuasi wake walikishutumu kwa usaliti baada ya serikali iliyokuwa ikiongozwa na SPD kulazimisha mageuzi ya sharia za kazi kuanzia mwanzo wa karne. Mageuzi hayo yanatajwa kuwa yalisaidia kukuza uchumi wa Ujerumani. SPD imejitahidi kushamiri kama mshirika mdogo katika muungano mkubwa wa serikali ya Merkel katika miaka mine iliyopita, licha ya kusukuma suala la kima cha chini cha mshahara, ndoa za jinsia moja na hatua zaidi za usawa mahali pa kazi. Matumaini kwamba kiongozi wake,  Martin Schulz anaweza kugeuza kibao na kumuondoa Merkel kama Kansela yameonekana kufifia kutokana na upungufu wake katika kura za maoni.

FDP

Conflict Zone - The Debate
Picha: DW/M. Altmann

Free Democartic Party ni chama kinachounga mkono biashara, yaani  kinasimamia misingi ya kiliberali, kinahamasisha ubepari wa soko huria na uhuru binafsi. Kimetumia muda mwingi serikalini kuliko chama kingine chochote, mara zote ni mshirika mdogo wa aidha CDU/CSU au SPD.

Lakini baada ya kukosekana kwa ushawishi katika kivuli cha serikali inayoongoza ya Merkel, kilipata aibu ya kuondolewa bungeni katika uchaguzi ulipita. FDP sasa inamatumaini ya kurejea ulingoni chini ya kiongozi kijana Christian Lindner, ingawa wakosoaji wanasema jukwaa la chama hicho haiko wazi.

Chama cha Kijani-The Greens

Conflict Zone - The Debate
Picha: DW/M. Altmann

Chama hiki mizizi yake ya kupinga vita imeanzia mwaka 1970. Pia kinasimamia harakati za kupambana na nyuklia na kimeongoza uhamisishaji wa haki za watu wa jinsia moja na kuondokana na nguvu za nyukilia. Kwa hivi sasa kwa mujibu wa utafiti wa maoni kinasimamia katika tarakimu moja, baadhi ya wakosoaji wanatabiri kwamba chama hicho kitapaswa kuchagua kusalia katika upinzani au kufungamana na serikali inayoongozwa na Merkel ambayo pia inaweza kujumuisha chama cha FDP na kupewa jina la "Muungano wa Jamaica” kutokana na rangi za kila chama.

Die Linke

Conflict Zone - The Debate
Picha: DW/M. Altmann

Kilianzishwa na wakomonisti kutoka iliyokuwa Ujerumani Mashariki na waasi wa SPD, wapinga vita wenye mgongano mkali, wanaopinga ushirika. Chama hiki cha Die Linke chenye siasa kali za mrengo wa kushoto ndicho chama kikuu cha upinzani hapa Ujerumani. Pamoja na kufanikiwa kuingia katika serikali kadhaa za kikanda, matakwa yake makubwa ni kuvunjwa kwa NATO na Ujerumani kuacha kupeleka wanajeshi wake nje ya nchi, maana yake ni kwamba ni mshirika asiyewezekana katika ngazi ya kitaifa.

AfD

Conflict Zone - The Debate
Picha: DW/M. Altmann

The Alternative for Germany, ama chama mbadala kwa Ujerumani kilianza harakati zake 2013 kwa kupinga kuongeza nguvu za Umoja wa Ulaya kabla ya kuingia katika kuupinga Uislamu na wahamiaji. Baada ya kuonyesha hasira juu ya suala la utitiri wa wakimbizi la Merkel, chama hicho cha siasa za mrengo wa kulia cha kizalendo kilishinda viti 13 katika mabunge ya majimbo 16 ya Ujerumani.

Lakini kuendelea kupigana kusikokuwa na mwisho na kushuka kwa hivi karibuni kwa waomba hifadhi kumedhoofisha uungaji mkono wa chama hicho. Hata hivyo, kinasalia katika nafasi ya kuingia bunge la kitaifa kwa mara ya kwanza. Kikifunikwa na vyama vingine AfD kitakwenda moja kwa moja katika benchi la upinzani.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef