1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waafrika Kusini wamaliza kumuaga Mandela

Oumilkher Hamidou13 Desemba 2013

Milolongo isiyomalizika ya watu waliojaa huzuni na fahari wanaendelea kupita mbele ya jeneza lililofunikwa nusu, la shujaa wao wa taifa Nelson Mandela na kumpa hishma zao za mwisho .

https://p.dw.com/p/1AYlI
Jeneza la Nelson Mandela limewekwa katika ukumbi wa Union BuildingsPicha: Reuters

Milolongo isiyomalizika ya watu waliojaa huzuni na fahari wanaendelea kwa siku ya tatu Umati wa watu wanapiga foleni tangu alfajiri huko Pretoria wakitaraji kumpa hishma za mwisho shujaa wao Nelson Mandela kabla ya maiti yake kusafirishwa hadi katika kijiji alikozaliwa ambako ndiko atakakozikwa jumapili ijayo.

"Kumuona kwa mara ya mwisho,ni jambo linalonituliza moyo" anasema Tieho Motspal,anaepiga foleni pamoja na mkewe tangu saa sabaa za usiku wa jana kuamkia leo.

"Tutakapomuona rais wetu tu,tutarejea nyumbani,katika mji mdogo wa Frankfurt, saa tatu kwa gari kutoka Pretoria, anasema Tieho Motspal akizungukwa na maelfu ya wengine, wanaosubiri kupita mbele ya jeneza la shujaa wao.

Jana jioni maafisa wa serikali waliifunga milango ya ikulu-Union Buildings,ambako maiti ya Nelson Mandela imewekwa,katika wakati ambapo maelfu walikuwa bado wamepiga foleni kusubiri kuingia.

Baadhi ikiwa ni pamoja na Stanley Luvhimbe aliyesafiri masafa ya kilomita 450 hadi Pretoria wakaamua kulala nje kususbiri hadi leo:"Ni fursa pekee.-hatutomuona tena" anasema.

Leo ni Siku ya Mwisho

Wengine wamekuja leo kubahatisha kama watafanikiwa kumuona,mfano wa Ompelege Majafa mwenye umri wa miaka 27 aliyesafiri kwa muda wa saa tatu usiku kucha."Ni tukio ambalo kamwe hatutolisahau" anasema.

Nelson Mandela Abschied 13.12.2013
Waafrika kusini bila ya kujali kabila wala dini wanamlilia shujaa waoPicha: Reuters

Kila asubuhi na kwa muda wa siku tatu sasa,maiti ya bingwa wa mapambano dhidi ya mfumo wa ubaguzi wa rangi na mtengano Apartheid ,rais wa kwanza mweusi wa Afrika kusini,inatolewa katika hospitali ya kijeshi ya Pretoria na kuletwa katika ikulu ya Union Buildings.

Jeneza lake likiwa ndani ya gari na kufuatiwa na mlolongo wa magari mengine na pikipiki za serikali huzunguka barabara za mji mkuu ambako wananchi wanasimama njiani wakipepea bendera kumpa hishma na kumuwaga baba wa taifa.

"Watu wana huzuni lakini siamini mie kama wanahisi mustakbal wao hautakuwa mwema.Nnahisi tuna mengi ya maana yanayotufanya tuamini tutakuwa na mustakbal mwema.Na hata kama tumempoteza mbabe shujaa wetu,naamini kuna mambo mengi mazuri yanayotoa matumaini mema. Afrika ya Kusini tumejifunza na tunajifunza kutoka kwa Nelson Mandela na kila mmoja anajiuliza atachangia vipi kuyafanya mambo yawe bora."

Maiti ya Nelson Mandela itasafirishwa kwa ndege kesho alfajiri hadi katika kijiji alikozaliwa cha Qunu alikousia mwenyewe ndiko anakotaka akazikwe.

Kamera na Wageni Hawatoruhusiwa

Mazishi rasmi ya jumapili yatahudhuriwa na watu kama elfu tano hivi wakiwemo pia viongozi mashuhuri wa kimataifa ikiwa ni pamoja na mwanamfalme Charles wa Uingereza.

Angela Merkel Kondolenz Buch Nelson Mandela
Kansela Angela Merkel aandika katika daftari la rambi rambi katika ubalozi wa Afrika kusini mjini BerlinPicha: Reuters

"Kamera hazitaruhusiwa wakati wa mazishi, familia haitaki watu waone maiti itakapoteremshwa kaburini," amesema msemaji wa serikali Phumla William. Vyombo vya habari na wageni wa hishma hawatoweza kuhudhuria, amesisitiza.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/

Mhariri: Mohammed Khelef