1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vyombo vya habari na malengo ya millenia

Maja Dreyer4 Septemba 2007

Ni miaka saba na nusu iliyopita pale nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zilipopitisha malengo ya Millenia, malengo ya kimaendeleo yanayoweka viwango fulani katika maeneo mbalimbali ya kijamii na kiuchumi ambavyo vinataka kufikiwa hadi mwaka 2015. Mpaka mwaka huu, nusu ya muda uliokubaliwa umepita na wakati umewadia kuangalia juhudi zimefikia wapi na vipi kuendelea.

https://p.dw.com/p/CHjR
Waandishi wa habari wana jukumu pia kuhusiana na maendeleo
Waandishi wa habari wana jukumu pia kuhusiana na maendeleoPicha: DW

Vyombo vya habari pia vinabeba dhamana kusaidia malengo haya yafikiwe – suala hilo limezungumziwa kwenye mkutano maalum wa kimataifa unaofanyika mjini Bonn tangu mwanzoni mwa wiki hii. Maja Dreyer ana ripoti kamili.

"Mengi yanazunguziwa lakini kweli hatua zinachukuliwa – sijui!" Ni maneno kutoka kwenye filamu iliyoonyeshwa katika kufungua rasmi mkutano wa vyombo vya habari mjini Bonn. Maneno haya yanasema kwa ufupi yale ambayo watu wengi ulimwenguni wanayafikiri. Juu ya hayo, bado malengo ya millenia hayajafikia umaarufu mkubwa kama wanafunzi wa idara ya masomo ya Deutsche Welle walivyogundua katika kura ya maoni duniani kote.

Hizo ndizo sababu kwa nini inabidi kuzungumzia kwa kina mpango huu wa kimaendeleo. Haya aliyasisitiza mkuu wa Deutsche Welle, Erik Bettermann: “Tukiangalia kiwango cha maendeleo duniani tunaweza kuona kuwa demokrasia inahitaji kuwa na msingi wa maadili, yaani uhuru wa maoni na vyombo vya habari. Bila ya hiyo, utaratibu wa maendeleo ni mgumu sana. Tukitaka kupunguza umaskini kwa nusu hadi mwaka 2015 inabidi kuwa na msingi kama huu. Tupambane basi na changamoto hiyo kwa jamii na vyombo vya habari.”

Maswali yanayojadiliwa ni vipi vyombo vya habari vinaweza kuchangia ili malengo ya millenia yafikiwe. Au: vyombo vya habari vyenye uhuru vina dhamana gani katika kupunguza umaskini, idadi ya akinamama na watoto wanaofariki wakati wa uzazi au kupunguza idadi ya watu wanaoambukizwa ukimwi na Malaria?

Bi Eveline Herfkens ambaye aliwahi kuwa waziri wa mambo ya maendeleo wa Uholanzi na sasa ni mratibu wa kampeni juu ya malengo ya millenia, naye anasema waandishi wa habari wanahitajika katika kupigia debe utekelezaji wa malengo ya millenia, kwa sababu: “Kama katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon na Kofi Annan aliyemtangulia walivyosema mara nyingi pale walipozungumzia malengo ya millenia: Kinachokosekana ni nia ya kisiasa. Umoja wa Mataifa peke yake hauwezi kutekeleza malengo haya. Ni kama jukwaa ambapo wanasiasa wanaweza kutoa hotuba nzuri, ahadi nyingi na kutia saini makubaliano. Lakini hatuwezi kuzilamizisha serikali hizo nyingi kuchukua hatua barabara ikiwa zinakwama katika siasa za kila siku.”

Kwa hivyo, Bi Herfkens alitoa mwito kwa waandishi wa habari kushirikiana na kuwalaumu hadharani wahusika, si tu katika nchi zinazoendelea bali pia katika nchi wafadhili ili watekeleze ahadi zao. Amesema: “Wakati umefika tulishughulikie suala hili vizuri. Lazima tuwe na hakika kwamba ujumbe huu umefahamika, yaani sisi ni kizazi cha kwanza katika historia ya wanadamu ambacho kina uwezo wa kifedha, kiujuzi na kisiasa kuondosha umaskini mkali. Tusikose fursa yetu hiyo .”